Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika, Dkt. Taufila Nyamadzabo, baada ya kumalizika kwa kikao cha Magavana wa Benki ya Dunia kutoka Kanda ya Afrika, kilichofanyika Makao Makuu ya Benki hiyo, wakati wa Mkutano wa Kipupwe unaofanyika Jijini Washington DC, Marekani.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiwasilisha hoja za Tanzania kwenye Mkutano wa Magavana wa Benki ya Dunia wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika (Africa Group I Constituency-WB), wakati wa Mikutano ya Kipupwe inayoendelea Jijini Washington DC, Marekani.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa tatu kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika, Dkt. Taufila Nyamadzabo (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, (wa tatu kulia) Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika, Dkt. Zarau Kibwe (wa pili kulia) na kamishna wa Idara ya Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Sauda Msemo, wakati wa mikutano ya Majira ya Kipupwe, Jijini Washington DC, Marekani.
Na Benny Mwaipaja, Washington DC
Waziri wa Fedha na Mipango. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kuwa Serikali itaendelea kubuni sera zitakazochangia kupunguza makali ya maisha na kuimarisha uchumi ikiwa ni hatua za kupambana na athari za UVIKO 19 na Vita baina ya Urusi na Ukraine.
Dkt. Nchemba alisema hayo Mjini Washington DC nchini Marekani, baada ya kikao cha Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka Kundi la Kwanza la nchi za Afrika, ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Alisema kuwa sera hizo zitalenga kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa zinazotokana na mzozo unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine uliosababisha bei za mafuta ya kula na baadhi ya vyakula na mazao kama ngano kupanda bei kupindukia.
Dkt. Mwigulu alisema kuwa nchi wanachama wa Benki ya Dunia hususan kutoka Bara la Afrika zimeathirika kwa kiasi kikubwa na majanga ya UVIKO 19 pamoja na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine hivyo njia za kukabiliana na hali hiyo zinachukuliwa kwa uzito unaofaa.
“Tumejadiliana hatua za kuchukua kutokana na athari za UVIKO19 na Vita vya Ukraine na Urusi, namna tutakavyokabiliana na madhara ya kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu zinazotumiwa na wananchi wetu ili ziwe nafuu ambapo tumetazama fursa zinazopatikana kupitia Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF” alisema Dkt. Nchemba.
Tathimini iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF inaonesha kuwa uchumi wa dunia ulikua kwa wastani wa asilimia 5.9 mwaka 2021 na unatarajiwa kukua kwa asiimia wastani wa 4.9 mwaka 2022.
Katika kukabiliana na UVIKO 19, Benki ya Dunia ilitoa kiasi cha dola za Marekani bilioni 25.2 ili kuzisaidia nchi wanachama ikiwemo kufadhili program 43 za chanjo ya ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment