Matokeo chanyA+ online




Tuesday, July 28, 2020

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN ASHIRIKI KUAGA MWILI WA MZEE MKAPA






Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, leo Julai 28, 2020 ameshiriki kwenye Ratiba ya Viongozi Wakuu kuaga Mwili wa Marehemu Mzee Benjamin William Mkapa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania iliyofanyika Uwanja wa Taifa wa Mkapa Jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Monday, July 27, 2020

WAZIRI MKUU WA BURUNDI AWASILI NCHINI KUHUDHURIA MAZIKO YA KITAIFA YA HAYATI BENJAMIN MKAPA

Viongozi mbalimbali kutoka nje ya Tanzania wameanza kuwasili nchini kuhudhuria maziko ya kitaifa ya Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Benjamin William Mkapa aliyefariki usiku wa kuamkia ijumaa ya Julai 24,2020 Jijini Dar es Salaam.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Jenerali Alain Guillaume Bunyoni akishuka kwenye mdege ya Shirika la Ndege la Tanzania mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuhudhuria maziko ya kitaifa ya Hayati Benjamini William Mkapa.

 

Waziri Mkuu wa Burundi Jenerali Alain Guillaume Bunyoni amekuwa kiongozi wa kwanza kutoka mataifa ya nje kuwasili hapa nchini majira ya saa tano na dakika 20 kwa ndege ya Shirika la ndege la (Tanzania Air Tanzania) ambapo amesema Burundi imepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha Hayati Benjamin William Mkapa na hivyo kutokana na urafiki wa kindugu baina ya Tanzania na Burundi amekuja nchini kuwakilisha wananchi Waburundi kuomboleza na Watanzania kifo cha Mkapa.

 

Katika msafara wake Waziri Mkuu huyo ameambatana pia na Spika wa Baraza la Seneti la Burundi Mhe. Reverien Ndikuriyo ambaye kwa upande wake amesema kifo kimeyapokonya Maisha ya Hayati Benjamin William Mkapa ambaye bado alikuwa akihitajika kwa kiasi kikubwa hususani na Bara la Afrika kutokana na uwezo wake mkubwa aliokuwa nao katika usuluhishi na hivyo Burundi imempoteza msuluhishi mkubwa.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiteta jambo na Waziri Mkuu wa Burundi Mhe. Jenerali Alain Guillaume Bunyoni mara baada ya kuwasili nchini kuhudhuria maziko ya kitaifa ya Hayati Benjamini William Mkapa.

 

Mbali na Spika wa Baraza la Seneti la Burundi Mhe. Reverien Ndikuriyo,pia Waziri Mkuu wa Burundi Jenerali Alain Guillaume Bunyoni ameambatana na Naibu katibu Mkuu wa chama kinachotawala nchini Burundi cha CNDD-FDD Mhe. Joseph Ntakarutimana.

 

Akizungumza mara baada ya kuwapokea viongozi hao Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema wageni hao wamewasili jana Mkoani Kigoma wakitokea Burundi na baadae kupanda ndege na kuwasili Dar es Salaam hii leo na kuongeza kuwa ujio wa viongozi hao wa Burundi unaidhihirishia dunia mahusiano mema nay a kindugu yaliyopo kati ya Tanzania na Burundi bila ya kujali nyakati za shida,kuomboleza ama raha.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akisalimiana na Waziri Mkuu wa Burundi Mhe. Jenerali Alain Guillaume Bunyoni mara baada ya uwasili uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuhudhuria maziko ya kitaifa ya Hayati Benjamini William Mkapa.


Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kutoa taarifa za kuwasili kwa viongozi wa Mataifa mbalimbali katika maziko ya kitaifa ya Hayati Benjamin William Mkapa kwa kadri zitakavyopokelewa.

WIZARA YA KILIMO YAMLILIA RAIS MSTAAFU BENJAMIN WILLIAM MKAPA


Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akizungumza na Wakulima, Waoneshaji na wadau wengine wa Kilimo kabla ya kuzindua rasmi maonesho hayo ya Kilimo Biashara yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian cha Jijini Arusha. 

