Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amewahimiza waombaji mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 kusoma na kuuzingatia ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa 2022/2023’ ili kuwasilisha maombi kwa usahihi.
Prof. Mkenda ameyasema hayo katika hafla fupi ya kuzindua mwongozo huo iliyofanyika katika ofisi za HESLB jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa HESLB Prof. Hamisi Dihenga na wadau wengine wa HESLB.
Prof. Mkenda amesema: “Kuanzia leo (Jumanne, Julai 12), mwongozo huu utapatikana katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) na ya Wizara (www.moe.go.tz) katika lugha mbili za Kiswahili na Kiingereza … na kuwapa fursa waombaji kuusoma. Dirisha la kupokea maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao linatarajiwa kufunguliwa Julai 19 hadi Septemba 30, 2022,” amesema na kuongeza:
“Dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2022/2023 litakuwa wazi kwa muda wa siku 70 kuanzia Julai 19 hadi Septemba 30 mwaka huu, hivyo tunawasihi wanafunzi waombaji wasome mwongozo kabla ya kuomba mkopo kwa kuwa ndiyo unataja sifa, vigezo na utaratibu wa kuomba mkopo,” amesema Prof. Mkenda.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe amewakumbusha waombaji mikopo kuzingatia maelekezo yaliyomo kwenye mwongozo ili kuondokana na changamoto ambazo hujitokeza kwa waombaji.
“Uzoefu unaonesha kuwa wanafunzi waombaji wamekuwa hawazingatii taratibu wakati wa kufanya maombi. Tunawasii mzingatie maelekezo ya mwongozo. Wakati wa dirisha la maombi kumekuwepo na changamoto nyingi zinazojitokeza kwa waombaji”, amesema Prof. Mdoe.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema kila mwaka mwezi Julai, HESLB huanza kupokea maombi ya mkopo kwa mwaka wa masomo unaofuata ambapo mwongozo huo hutoa maelezo ya kina kuhusu sifa na utaratibu wa kupanga mikopo kwa mwaka husika.
“Mwongozo huo umekamilika na kuidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi. Kuanzia wiki ijayo, tutaanza kuendesha programu za elimu kwa umma kupitia redio, televisheni, mikutano katika Kambi za JKT na mitandao ya kijamii” amesema Badru.
Katika mwaka wa masomo 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha TZS 573 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo na skolashipu kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.
Waziri wa ElLmu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda (katikati) akikata utepe kuashiria
uzinduzi wa Mwongozo wa Uombaji Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa
masomo 2022/2023. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru na
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi HESLB, Prof. Hamisi Dihenga. Hafla hiyo imefanyika leo
Jumanne Julai 12, 2022 Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment