Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba katika
Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika hii leo Jijini Dodoma na
kusisitiza kuwa katazo la Mifuko ya Plastiki lililotolewa jana na Waziri
Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa linakuwa na nguvu kisheria kwa kuandika
kanuni za katazo ya mifuko ya plastiki zitakazotangazwa katika gazeti
la Serikali chini ya Sheria ya Mazingira na kutoa adhabu kwa kila mtu
atakaekiuka utaratibu uliowekwa.
“Kabla ya Serikali kutangaza hatua ya
kupiga marufuku mifuko ya plastiki, ulifanyika utafiti na maandalizi ya
mifuko mbadala. Uwezo wa kuzalisha upo na mifuko ya karatasi inayotumika
Kenya na Rwanda inatumia malighafi inayozalishwa
Mgololo-Iringa,Tanzania.” Makamba alisistiza
Waziri Makamba ameainisha kuwa kuna
vifungashio ambavyo havitapigwa marufuku ambavyo ni pamoja na
vifungashio vya dawa za hospitalini, vifungashio katika sekta ya kilimo
na ujenzi pia vile vya kuhifadhi maziwa na kutolea mfano wa vifungashio
vya maziwa ya ASAS na Tanga Fresh, hata hivyo utaratibu maalumu utawekwa
kwa wamiliki wa kukusanya vifungashio hivyo mara baada ya matumizi
yake.
Akizungumzia juu ya ushirikishwaji,
Waziri Makamba amesema kuwa zoezi hili limekuwa ni shirikishi na hatua
iliyotangazwa na Waziri Mkuu sio ya kushtukiza kwa kuwa Ofisi yake
iliratibu mikutano katika maeneo kadhaa nchini kusikiliza maoni ya
wananchi kuhusu zuio la mifuko ya plastiki.
Katika kukamilisha utekelezaji wa agizo
la Waziri Mkuu, Waziri Makamba amesema Ofisi yake imeunda kikosi kazi
cha kusimamia katazo hilo kikihusisha wajumbe kutoka Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Idara ya
Uhamiaji, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Shirika la Viwango Tanzania,
Mamlaka ya Chakula na Dawa, Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa
Serikali. Wengine ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Katika hatua nyingine Waziri Makamba
amesema kuwa mapema wiki ijayo ataitisha mkutano wa wawekezaji wa mifuko
mbadala kote nchini na kujadili kwa kina namna bora ya kuwekeza katika
uzalishaji wa mifuko mbadala rafiki wa mazingira.
Serikali imetangaza kuanzia Juni Mosi
2019 kuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya
plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote na matumizi yake.
No comments:
Post a Comment