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akikabidhi majembe matano ya kukokotwa na ng'ombe yaliyotokewa na Kituo cha Utafiti cha Selian kwa kikundi cha Wakulima kinachofanya kazi karibu sana na kituo hicho. ( kwenye picha ni baadhi ya viongozi wa kikundi hicho.)

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Cha Selian cha Jijini Arusha Dkt. Joseph Ndunguru akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunguliwa rasmi kwa maonesho hayo kituoni hapo.
 Bango la maonesho hayo.

 Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akikata keki iliyotengenezwa kwa kutumia unga wa maharage ambayo lengo lake ilikuwa kuonesha matumizi mbalimbali ya maharage katika jamii.
 Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga pamoja na wananchi na viongozi wengine waliotembelea  vipando vya mazao mbalimbali vilivyopandwa kuonesha teknolojia mbalimbali za Kilimo. 
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, akitembelea mabanda katika maonesho hayo.



 Na Calvin Gwabara, Arusha

Waziri  wa Kilimo Japhet Hasunga amesema Wakulima na Wizara yake imempoteza Kiongozi ambaye si tu kwamba alisisitiza Watanzania kutumia nguvu zao kama mtaji katika kufanya kazi bali aliyehakikisha kilimo kinatoa mchango mkubwa katika maendeleo yao na Taifa.

Akizungumza kwenye Maonesho ya Kilimo Biashara yaliyofanyika kwenye Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian cha Jijini Arusha Hasunga alisema kuna mambo mengi sana ambayo tunajivunia leo kwenye Kilimo yametoka na mchango Mkubwa wa Rais wa Awamu ya Tatu Marehemu Mhe. Benjamin William Mkapa.

 Akizungumzia baadhi ya mambo hayo alisema ni msimamo wake thabiti katika kuhakikisha wataalamu wa kilimo kwa ngazi zote wanatoka maofisini na kwenda kutoa elimu stahiki kwa wakulima na wafugaji ili kilimo kinachotegemewa na zaidi ya asilimia 75 ya watanzania kitoe mchango unaostahili.

 “Aliposema mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe alisisitiza watu kutumia nguvu zao kama mtaji katika uzalishaji mali kwa kufanya kazi mbalimbali hasa za kilimo ili kutokomeza njaa na umasikini kwenye kaya.” alisema  Hasunga.

Waziri huyo wa kilimo pia akibainisha kuwa uanzishwaji wa TASAF ilikuwa ni moja ya jitihada za kusaidia kaya masikini ambazo nyingi zipo vijijini zinajishughulisha na kilimo huku akipambana na rushwa kwa kuanisha Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ili masikini wapate haki kwenye ofisi za serikali na kwenye maeneo mengine wanapokwenda kutafuta huduma.

 “ Niwatakie watanzania hasa wakulima na wataalmu wa kilimo kumuenzi kwa vitendo Marehemu Benjamin Mkapa kwa yale yote ambayo aliyaanzisha na kuyasisitiza ili kuwakomboa watanzania wanyonge na wale wenye kipato cha chini” alisisitiza Hasunga.

 Waziri huyo wa kilimo ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI na Kituo cha Utafiti cha Selian cha Jijini Arusha kwa kuandaa maonesho hayo ya Kilimo Biashara kwa lengo la kuwezesha wakulima kujionea na kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa za kilimo ili ziwaisaidie kuboresha kilimo chao na kuongeza tija.

 Alisema kilimo cha kizamani na cha kutumia mbegu za asili hakina tija kwa mtazamo wa kibiashara na badala yake watumie mbegu zilizoboreshwa ili wazalishe zaidi na kupata ziada lakini serikali haizuii wakulima kulima mbegu za asili lakini tafiti zinaonesha mbegu za asili hazina tija sana kutoka na uwezo wake wa kushindwa kuhimili Magonjwa, Wadudu na mabadiliko ya tabia nchi.

 Awali akieleza malengo ya maonesho hayo Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian cha Jijini Arusha ambao ndio walioandaa maonesho hayo Dkt. Joseph Ndunguru alisema ni kuwaonesha wadau wote wa kilimo teknolojia, mbinu na aina mbalimbali za mbegu ambazo wamezalisha ili Wakulima wazione na kuchagua zinazowafaa kwenye maeneo yao.

