Matokeo chanyA+ online




Monday, June 30, 2025

VIJANA WALIOACHANA NA DAWA ZA KULEVYA WAIPONGEZA DCEA

Baadhi ya vijana waliowahi kuwa watumiaji wa dawa za kulevya wameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa juhudi zake thabiti katika kupambana na biashara na matumizi ya dawa hizo. Vijana hao Pendo Athuman, Tonny Michael na Gabriel Nyangasi wamesema kuwa hatua zilizochukuliwa na mamlaka hiyo, ikiwemo kuziba mianya ya usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya, zimechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa upatikanaji wa dawa hizo mitaani, jambo ambalo limekuwa msaada mkubwa kwao na kwa wengine walioko katika safari ya kuachana na uraibu huo.

Wameeleza kuwa kwa sasa DCEA haijajikita tu katika ukamataji, bali pia inawekeza kikamilifu katika kutoa elimu ya kinga pamoja na huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya, jambo walilolieleza kuwa ni la kupongezwa kwani linagusa maisha ya moja kwa moja ya vijana wengi waliokuwa hatarini.

Aidha, wamepongeza juhudi za Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mahakama kwa kusimamia sheria na kutoa hukumu stahiki kwa wote wanaobainika kushiriki katika biashara ya dawa za kulevya, wakisema hatua hizo zinaongeza hofu kwa wahusika na kulinda kizazi cha sasa na baadaye.

Kauli mbiu: "Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya"

#DCEA
#OktobaTunatiki

Sunday, June 29, 2025

USHIKIANO BAINA YA DCEA NA TAASISI NYINGINE KATIKA KUKABILIANA NA DAWA ZA KULEVYA NDIO SIRI YA MAFANIKIO

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeendelea kutumia mkakati madhubuti wa nguzo kuu nne katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini. Nguzo hizo ni: (i) Kupunguza upatikanaji wa dawa za kulevya; (ii) Kupunguza uhitaji wa matumizi ya dawa hizo; (iii) Kudhibiti madhara yatokanayo na matumizi; na (iv) Kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na kimataifa.

Kupitia mikakati hiyo, katika mwaka 2024 pekee, DCEA imefanikiwa kukamata jumla ya kilo 2,327,983.8 za dawa za kulevya, zikiwemo bangi, mirungi, heroin, cocaine, metamphetamine, hashish, dawa tiba zenye asili ya kulevya na skanka. Mafanikio haya yanatokana na operesheni maalum, doria, na mashirikiano baina ya vyombo vya ulinzi na usalama.

Kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, jumla ya mashauri 2,785 yaliwasilishwa mahakamani ambapo mashauri 2,021 yalishinda, sawa na asilimia 72 ya mafanikio. TAKUKURU nayo imekuwa kiungo muhimu kwa kuziba mianya ya rushwa katika mfumo wa udhibiti wa dawa hizo, wakati Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni za mara kwa mara na kampeni za uelimishaji kwa jamii.

Kwa ujumla, mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kulinda afya, usalama na ustawi wa Watanzania dhidi ya athari za dawa za kulevya.

Kauli mbiu: "Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya"

#DCEA
#OktobaTunatiki

MKEMIA MKUU WA SERIKALI NDIYE SHAHIDI MKUU WA KITAALAMU KATIKA KESI ZINAZOHUSISHA DAWA ZA KULEVYA

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imeendelea kuwa mhimili mkuu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini kwa kutoa ushahidi wa kitaalamu wa kisayansi unaotumika mahakamani kuhakikisha haki inatendeka. Kupitia maabara zake za kisasa, GCLA hupokea na kuchunguza sampuli zote za dawa za kulevya zinazokamatwa katika oparesheni mbalimbali zinazoendeshwa na DCEA ikishirikiana na Jeshi la Polisi, Uhamiaji na taasisi nyingine za usalama.

Mkemia Mkuu wa Serikali ndiye shahidi mkuu wa kitaalamu katika kesi nyingi zinazohusisha dawa za kulevya, ambapo hutumia ripoti za maabara kuthibitisha aina na kiwango cha kemikali zilizokamatwa, jambo ambalo huongeza uzito na uhalali wa ushahidi mbele ya vyombo vya sheria na mahakama. Ushahidi huu umesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza idadi ya mashauri yaliyomalizika kwa mafanikio dhidi ya wahalifu wa dawa za kulevya.

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika miundombinu, mitambo ya kisasa, vifaa vya maabara na rasilimali watu, hali ambayo imeongeza kasi na ufanisi wa uchunguzi wa sampuli za ushahidi.

Kauli mbiu: "Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya"

#DCEA
#OktobaTunatiki

Saturday, June 28, 2025

UHAMIAJI NA DCEA HUSHIRIKIANA KWA ULINZI WA MIPAKA NA VIPENYO VYA DAWA ZA KULEVYA


Idara ya Uhamiaji ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejikita kwa nguvu kubwa katika kuzuia mianya yote inayoweza kutumiwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya kuingia au kutoka nchini. Kwa kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Idara hii imeongeza ulinzi na ufuatiliaji katika mipaka ya nchi, viwanja vya ndege, bandari, vituo vya mabasi, na njia zote za nchi kavu zinazotumiwa na wasafiri.

