Matokeo chanyA+ online




Wednesday, March 18, 2020

SERIKALI IMETOA PIKIPIKI 448 KWA MAAFISA TARAFA NCHINI

Serikali imegawa pikipiki 448 kwa maafisa tarafa  nchini ili kurahisisha utendaji kazi wao ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt John Magufuli aliyoitoa kwao mwaka jana.

Akikabidhi pikipiki hizo kwa baadhi ya wakuu wa mikoa Machi 18 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani  Jafo amesema pikipiki hizo zimegaiwa kwa mikoa 24 kutokana na mkoa wa Songwe na Pwani kuwa walishapewa.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akijaribu pikipiki mojawapo zilizotolewa kwa maafisa tarafa nchini.

Amesema  hatua hiyo itaondoa kero ya vitendea kazi na serikali imeendelea kuzipatia ufumbuzi kero zingine kadri mapato ya serikali yanavyoimarika.

"Tuna maafisa tarafa 570 lakini wengine walishapata pikipiki,Mhe Rais kupitia serikali Imempendeza kutoa sh bilioni moja kwa ajili ya kununua pikipiki hizi 448 hivyo kuondoa kero,niwatake maofisa tarafa  kutotumia pikipiki hizi kama kitega uchumi kwa kubeba abiria,"alisisitiza Waziri Jafo.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akimkabidhi ufunguo wa pikipiki Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge kwa ajili ya maafisa tarafa,pembeni yake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Kessy Maduka.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika amesema pikipiki hizo zitarahisisha utendaji kazi kwa Maofisa hao hususan kipindi cha Uchaguzi Mkuu.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akizungumza kabla ya kukabidhi pikipiki kwa maafisa tarafa nchini,pamoja nae yupo Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapteni George Mkuchika na naibu waziri wa wizara hiyo Marry Mwanjelwa.

"Nikushukuru Waziri kwa hatua hii,tunajua maafisa hawa ndio kiungo kikubwa cha utendaji kazi,wakati mwingine tunawatuma huku na kule walete taarifa hii na ile,hivyo kwa kutumia usafiri huu itakuwa rahisi kwao,"alisema Waziri Mkuchika.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akimkabidhi funguo wa pikipiki Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi kwa ajili ya maafisa tarafa nchini,wakuu hao wa mikoa wamepokea kwa niaba ya wakuu wa mikoa wengine.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi  na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta BIinilith Mahenge wameishukuru serikali kwa kutatua kero ya usafiri kwa Maofisa hao huku wakiahidi kutunza vyombo hivyo.

SAKINA ABDULMASOUD,DODOMA.

No comments:

Post a Comment