Matokeo chanyA+ online




Monday, April 6, 2020

MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERERE HAUJAWAHI KUSIMAMA – WAZIRI KALEMANI


Veronica Simba – Pwani
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amekagua Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kwa mara ya 11 tangu kuanza utekelezaji wake na kukiri kuridhishwa na maendeleo yake.
Hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), wakati Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) alipotembelea Mradi huo Aprili 5, 2020 kwa mara ya 11 tangu kuanza kutekelezwaji wake.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea sehemu mbalimbali za Mradi huo ulioko Rufiji mkoani Pwani, Aprili 5 mwaka huu, Dkt Kalemani amewataka Watanzania kuiamini Serikali na kuondoa hofu kuhusu ukamilikaji wake kwa wakati.
“Napenda niwatoe hofu Watanzania kuwa, Mradi huu haujawahi kusimama, hautasimama na utakamilika kwa wakati kama Serikali ilivyoahidi.”
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akisikiliza maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Mhandisi Steven Manda (wa pili kutoka kulia), kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mradi huo, Aprili 5, 2020.
Waziri alikuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi aliyetaka kufahamu kuhusu tetesi kutoka kwa baadhi ya watu kuwa huenda Mradi huo usikamilike kwa wakati.
Akieleza kwa kina kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mradi husika, Dkt Kalemani alibainisha kuwa kwa ujumla maendeleo ni mazuri kwani tathmini inaonesha kuwa kwa kazi za msingi, ujenzi umefikia asilimia 78.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Aprili 5 mwaka huu
Alifafanua kazi hizo kuwa ni pamoja na ujenzi wa njia ya kupokelea umeme (switch yard) ambayo hadi sasa Mkandarasi ametekeleza kulingana na mpango-kazi.
Nyingine ni ujenzi wa eneo ambalo maji yataingia kwa ajili ya kupelekwa kwenye mitambo (wáter in-take) ambalo nalo utekelezaji wake hadi sasa unaendana na mpango-kazi wa mkandarasi.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Aprili 5 mwaka huu
“Hata hivyo, katika eneo hili, kwenye kingo za maji kuna shida kidogo kwa sababu maji ni mengi, hivyo nimemwagiza Mkandarasi kuongeza kasi pindi maji yatakapopungua ili afidie muda na hivyo hali hiyo isiathiri ukamilishaji kazi husika kwa wakati uliopangwa,” alieleza Waziri.
Alielezea kazi nyingine aliyokagua kuwa ni eneo lililojengwa mitambo ya kusaga mawe kwa ajili ya kokoto za ujenzi ambapo alibainisha kuwa kazi husika imekamilika kwa asilimia 100.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Aprili 5 mwaka huu
Vilevile, Waziri alibainisha kuwa amekagua eneo ambako zitafungwa mashine tisa kwa ajili ya kufua umeme na kubaini kuwa kazi ya ujenzi katika eneo hilo hadi sasa imetekelezwa kwa kiasi kinachozidi kile kilichoainishwa katika mpango-kazi kwa siku takribani 30.
Aidha, Dkt Kalemani alikagua pia kituo cha Reli ya TAZARA cha Fuga ambacho ni maalumu kwa kushushia mitambo yenye uzito mkubwa inayotumika katika ujenzi wa Mradi. Akiwa eneo hilo, Waziri alishuhudia mizigo ikishushwa na kupelekwa eneo la Mradi.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Aprili 5 mwaka huu
“Naipongeza Serikali kwa kujenga Reli hii na kuweka Kituo rasmi kwa ajili ya kushusha mizigo ya Mradi huu. Hii inawezesha kazi za Mradi huu kuendelea kama kawaida pamoja na changamoto ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Hata hivyo, Waziri Kalemani alitoa wito kwa watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuijenga kwa kiwango cha lami, barabara kutoka kituo cha Reli cha Fuga hadi eneo la Mradi, umbali wa kilomita 35.8 ili iwe katika viwango bora zaidi kuwezesha usafirishaji wa mizigo mizito ya Mradi.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye shati la bluu) na Ujumbe wake, akiteremka kutoka katika Mashine maalumu ya kutengeneza kokoto zitakazotumika katika ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP). Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua maendeleo ya Mradi huo, Aprili 5, 2020
Waziri pia alikagua barabara zote zilizo ndani ya eneo la Mradi na kuthibitisha kuwa zinapitika vizuri. Alitoa wito kwa Mkandarasi kuendelea kukarabati maeneo korofi ya barabara hizo ikiwa ni pamoja na zile zilizo nje ya Mradi, hususan zilizo ndani ya wajibu wake ili ziendelee kutumika kusafirisha mizigo na wafanyakazi pasipo tatizo lolote.
Akizungumzia malipo kwa Mkandarasi, Dkt Kalemani aliipongeza Serikali kwa kulipa jumla ya shilingi trilioni 1.19 kati ya trilioni 6.5 za malipo yake yote, ambayo ni sawa na asilimia 18.8 huku akibainisha kuwa kiwango hicho ndicho stahili iliyopaswa kulipwa kufikia wakati huu, hivyo Mkandarasi hana kisingizio cha kutotekeleza majukumu yake.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Aprili 5 mwaka huu
Katika hatua nyingine, Waziri aliushukuru Uongozi wa Mikoa ya Morogoro na Pwani kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika usimamizi wa Mradi.
Hata hivyo alitoa wito kwa Mikoa inayohusika na vyanzo vya maji yatakayotumika katika Mradi huo, kuhakikisha kuwa pamoja na matumizi ya maji katika shughuli zao za kiuchumi lakini wananchi wake wanapaswa kuhakikisha matumizi hayo hayaathiri upatikanaji wa maji kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi.
Aliitaji mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Morogoro, Njombe, Iringa na Mbeya.
“Bwawa hili litakapokamilika litahitaji maji mengi kiasi cha mita za ujazo bilioni 32.3 hivyo nawasihi sana wananchi wa Mikoa husika kutoathiri upatikanaji wake,” alisisitiza Waziri.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye miwani) na Ujumbe wake, wakiangalia shehena ya nondo zenye uzito wa tani 2,000 zilizoagizwa na Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kutoka nje ya nchi na kupigwa marufuku na Serikali kuzitumia ambapo ametakiwa atumie vifaa vya ndani ya nchi. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua maendeleo ya Mradi huo, Aprili 5, 2020.
Vilevile, Dkt Kalemani alitoa maelekezo kwa Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuanza taratibu za kumpata Mkandarasi atakayejenga njia ya kusafirisha umeme kutoka eneo la Mradi hadi Kinyerezi jijini Dar es Salaam, umbali wa kilomita 167 ili kuuingiza kwenye gridi ya Taifa.
“Nataka Mradi huu unapokamilika na njia ya kusafirisha umeme huo iwe imekamilika tayari kwa kuanza kuusafirisha na kuuingiza kwenye gridi ya Taifa.”
Hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), wakati Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) alipotembelea Mradi huo Aprili 5, 2020 kwa mara ya 11 tangu kuanza kutekelezwaji wake.
Katika ziara hiyo, Waziri alifuatana na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wataalamu akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka, Meneja wa Shirika hilo mkoani humo, Mhandisi FedGrace Shuma, Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Ahmed Chinemba pamoja na wataalamu wengine mbalimbali.

No comments:

Post a Comment