Baraza la Mawaziri la
Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), limeridhia usafirishaji wa bidhaa
muhimu katika ukanda huo wakati wa janga
la homa ya mapafu (Covid-19) ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kwa nchi
wanachama.
Akizungumza katika
Mkutano wa dharura wa Maafisa Waandamizi wa SADC, kuhusu Covid-19, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC na
Waziri wa Mambo ya Nje kutoka Tanzania, Prof.Palamagamba kabudi alisema kuwa Baraza
limepitisha mapendekezo ya Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Afya uliofanyika
Machi 9, 2020, Dar es Salaam, Tanzania.
“Mkutano wa Dharura wa
Mawaziri wa Afya wa tarehe 9, Machi 2020, ulitoa mapendekezo ambayo yamefanyiwa
kazi na Mkutano wa Baraza la Mawaziri yakiwa ni
ufuatiliaji na utekelezaji
masuala ya afya kuhusu mlipuko wa Covid-19, kujadili namna ya kujiandaa na
kukabiliana na virusi vya Covid -19,kubaini wagonjwa na kufuatilia waliokutana
nao na huduma za tiba katika ukanda wetu” Alisema Prof. Kabudi.
Alisema masuala mengine
ni uchunguzi na upimaji wa kimaabara, uzuiaji na udhibiti wa maambukizi,
uelimishaji wa madhara na ushirikishaji wa jamii, uratibu wa kikanda wa
kukabiliana na Covid-19, uwezeshaji na usafirishaji wa bidhaa muhimu katika
ukanda huo wa SADC wakati huu wa Covid-19.
Mengine yaliyopitishwa
ni Covid-19 na uwezeshaji wa biashara, Covid-19 na masuala ya udhibiti biashara
na usimamizi wa majanga hatarishi katika ukanda huo wa Nchi za Kusini mwa
Afrika, mapendekezo hayo yanatokana na ukweli kwamba Covid-19 imeendelea kusambaa duniani kwa hiyo Jumuiya ikaona iweke
mikakati madhubuti kukabiliana na ugonjwa huo.
Na.Paschal
Dotto-MAELEZO.
“Mkutano huu wa Baraza la Mawaziri SADC uliitishwa kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa maambukizi na vifo katika baadhi ya nchi Duniani, kwa mujibu wa taarifa namba 76 ya Shirika la Afya Duniani(WHO), ya April 5, 2020 inaeleza kuwa takribani watu 1,133,759 wameambukizwa ugonjwa huo na kati ya hao matukio mapya ni 82,061 na vifo 62,784 huku Afrika kwa nchi 51 kuna wagonjwa 9,198 na vifo viko chini ya watu 500, lakini kwa ukanda wetu wa SADC kuna matukio 2,127 katika nchi 14 huku vifo vikiwa 38” Alisema Prof.Kabudi.
Aidha, Prof. Kabudi
alieleza kuwa Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri uliofanyika sambamba na
Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa SADC ulilenga katika kupokea taarifa ya wataalamu
pamoja na muongozo wa urazinishaji na uwezeshaji usafirishaji wa bidhaa muhimu
na huduma katika nchi za SADC wakati huu wa mlipuko wa Covid-19.
Bidhaa zilizopitishwa
kwenye muongozo ni pamoja na usafirishaji wa vyakula, vifaa tiba, Dawa na vifaa
vya kujinga na Corona, mafuta na mkaa wa mawe, pembejeo za kilimo na madawa,
vifungashio, bidhaa zote zinazotumika katika utengenezaji, uchakataji na
uhifadhi wa vyakula na vifaa ambavyo vinahusu usalama na dharura kwenye majanga
mbalimbali.
Prof. Kabudi aliongeza
kuwa SADC wamefanya hivyo ili kuzuia kuenea kwa Covid-19 na kuwezesha utekelezaji mikakati ya kitaifa ya kupambana na ugonjwa
huo na kuwezesha upatikana wa bidhaa muhimu ili kuzuia usafirishaji usio wa
lazima kwa abirika katika ukanda huo wa Afrika .
No comments:
Post a Comment