Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akifuta machozi wakati
akielezea namna alivyomjua Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin
William Mkapa wakati akihutubia katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28
Julai, 2020 amewaongoza Watanzania kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa aliyefariki dunia tarehe
23 Julai, 2020.
Mwili
wa Hayati Benjamin William Mkapa ulianza kuagwa tarehe 26 Julai, 2020 katika
uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na kuhitimishwa leo ambapo pamoja na
Rais Magufuli na familia ya Hayati Mkapa, viongozi wengine wakiwepo Makamu wa
Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Jen. Alain Guillaume Bunyoni (kwa niaba ya Rais wa Burundi Mhe. Jen.
Evariste Ndayishimiye) na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd wamepata fursa ya kutoa heshima za mwisho.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, akitoa hashima ya mwisho kwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa, wakati wa hafla ya Kitaifa ya kuuaga mwili wa marehemu katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar leo
Wengine
ni Waheshimiwa Maspika, Majaji Wakuu, Marais Wastaafu, Mawaziri Wakuu Wastaafu,
Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa Dini, Viongozi
wa Vyama vya Siasa na viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Katika
salamu zake, Rais Magufuli amesema Taifa limepoteza mtu aliyetoa mchango
mkubwa katika kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi, kuimarisha huduma za kijamii
(elimu, maji, afya),
kuanzisha na kuimarisha taasisi muhimu za Serikali, kuimarisha sekta binafsi, kujenga
miundombinu hasa barabara na madaraja, kuinua ukusanyaji wa kodi, kuimarisha
uhusiano na ushirikiano wa kimataifa, ukombozi na utatuzi wa migogoro ya
Mataifa mbalimbali ya Afrika na aliyekuwa mahiri katika kuibua vipaji vya
viongozi akiwemo yeye mwenyewe, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein na
Mgombea wa Kiti cha Urais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitoa heshima ya mwisho kwa mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Benjamin William Mkapa, wakati wa hafla ya kuuaga mwili wa marehemu Kitaifa katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam Leo
Mhe.
Rais Magufuli amebainisha kuwa Hayati Benjamin William Mkapa ameacha mengi mazuri
ya kujivunia na kuendelea kujifunza yakiwemo uongozi bora uliosimamia umoja,
mshikamano, uchapakazi, uzalendo, uwajibikaji, uwazi na uhusiano mzuri wa
kimataifa na ameahidi kuwa Serikali anayoiongoza itafanya kila liwezekanalo ili
kudumisha na kuendeleza mambo yote mazuri yaliyoasisiwa nae.
Mjane wa Marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Benjamin William Mkapa Mama Anna Mkapa akitoa heshima yake ya mwisho kwa mwili wa marehemu wakati wa hafla ya Kitaiga ya kuuaga mwili huo iliofanyika katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam Leo
Rais Magufuli amesema yeye binafsi amefanyiwa mengi mazuri na Hayati Benjamin
William Mkapa ambaye hakutaka aanguke kwa kumlea kama mwanae na kwa upendo
mkubwa.
“Mzee
Mkapa ni shujaa wangu na ni mtu muhimu sana katika historia ya maisha yangu,
hata nilipopatwa na shida ama kukumbwa na changamoto mbalimbali, Mzee Mkapa
hakuniacha, hivyo kuondoka kwake ni pigo kubwa sana kwangu kwa vile nimempoteza
mtu muhimu sana katika maisha yangu” amesisitiza
Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewapa pole wanafamilia wakiongozwa na Mjane wa Hayati
Benjamin William Mkapa, Mama Anna Mkapa na Watoto wake, amewaombea moyo subira,
uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa
na mpendwa wao.
Amewashukuru
Watanzania wote kwa utulivu na mshikamano katika kipindi hiki cha maombolezo ya
tangu Benjamin William Mkapa afariki dunia, pia amewashukuru viongozi wa
dini, vyombo vya ulinzi na usalama, vyombo vya habari, wageni mbalimbali na
wote waliotuma salamu za rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa uliolikumba
Taifa.
Mwili
wa Hayati Benjamin William Mkapa umesafirishwa kwa ndege ya Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
kwenda kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara ambapo hapo kesho utazikwa
kwa taratibu kidini na kwa heshima zote za kijeshi.