 Alisema kituo hicho ambacho kina dhamana kwenye utafiti wa maharage nimezalisha mbegu mbalimbali za maharage ambayo yana sifa mbalimbali ambazo ni kuvumilia magonjwa, zenye viinilishe mbalimbali hasa madini ya chuma, zinazoendana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na zinazofaaa kwa usindikaji kutimiza ndoto ya Tanzania ya Viwanda.

 Dkt. Ndunguru alisema pamoja na kuonesha kazi zinazofanywa na kituo hicho pia wametoa nafasi kwa wadau wengine wa kilimo hasa makampuni ya mbegu na pembejeo zingine kuonesha bidhaa wanazozalisha ili wananchi wapate uwanja moana zaidi wa kuchagua kulingana na mahitaji yao ya Kilimo kwenye maeneo yao.

 Mkurugenzi Mkuu wa TARI,  Dkt. Geofrey Mkamilo alisema Taasisi hiyo ina vituo 17 nchi nzima ambavyo vinafanga kazi kubwa ya kuzalisha teknolojia mbalimbali kulingana na mahitaji ya kanda husika za kilimo na kwamba kazi kubwa iliyo mbele yao ni kuhakikisha matokeo hayo mazuri ya Utafiti kwenye kila kituo ya wafikia wadau wote wa Kilimo ili wazitumie na kuongeza uzalishaji.

 “ Niwaatamkie leo rasmi waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini nyinyi ni sehemu ya TARI na naomba wakurugenzi wote wa vituo kokote nchini kufanya kazi na waandishi wa habari ili wasaidie kufikisha matunda ya tafiti zetu kwa jamii kwa upana wake maana hatuwezi kufika kila mahali kama ambavyo vyombo vya habari vinafika” alisisitiza Dkt. Mkamilo.

 Aidha, Mkurugenzi huyo Mkuu wa TARI alisema kuwa hivi sasa wameanzisha utaratibu mzuri ambao vituo vyote vya utafiti vitakuwa vinashamba la maonesho kwenye vituo vyao kuonesha teknolojia mbalimbali wanazozalisha kwa Mwaka mzima ili wananchi wakaone na kujifunza badala ya kutegemea wakati wa maonesho ya nanenane pekee ambayo hufanyika siku nanenane tu kwa mwaka.

Nao baadhi ya wakulima walioshiriki kwenye maonesho hayo ya Kilimo Biashara kwenye kituo cha Utafiti cha Selian Jijini Arusha wamemuomba waziri wa kilimo kusaidia somo ka kilimo kuanza kufundishwa kuanzia shule za msingi ili wale wanaoshindwa kuendelea na elimu ya juu washiriki kwenye kilimo kwa kulima kisasa.

 Katika kutambua mchango wa vikundi vya wakulima Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian Dkt. Joseph Nduguru alijibu ombi ka Kikundi cha wakulima kilichotembelea maonesho hayo ombi lao la kupatiwa majembe ya kukokota na ng’ombe matano ambayo yalikabidhiwa na Mhe. waziri wa kilimo huku mdau mwingine Mero Agro akiongezea majembe mengine mawili na hivyo kupata majembe 7.

Sunday, July 26, 2020

MWANADIPLOMASIA NGULI NA MWANASIASA MARIDHAWA AACHA ALAMA

Na. Immaculate Makilika - MAELEZO

Nianzie wapi kumuelezea Mzee wa Uwazi na Ukweli? Hebu nianzie kwenye kitabu chake cha Maisha Binafsi ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa chenye jina la “Maisha Yangu, Dhamira Yangu: Rais wa Tanzania Akumbuka” alichokizindua hapo Novemba 12, 2019 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli alikuwa Mgeni Rasmi, Mzee  Mkapa anasimulia kuwa maono yake: ni maisha ya hali ya juu, amani, utulivu na umoja, utawala bora, jamii iliyoelimika na uchumi shindani wenye uwezo wa kukua kiendelevu na mgawanyo shirikishi wa kipato.