Katika jitihada hizi, Uhamiaji hutekeleza ukaguzi wa kina kwa abiria, mizigo na nyaraka ili kuzuia watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya kuingia au kutoka nchini. Hatua hizi pia hujumuisha kuzuia utoaji wa hati za kusafiria kwa watuhumiwa na kuwazuia wanaojaribu kuingiza dawa hizo nchini. Lengo kuu ni kuhakikisha Tanzania inasalia kuwa nchi salama, isiyokuwa na nafasi kwa biashara haramu ya dawa za kulevya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonyesha msimamo thabiti dhidi ya dawa za kulevya, akisisitiza kuwa biashara hiyo haramu huathiri uchumi wa taifa kwa kuficha fedha nyingi ambazo zingesaidia kwenye maendeleo ya jamii.

Kupitia ushirikiano huu wa kimkakati kati ya Uhamiaji na DCEA, Tanzania inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha usalama wa raia na mustakabali wa taifa unalindwa kwa nguvu zote dhidi ya janga la dawa za kulevya.

Kauli mbiu: "Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya"

#DCEA
#OktobaTunatiki

ONA USHIRIKIANO MADHUBUTI WA JESHI LA POLISI NA DCEA KATIKA VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA

Katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa taifa salama na lenye watu wenye afya bora na maadili mema, Jeshi la Polisi limeimarisha ushirikiano wake na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika jitihada za kuzuia, kubaini na kutokomeza kabisa matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini.

Kupitia kitengo maalum cha Anti-Drugs Unit (ADU), Jeshi la Polisi limekuwa likishirikiana na DCEA katika oparesheni za kitaifa ambazo zinajumuisha ukamataji wa watuhumiwa, uteketezaji wa dawa haramu na upelelezi wa kina katika kanda zote zilizoundwa na mamlaka hiyo. Wakuu wa upelelezi wa makosa ya jinai pia wamepewa maelekezo maalum ya kushirikiana kwa karibu na DCEA ili kuhakikisha mtandao wa usambazaji wa dawa hizo unavunjwa kwa ukamilifu.

Aidha, Jeshi la Polisi limekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa jamii kwa kuonesha kwa uwazi sampuli za dawa hizo haramu ili wananchi wazitambue, waweze kutoa taarifa, na kuchukua tahadhari mapema. Dawa hizo ni pamoja na heroin, cocaine, bangi, mirungi, methamphetamine, nk

Ushirikiano huu madhubuti unalenga kujenga jamii inayotambua hatari za dawa za kulevya na kujiwekea kinga dhidi ya janga hili, huku serikali ikidhamiria kuacha historia mpya isiyo na nafasi kwa biashara na matumizi ya dawa hizo hatari.

Kauli mbiu: "Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya"

#DCEA
#OktobaTunatiki


Friday, June 27, 2025

ESTHER MORRIS WA NAWEZA TENA AONGOZA MAPINDUZI CHANYA KWA DADA POA NA WARAIBU WA DAWA ZA KULEVYA MWANZA

Mkurugenzi wa Shirika la Naweza Tena, Bi. Esther Morris, ameibuka kama sauti ya matumaini kwa wanawake waliokuwa wakijihusisha na biashara ya ukahaba na matumizi ya dawa za kulevya jijini Mwanza. Kupitia mradi wa kutoa Stadi za Maisha, shirika hilo limekuwa likiwasaidia Dada Poa na waraibu wa dawa za kulevya kuachana na maisha hatarishi na kuingia kwenye njia salama ya kujitegemea kiuchumi.

Bi. Morris amesema kuwa shirika hilo linawafuatilia kwa karibu walengwa wake, kuwafundisha maadili, kazi halali, na kuwajenga kisaikolojia ili waweze kurejea katika hali yao ya kawaida. Miongoni mwa miradi inayowasaidia ni pamoja na ajira katika kituo cha kuoshea magari, hatua inayowapa kipato halali na heshima mpya katika jamii.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika kinga na tiba dhidi ya dawa za kulevya. Esther amewataka wadau wote wenye nia ya kusaidia kundi hili kuwasiliana nao kupitia namba 0753 85 85 85, ili kwa pamoja kuendeleza mapinduzi haya ya matumaini.

Kauli mbiu: "Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya"

#DCEA
#OktobaTunatiki

MCH. HANANJA ATOA WITO WA KITAIFA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA - TUIMARISHE KINGA, TUOKOE MAISHA

Mchungaji Richard Jackson Hananja ametoa wito kwa jamii na Serikali kuendelea kushirikiana kwa dhati katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika hatua za kinga na tiba kwa waathirika. 

Pia, Mch. Hananja ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa kwa kuongeza bajeti ya tiba, ujenzi wa vituo vya afya ya akili na huduma za tiba mbadala kwa waraibu.

Aidha, ametoa wito kwa wazazi, viongozi wa dini, walimu na jamii nzima kushirikiana katika kutoa elimu ya mapema kwa vijana kuhusu madhara ya dawa hizo, akibainisha kuwa kinga ni silaha madhubuti kuliko tiba. “Hatupaswi kusubiri vijana wetu waanguke kwenye janga hili ndipo tuingilie kati elimu, maombi, na ufuatiliaji wa karibu ni njia muhimu ya kuzuia,” amesisitiza.

Mch. Hananja amehimiza ushirikiano baina ya taasisi za dini, mashirika ya kiraia na Serikali katika kuhakikisha Taifa linaibuka na kizazi salama, kisichoathirika na matumizi ya dawa za kulevya.

Kauli mbiu: "Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya"

#DCEA
#OktobaTunatiki