Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha
Katika kuendeleza ushirikiano na Sekta binafsi, ambalo ni
jukumu la kisheria la Serikali kuhamasisha sekta binafsi katika uzalishaji wa
Mbegu Bora, Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda katika ziara yake Jijini
Arusha, leo tarehe 30 Mei 2021 ametembelea moja ya kampuni binafsi ya
uzalishaji wa Mbegu Bora za Kilimo nchini SEED.CO
Waziri
Mkenda pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao wa Wizara ya Kilimo Ndg Nyasebwa
Chimagu wamepata fursa ya kujionea na kujifunza shughuli mbalimbali
zinazofanywa na Kampuni hiyo binafsi hasa katika suala zima la uchakataji na
utunzaji wa Mbegu Bora unavyofanywa na kampuni hiyo kutoka hatua za awali Mbegu
zinapotoka shambani, zinapopokelewa, kuchakatwa, kupimwa na kupakiwa tayari kwa
kumfikia mkulima.
Katika ziara hiyo Waziri Mkenda amesema kuwa moja ya
ajenda kuu ya Wizara ya Kilimo ni kuhakikisha nchi inazalisha mbegu za kutosha za
kilimo kupitia sekta binafsi kadhalika Mamlaka ya Mbegu ya Serikali (ASA) ili
kufikia hatua ya kujitosheleza katika uzalishaji mbegu na kuanza kuuza nje ya
nchi.
Amesema kuwa serikali inahimiza Taasisi ya Utafiti
Tanzania (TARI) pamoja na Taasisi zote zinazojihusisha na utafiti hususani wa
mbegu kuhakikisha kuwa zinazendelea kufanya utafiti wa mbegu bora na zitakazo ongeza
tija katika kilimo.
“Tunataka mtu aweze kuzalisha kiasi kikubwa zaidi kwa
Hekari moja ili nguvu ya mkulima iwe inazaa matunda makubwa na vilevile
itatusaidia sana kwenye masoko kwa sababu ukizalisha kwa wingi hata kama bei ya
mazao imeshuka lakini kipato kinakuwa kikubwa” Amekaririwa Prof Mkenda
Waziri Mkenda amesema kuwa pamoja na juhudi za serikali za
kutumia taasisi ya utafiti (TARI) na mamlaka ya Mbegu (ASA) ambayo ina kazi ya
kuchukua mbegu bora na kuzalisha kwa wingi ili kuzipeleka kwa mkulima lakini
pia serikali inafanya kazi kwa karibu na sekta binafsi ikiwemo kampuni ya mbegu
ya SEED.CO
Prof Mkenda ameipongeza kampuni binafsi ya uzalishaji wa
Mbegu Bora za Kilimo nchini SEED.CO kutokana na uzalishaji wa mbegu bora ambazo
zimekuwa na matokeo mazuri kwa wakulima ambapo amewahakikishia hitaji lao kubwa
la kukodi mashamba ya serikali kwa ajili ya uzalishaji mbegu bora linafanyiwa
kazi kwa haraka iwezekanavyo.
“Lakini nimewaahidi endapo watajenga maabara kubwa ya
kisasa kwa ajili ya shughuli za mbegu hapa Tanzania, nitajitahidi kuhakikisha
kuwa wanapata mashamba makubwa angalau mawili kwa ajili ya kuongeza uzalishaji
wa mbegu” Amesema Mkenda
Amewasihi kuongeza zaidi uzalishaji wa mbegu ikiwa ni
pamoja na kuanzisha uzalishaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali badala ya
Nafaka na Mbogamboga pekee, Kwa kufanya hivyo kutakuwa na uwezekano wa kuongeza
mbegu bora na zenye tija kwa wakulima nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa jumuiya ya
Wafanyabiashara wa Mbegu (TASTA) Ndg Bob Shuma amepongeza Serikali kwa kuamua
kulichukulia kwa msisitizo swala la uzalishaji wa mbegu bora nchini ambapo
ameeleza furaha yake na kumuhakikishia Waziri wa Kilimo kuwa umoja huo
unaendelea na mkakati madhubuti katika uzalishaji wa mbegu bora na kwa wingi.
Hata hivyo amerejea msisitizo wa Waziri wa Kilimo kuyaomba
mashirika mengine nchini na nje ya nchi kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza
katika sekta ya mbegu ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa karibu na serikali
kupitia taasisi ya TARI na ASA ili kuongeza ufanisi katika sekta ya mbegu.