Ni dhahiri kuwa kifo cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa kilichotokea hapo jana Julai 24, 2020 ni pigo kwa taifa, Afrika pamoja na dunia kufuatia mchango wake ulioakisi mabadiliko ya uchumi, mahusiano ya kimataifa na mapinduzi katika sekta za umma na binafsi.

Kama mjuavyo ni katika uongozi wa Mzee Mkapa ambapo mikakati mbalimbali ya kimaendeleo ilianzishwa, baadhi ni Dira ya Taifa 2025, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA), Mpango wa Kurasimisha Biashara na Mali  za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) na  Mini Tiger Plan 2020.

Aidha, Rais  Mkapa alianzisha Bima ya Taifa, Mageuzi katika Elimu, na Mradi wa Maji ziwa Victoria, halikadhalika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), mageuzi haya yalihitaji kiongozi makini mwenye mapenzi kwa taifa lake lakini aliyeishi na kuamini ndoto zake za kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Shughuli za maendeleo na ukuaji wa uchumi

Wakati wa uongozi wake Mzee Mkapa aliyekuwa Rais, mwandishi wa habari na mwanadiplomasia nguli  aliweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii, ikiwa ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kupitiliza malengo na kukusanya kiasi cha sh. bilioni 133 kwa mwezi kati ya Julai na Novemba 2004, kulingana na takwimu za Serikali, kudhibiti mfumuko wa bei kutoka asilimia 30 hadi chini ya 5.5 na  kukua kwa uchumi kwa asilimia sita.

Duru za siasa za ndani na kimataifa

Itakumbukwa kuwa Mkapa ni Rais wa kwanza nchini Tanzania kuingia madarakani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika zama za siasa za vyama vingi mnamo mwaka 1995.

Akiwa amebakiza takriban miezi kumi tu kumaliza kipindi chake cha kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Benjamin William Mkapa aliwahi kukemea tabia ya watu wanaotishia kuvunja amani katika nchi aliyoipokea  kutoka kwa wenzake waliomtangulia ikiwa na amani na utulivu.

Alionesha wazi kuwa mfumo wa siasa wa vyama vingi haukuanzishwa nchini ili kudhoofisha utaifa, umoja na mshikamano kwa taifa.

“Hatukuanzisha mfumo wa siasa wa vyama vingi ili watu wetu wachukiane, watishane kwa kunoa mapanga waumizane, wauane au waharibiane mali zao,” alisema Mzee Mkapa.

Hakuna shaka kwamba utawala wa Rais Mkapa ulijaa mambo mengi mazuri ambayo hayataweza kufutika katika kizazi hiki na mara kadhaa alihubiri juu ya  amani, na kuheshimu  haki za binadamu ikiwemo haki ya kuishi.

Katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu, ni vyema tukakumbuka aliyowahi kusema Rais  Mkapa mwaka 2005 wakati ambapo nchi ilifanya Uchaguzi Mkuu.

“Tuje tuwaogope sana wanaohubiri chuki kwa kisingizio cha ushindani wa kisiasa. Ushindani tunaotaka sisi ni wa hoja, wa fikÅ•a, wa mikakati na mipango ya maendeleo. Tunashindanisha ilani za uchaguzi wa vyama. Ningependa vyama vyetu vyote vya kisiasa viwe na malengo makuu yanayofanana yaani umoja, amani, upendo, maendeleo na ustawi wa taifa na wananchi. Tunachotofautisha na tunachoshindania kiwe mipango na mikakati ya kufikia malengo hayo makuu,” alisema Mzee Mkapa.

Aidha, Mzee Mkapa alikuwa mpatanishi wa mgogoro wa Burundi ambapo alizitaka pande husika katika nchi hiyo kushikamana na kuheshimu mchakato wa amani na hatua zilizopigwa za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo. Pia, alihusika  katika upatanisho wa migogoro ya nchi za  Sudani ya Kusini, Congo Mashariki, na Kenya.

