Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amempongeza mwakilishi wa Shirika la Umoja wa
Mataifa la Watoto (UNICEF) kwa kazi kubwa iliyofanywa na Shirika hilo
hapa nchini.
Ametoa pongezi hizo leo (Alhamisi, Aprili 11, 2019) alipokutana na
mwakilishi wa UNICEF, Bibi Maniza Zaman ofisini kwake Magogoni, jijini
Dar es Salaam.
Waziri
Mkuu amempongeza Bibi Zaman kwa upendo mkubwa aliouonesha kwa watoto wa
Tanzania hasa katika kusimamia masuala ya afya, elimu na haki za watoto
wa kike. “Tumenufaika na mengi kutoka UNICEF wakati ukiwa hapa hasa
kwenye masuala ya haki za watoto,” amesema na kuongeza:
“Utendaji
wako wa kazi katika nyanja hizi uliwezesha tufanye kazi kwa utulivu kwa
sababu ulikuwa ukisukuma mambo mengi, kwenye maeneo mbalimbali hapa
nchini. Tunasikitika kwamba utaondoka hivi karibuni lakini tunakutakia
heri na maisha mema huko uendako Kenya.”
Kwa
upande wake, Bibi Zaman ambaye amekaa hapa nchini kwa miaka mitatu na
miezi minne, amesema anaishukuru Serikali kwa ushirikiano iliompatia kwa
kipindi chote alichokuwa hapa nchini. “Ninaona siku zimeisha haraka
sana, lakini ninashukuru viongozi mbalimbali kwa ushirikiano
walionipatia,” amesema.
Amesema
katika kipindi chote hicho, ameshirikiana vizuri na Ofisi ya Waziri
Mkuu, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, na wizara nyingine tano za kisekta ambazo
amekuwa akifanya nazo kazi kwenye masuala ya watoto.
Bibi Zaman amesema jambo kubwa la kujivunia ni mafanikio yaliyopatikana
kwenye kazi ya kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye
umri usiozidi miaka mitano ambayo ilifanyika kwa kushirikiana na Wakala
wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).
“Tuliweza
kuunda mfumo rahisi wa kusajili watoto wenye umri chini ya miaka mitano
ambao iliwasaidia kupata vyeti ndani ya siku moja na tumeweza kuifikia
mikoa 13 ambayo ni nusu ya mikoa yote hapa nchini. Kazi hii imewezesha
watoto milioni 3.5 wapate vyeti vya kuzaliwa na kuongeza kiwango cha
watoto wenye vyeti hivyo, iongezeke kutoka asilimia 13 hadi kufikia
asilimia 38 katika kipindi cha miaka minne na nusu,” amesema.
Ameitaja
mikoa hiyo kuwa ni Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Mwanza, Lindi na
Geita. Mingine ni Shinyanga, Mara, Simiyu, Mtwara, Dodoma na Singida.
Amesema ana imani kuwa kwa mikoa iliyobakia, kazi hiyo itakamilika pindi
fedha zitakapopatikana.
Pia amepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kupunguza tatizo
la utapiamlo. Maeneo mengine ambayo wamefanyia kazi ni elimu na afya.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwakilishi wa UNICEF Tanzania
Maniza Sultan Zaman, walipokutana kwa mazungumzo, ofisini kwa Waziri
Mkuu, Magogoni, jijini Dar es Salaam Aprili 11, 2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Mwakilishi wa UNICEF Tanzania
Maniza Sultan Zaman, ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni, jijini Dar es
Salaam Aprili 11, 2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akioneshwa picha ya watoto na
Mwakilishi wa UNICEF Tanzania Maniza Sultan Zaman, baada ya mazungumzo
yao, ofisini Magogoni, jijini Dar es Salaam Aprili 11, 2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment