Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye (Mb.) amewaahidi
wakazi wa Kisiwa cha Mafia kuwa Serikali imejipanga kuboresha
mawasiliano katika vijiji vitatu vyenye usikivu hafifu wa mawasiliano ya
simu za mkononi.
Akizungumza
na wananchi wa vijiji vya Miburani, Chunguruma na Banja kisiwani Mafia
wakati wa ziara ya kukagua usikivu wa mawasiliano ya simu za mkononi,
alisema anatambua na amethibitisha kuwa wananchi wa vijiji hivyo
wanapata usikivu hafifu na kuahidi kuwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa
Wote (UCSAF) Serikali itaboresha mawasiliano hayo katika kipindi cha
miezi saba kuanzia mwezi huu wa Aprili.
Nditiye
amesema hayo katika ziara ya kukagua usikivu wa mawasiliano na masuala
ya Uchukuzi akiwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano mwenye dhamana ya Sekta ya Mawasiliano Dkt. Jim
Yonazi, Mbunge wa Mafia Mbaraka Dau (Mb.) pamoja na Mtendaji Mkuu wa
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Injinia Peter Ulanga.
“Nawaomba
muwe na subira, serikali inalitambua hili na Mfuko wa Mawasiliano kwa
Wote utahakikisha kuwa mawasiliano yanakuwa bora na yenye usikivu wa
kutosha,” aliahidi Nditiye.
Pamoja
na kukagua usikivu wa Mawasiliano katika kisiwa cha Mafia, Nditiye pia
alikagua uwanja wa ndege wa Mafia na kumuagiza Meneja wa Uwanja huo
kupeleka mara moja makao makuu mahitaji ya kuboresha uwanja huo ili
kuhakikisha unafanya kazi kwa viwango vinavyohitajika kwa ajili ya
usalama wa usafiri wa anga kisiwani humo.
Vilevile
Nditiye alifanya ukaguzi katika gati ya Kilindoni na kuagiza
matengenezo ya mbao za gati hiyo zifanyiwe ukarabati na matengenezo
mengine muhimu mara moja kuanzia wiki hii na taarifa za kukamilika kwa
marekebisho hayo zipelekwe Wizarani mara matengenezo yatakapokamilika.
Pia
Nditiye alizungumza nawananchi wa Mafia na kupokea kero za wananchi
kuhusu masuala ya usafiri hususani barabara na vivuko. Akizungumzia
suala la kivuko, alisema kivuko kipya kimeanza kutengenezwa na
kinategemewa kukamilika hivi karibuni. Hali kadhalika aliwaambia
wananchi kuwa wakati kivuko kipya kinatengenezwa, kivuko kilichopo Chuo
cha Mabaharia Tanzania kitaanza kuhudumia wananchi katika kipindi cha
mwezi mmoja kwa ajili ya usafiri kati ya Jiji la Dar es Salaam,
Kilindoni, Mafuya na Nyamisati Kibiti.
Nditiye
alimshukuru sana Mbunge wa Mafia Dau kwa kuwa mstari wa mbele kusimamia
maendeleo ya Mafia katika maeneo yote ya Uchukuzi na Mawasiliano na
aliahidi Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John
Pombe Magufuli inafanya kila linalowezekana kuhakikisha maeneo yote ya
Tanzania yanafikika kwa usafiri na mawasiliano.
Aidha
aliwaeleza wananchi wa Mafia kuwa ujenzi wa gati la Nyamisati limefikia
asilimia 88 na inatarajiwa litakamilika hivi karibuni na kuondoa kero
za wananchi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakipata shida ya usafiri katika
Kisiwa cha Mafia.
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye (wa 4 kutoka kulia)
akikagua mbao za Gati la Kilindoni Wilayani Mafia.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Jim
Yonazi akisalimia wananchi wa Mafia wakati wa mkutano wa Naibu Waziri
Uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye kusikiliza kero za wananchi wa
Wilaya hiyo kuhusu masuala ya usafiri na mawasiliano.
No comments:
Post a Comment