Katika hali isiyotarajiwa na wengi ni kwa kiongozi aliyewahi kuwa Rais kukiri wazi juu ya udhaifu wake, ambapo aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala amechambua wasifu wa Mzee Mkapa katika kitabu chake cha Maisha Yangu, Dhamira Yangu: Rais wa Tanzania Akumbuka, anaandika, “Mheshimiwa Mkapa anakiri kuwa, kabla hajawa Rais, hakujua kuwa kazi moja wapo ya Rais ni kutoa pole. Mojawapo ya mapungufu yangu ni kwamba si mwepesi wa kuonyesha hisia zangu. Mrithi wangu Rais Kikwete ni mzuri sana katika hili. “Anasema Mheshimiwa Mkapa, ameandika Profesa Mkandala.

Mwisho kabisa Mzee Mkapa, anamalizia kwa kusema; Nitamuachia Mungu wangu na nyinyi kuamua ni tofauti gani nimeifanya humu duniani.

Kama taifa yapo mengi ya kujifunza kutoka kwa Mzee Mkapa na kumuenzi ni pamoja na kuthamini mchango uliosaidia kuleta maendeleo ya kijamii, kiasiasa na kiuchumi.

MKAPA MSHUMAA ULIOZIMIKA GHAFLA, TUTAKUKUMBUKA DAIMA MZEE WA UKWELI NA UWAZI

Jonas Kamaleki

Ni majuzi Mzee wetu Mpendwa, Benjamin William Mkapa ukiwa Dodoma uliongoza Kikao cha Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa umahiri mkubwa, kumbe ndo ulikuwa ukituaga! Wengine tulijua kuwa utapiga kura Oktoba na kushiriki katika sherehe za kumwapisha Rais atakayekuwa amechaguliwa, kumbe sivyo, Mkapa umetutangulia ghafla kwenda kwa Muumba wetu. Burian Mzee wetu wa Uwazi na Ukweli.

Tutakukumbuka kwa uongozi wako uliotukuka na unyenyekevu uliokuwa nao kwa kuwaheshimu wakubwa kwa wadogo tangu ukiwa Pugu Sekondari, Chuo Kikuu Makerere hata ulivyorudi nchini na kuendelea na majukumu yako kwa uzalendo mkubwa. Kwenye Tasnia ya Habari msiba huu ni pigo kwani Mzee Mkapa alikuwa  Mhariri mahiri wa The Nationalist hadi Daily News. Waliofanya nawe kazi akiwemo mwandishi nguli, Jenerali Ulimwengu anasema kuwa kwenye chumba cha habari Mzee Mkapa alikuwa mwalimu na mlezi.

Mkapa atakumbukwa kwa kupinga na kupambana na rushwa. Katika kudhihirisha hilo, Mzee Mkapa aliunda Tume ya Warioba kuchunguza vitendo vya rushwa na kutoa mapendekezo. Hakuishia hapo kwani aliunda Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) ambayo baadae ikaja kujulikana kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Wakati Mzee Mkapa anaingia madarakani alikuta uchumi wa nchi unayumba, hivyo alibuni mbinu kadhaa za kufufua uchumi. Moja ya mbinu aliyoibuni kiongozi huyo ni kuunda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kubuni vyanzo vya mapato na kukusanya kodi.

Hakuishia hapo bali alitilia mkazo ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na kuboresha usafiri wa majini. Katika hili alianzisha Wakala wa Barabara nchini (TANROADS). Wakala ambao ulijenga barabara kwa kiwango cha lami za kuunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara. Kwenye hotuba zake za kila mwezi hakuchoka kujinadi na kazi yake ya kuboresha miundombinu. Mzee Mkapa alisikika akisema, “Tumeboresha miundombinu, tumejenga shule za msingi na sekondari”.

Mkapa alifanikisha kuunda Taasisi za udhibiti, Taasisi na mifuko ya kuinua Wananchi kama  Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) na Mpango wa Kurasimisha Biashara na Mali za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).

Jambo jingine ambalo watanzania wanapaswa kulijua au kulikumbuka ni lile la kumuibua Jemedari Mkuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipomteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi chini Waziri Anna Abdallah mwaka 1995.

Ukweli na Uwazi ndio ilikuwa Kaulimbiu maarufu ya Mpendwa wetu Benjamin William Mkapa. Aliamini kuendesha Serikali yake kwa ukweli na uwazi.

