Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaangalia uwezekano ili
viongozi wa ngazi mbalimbali wapate mafunzo ya uongozi na maadili
kwenye Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kama sehemu ya kurejesha
maadili kwa viongozi.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 11, 2019) wakati akifungua
kongamano la Kumbukizi ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere lililofanyika kwenye chuo hicho, Kigamboni, jijini
Dar es Salaam.
Amesema Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi wa Halmashauri, Manispaa, Miji na Wakuu wa taasisi
mbalimbali za umma wanastahili kupelekwa kwenye chuo hicho ili wapigwe
msasa juu ya maadili ya uongozi.
“Kwa viongozi wetu wote kuanzia Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa
Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurgenzi wa Halmashauri na Wakuu wa taasisi
mbalimbali za umma ambao wanatakiwa kujengewa msingi imara wa namna ya
kuongoza, hapa ndiyo mahali pake. Nalichukua ombi lenu ili tuwape
fursa ya wiki moja au mbili waje hapa wajifunze miiko ya uongozi,”
amesema.
“Wanatakiwa waje kupata namna ya kuwa kiongozi, miiko ya namna
kiongozi anavyotakiwa awe. Unapokuwa kiongozi unatakiwa ujue mambo
gani unapaswa uyaache. Unapokuwa kiongozi kuna baadhi ya mambo
unatakiwa uyaache. Hata kama ulikuwa umezoea kushangilia mpira kwa
kuvua shati, ukiwa kiongozi unaacha kuvua shati.”
Amesema kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia hakuna namna ya kukwepa
kujifunza na kupata maarifa mapya huku akinukuu maneno ya Baba wa
Taifa, Mwl. Julius K. Nyerere ambaye aliwahi kusema: “…Watu walio
hatari sana ni wale ambao wanafikiri kuwa wanajua kila kitu, wala
hawana haja kujifunza zaidi. Hii ni tabia mbaya ambayo huzuia kabisa
maendeleo.”
“Napenda kuwahakikishia kuwa nimepokea changamoto hii ya msingi na
tutazama namna nzuri ya kuwezesha viongozi katika ngazi mbalimbali
waje kupata mafunzo ya uongozi katika chuo hiki.”
Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na Mkuu wa Chuo hicho,
Prof. Shadrack Mwakalila kwamba mwitikio wa viongozi na watendaji
wakuu wa Serikali kushiriki katika mafunzo ya uongozi, maadili na
utawala bora umekuwa hafifu licha ya jitihada kubwa za kutangaza
mafunzo haya kupitia njia mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ombi lililotolewa
na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Mzee
Stephen Wassira la kutaka chuo hicho kipandishwe hadhi na kuwa chuo
kikuu ni jambo linalowezekana kwa sababu waziri mwenye dhamana ya
elimu ya juu nchini alikuwepo na amesikia ombi lao.
“Mwelekeo wa chuo ndiyo unaotiliwa mkazo na Serikali hii, jina lenyewe
la chuo ni tunu. Kama Tanzania tuna chuo chenye jina la Waziri Mkuu,
tutashindwaje kutoa jina kwa muasisi wa nchi yetu? Mheshimiwa Waziri
uko hapa, libebe suala hilo na ulifuatilie.”
Mapema, Mzee Wassira alitoa maombi matatu la kwanza likiwa ni kutaka
chuo hicho kipewe hadhi ya kuwa chuo kikuu na jina lake libadilishwe
na kuwa Mwalimu Nyerere Memorial Leadership University. Pia aliomba
mazingira ya chuo yabadilishwe ili yalingane na hadhi ya mwenye jina.
Pia Mzee Wassira aliomba Serikali ikitumie chuo hicho kuendeleza kazi
iliyokuwa ikifanywa na chuo cha Kivukoni ya kuwaandaa viongozi kwa
kuwapa mafunzo juu ya maadili ya uongozi na kuongeza kuwa wakipata
mafunzo ya wiki moja au mbili ni lazima watabadili mitazamo yao.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na balozi wa Namibia hapa nchini Bibi
Theresia Samaria, balozi wa Msumbiji hapa nchini Bibi Monica Patricio
Clemente, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye
alikuwa mwenyekiti wa kongamano hilo. Wengine ni mawaziri wastaafu wa
Serikali ya awamu ya kwanza, Mzee Ibrahim Kaduma, na Mama Thabitha
Siwale. Wengine ni Mzee Wilson Mukama na Bw. John Shibuda.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, wakati alipo
wasili kufungua kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere
Aprili 11, 2019, katika Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar
es Salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha
kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen Wasira wakati alipo wasili kwenye
ufunguzi wa kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere
Aprili 11, 2019, Kigamboni jijini Dar es Salaam. Tokea kushoto ni Mkuu
wa Chuo hicho, Profesa Shadrack Mwakalila, Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph
Warioba, kwenye ufunguzi wa kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya
Mwalimu Nyerere Aprili 11, 2019, katika Chuo cha Mwalimu Nyerere,
Kigamboni jijini Dar es Salaam. Katikati ni Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akitoka kwenye jengo la Utawala la Chuo cha
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam, kabla ya
kufungua kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere Aprili
11, 2019. Kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha
kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen Wasira, kwenye ufunguzi wa
kongamano la maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere yaliyofanyika
katika Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam Aprili
11, 2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia, kwenye ufunguzi wa kongamano la
maadhimisho ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Chuo
cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam Aprili 11, 2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la maadhimisho ya
kumbukizi ya Mwalimu Nyerere yaliyofanyika katika Chuo cha Mwalimu
Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam Aprili 11, 2019.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen
Wasira akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la maadhimisho ya
kumbukizi ya Mwalimu Nyerere yaliyofanyika katika Chuo cha Mwalimu
Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam Aprili 11, 2019.
No comments:
Post a Comment