MABALOZI: TANZANIA, AFRIKA IMEPOTEZA MSULUHISHI NGULI WA AMANI

Balozi wa Denmark nchini Mhe. Mette Dissing-Spandet akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Rais Mstaafu wa Tanzania Mzee Benjamin Mkapa tarehe 26 Julai 2020 jijini Dar es Salaam

Balozi wa Hispania nchini Mhe. Fransisca Pedros akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Rais Mstaafu wa Tanzania Mzee Benjamin Mkapa leo tarehe 26 Julai 2020 jijini Dar es Salaam


Mwakilishi wa Ubalozi wa Sweden nchini Bw. Michael Sulusi akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Rais Mstaafu wa Tanzania Mzee Benjamin Mkapa

Mwakilishi wa Ubalozi wa Uganda nchini Bibi. Musekura Eseza akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mzee Benjamin Mkapa 


Balozi wa Algeria nchini Mhe. Ahmed Djellal akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mzee Benjamin Mkapa  

Mwakilishi wa Ubalozi wa Sudan nchini Bw. Jaafar Nasir Abdalla akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mzee Benjamin Mkapa


Balozi wa Zambia nchini Mhe. Benson Keith Chali akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mzee Benjamin Mkapa


Balozi wa Somalia nchini Mhe. Mohamed Hassan akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mzee Benjamin Mkapa


Balozi wa Congo DRC nchini Mhe. Jean -Pierre Mutamba akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mzee Benjamin Mkapa
Mwakilishi wa Ubalozi wa Uturuki nchini Bw. Onur Yay akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mzee Benjamin Mkapa

Balozi wa Morocco nchini Mhe. Abdelilah Benryane akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mzee Benjamin Mkapa

Baadi ya mabalozi wakiwa katika picha ya pamoja na mama Anna Mkapa mara baada ya kutoa salamu za pole nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam  


Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, wameendelea kujitokeza kusaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa na kumuelezea kuwa ni kiongozi mahiri na msuluhishi nguli wa amani barani Afrika na duniani.

Mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo, baadhi ya mabalozi hao wakaelezea walivyoguswa na msiba wa Mkapa na kusema Tanzania imepoteza kiongozi na msuluhishi nguli wa amani barani Afrika na duniani.

Kwa upande wake, Balozi wa Zambia nchini Mhe. Benson Keith Chali amesema kuwa Zambia wameguswa sana na msiba kwani Tanzania na Zambia ni ndugu, "toka mwanzoni Nyerere na Kaunda walikuwa ndugu na sisi tumeendelea kuwa ndugu na unapopoteza ndugu unaumia sana. Sisi kama Zambia kwa kweli tumepokea kwa masikitiko makubwa tarifa za kifo cha Mzee Mkapa," .

"Tutamkumbuka Mzee Mkapa kama kiongozi aliyesimamia amani maeneo mbalimbali barani Afrika ikiwemo Kenya, Burundi, Congo DRC, na kwingineko duniani," amesema Mhe. Keith Chali   

Mhe. Keith Chali ameendelea kusema kuwa "Sisi kama Zambia tunatoa sana pole kwa familia yake, Serikali ya Tanzania na Watanzania kwa ujumla ……tunaomboleza wote msiba huu mzito,".

Nae Balozi wa Denmark nchini Mhe. Mette Dissing-Spandet amesema kuwa Rais Mstaafu Mzee Mkapa alikuwa kiongozi mahiri kwa Tanzania lakini pia alikuwa rafiki na mfano wa kuigwa na mataifa mbalimbali.

"kwetu sisi kama Denmark alikuwa rafiki na tutaendelea kumkumbuka daima kwa upendo wake," Amesema Mhe. Mette.

Aidha, nae Balozi wa Algeria nchini Mhe. Ahmed Djellal amesema kuwa Mzee Mkapa alikuwa mtetezi wa amani barani Afrika na atakumbukwa kwa mema aliyoyafanya kwani aliyafanya kwa jitihada na weledi wa hali ya juu, Mungu ampumzise kwa Amani.