Matokeo chanyA+ online




Saturday, August 23, 2025

SERIKALI YAREJESHA TABASAMU KWA CHIDI BENZ

SERIKALI YAREJESHA TABASAMU KWA CHID BENZ:  AWAASA WASANI KUKAA MBALI NA DAWA ZA KULEVYA
 
SERIKALI ya Awamu ya Sita kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kumtibu bure rapa wa muziki wa hip hop nchini, Rashidi Abdallah Mohamed Makwiro (Chid Benz) ambaye kwa miaka kadhaa alitumbukia kwenye uraibu wa dawa za kulevya, hivyo kudhoofika kiafya na kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema,Chid Benz ni miongoni mwa Watanzania milioni moja ambao wamepatiwa matibabu bure kutokana na uraibu wa dawa za kulevya kote nchini. Ameyasema hayo leo Agosti 22,2025 katika ofisi za DCEA jijini Dar es Salaam wakati akimkabidhi Chid Benz kwa familia na Watanzania baada ya Serikali kumpatia matibabu yaliyodumu ndani ya mwaka mmoja.

Ameeleza kuwa, DCEA licha ya majukumu iliyokasimiwa na Serikali ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini, pia imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kunakuwa na ustawi bora wa jamii nchini. 
"Lakini, jukumu letu lingine ni kuhakikisha kwamba tunajenga ustawi wa jamii ili wale ambao wamekwishajingiza katika matumizi ya dawa za kulevya tunahakikisha kwamba, tunawaondoa kwenye hayo matumizi ya dawa za kulevya."

Amesema kuwa, mafanikio hayo ya kumpatia Chid Benz na watu wengine matibabu yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ikiwemo miundombinu kwa mamlaka hiyo ili kuhakikisha wale ambao wameathiriwa na dawa za kulevya hususani vijana wanawapatia matibabu nchini. Serikali inafanya jitihada hizo kwa kutambua kuwa, vijana ni nguvu kazi ya Taifa, hivyo inapaswa kulinda na kusimamiwa kikamilifu ili ilete matokeo chanya katika uchumi na tija kwa Taifa. Pia, amesema Serikali ina jukumu la kuhakikisha inatibu watu kupitia vituo vya Mat Clinics na kupitia nyumba za upataji nafuu ili kuhakikisha ustawi wa jamii unaendelea kuimarika nchini
"Ni ili kuhakikisha ustawi wa jamii unaendelea kuimarika na nchi inasonga mbele, na isiyokuwa na watumiaji wa dawa za kulevya. Chid Benz alijikuta ameingia kwenye matumizi  ya dawa za kulevya, lakini baada ya DCEA kufanya operesheni kali ambazo zimesababisha dawa za kulevya kuadimika nchini, aliamua kuanza kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya kama mbadala.

Aidha, Kamishna Jenerali amesema, kutokana na Chid Benz kutokuwa na uelewa kuhusu athari za dawa tiba hizo ambazo zinatumika kwa uangalizi maalum kutibu saratani na kufanyiwa upasuaji, zilimuathiri zaidi kiafya. Kutokana na madhara hayo, Serikali ilimchukua Chid Benz na kumpeleka katika kituo cha upataji nafuu cha Pili Missana Foundation kilichopo jijini Dar es Salaam na sasa amepona.

Ameongeza kuwa, kati watu hao milioni ambao kwa nyakati tofauti wamepatiwa matibabu bure na Serikali kote nchini wengi wao ni vijana.
"Tunamtoa Chid Benz kama mfano wa vijana ambao wamepatiwa tiba na Serikali na wanerudi katika hali yao ya kawaida, kwa wanaomzoea Chid Benz kabla ya kupata matibabu na kuchukuliwa na Serikali hali yake ilikuwa mbaya sana na walimzushia kifo."

Amesema, baada ya Serikali kumpatia matibabu sasa afya yake imeimarika na yupo tayari kuanza kuwahudumia wananchi kwa burudani kama zamani na kuhakikisha nchi inaendelea kufurahi kwa kuwa na mwanamuziki hodari.
Chid Benz 

Kwa upande wake, Chid Benz ameishukuru DCEA kwa kumuonesha moyo wa upendo, kwani awali alikata tamaa baada ya kuathiriwa na matumizi ya heroin na dawa tiba zenye asili ya kulevya, lakini sasa yupo imara.
"Kwa kawaida watu husema bahati haiji mara mbili, sasa hivi nipo sawa na karibuni nitarudi mtaani kuendelea na kazi zangu, ninaombeni ushirikiano wenu, ninaishukuru sana mamlaka, ninamshukuru Brother Lyimo (Kamishna Jenerali Lyimo) kwa kunisaidia, Dkt.Mapana nipo bega kwa bega nao na nitafanya kazi kwa bidii."

Aidha, Chid Benz ametoa angalizo kwa wasanii wenzake kuepuka matumizi ya dawa za kulevya kwani si tu kwamba zinaathiri afya, bali pia zinaua ndoto na kipaji.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dkt.Kedmon Mapana ameishukuru DCEA kwa kazi kubwa iliyofanya kuhakikisha msanii Chid Benz anarejea katika hali yake.
Amesema, wakati baraza hilo likimkabidhi Chid Benz kwa mamlaka ili Serikali ikampatie matibabu hali yake ilikuwa mbaya zaidi, lakini leo ana afya njema na anatarajia kuanza kutekeleza majukumu yake ya kimuziki hivi karibuni.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Pili Missana Foundation, Bi.Pili Missana amewataka Watanzania kuondoa hofu kuhusu muonekano mpya wa Chid Benz.
Amesema, afya ya msanii huyo imeimarika na kuonekana mnene kutokana na matumizi sahihi ya lishe,na si makemikali ambayo alikuwa akiyatumia awali.

#KaziNaUtuTunasongaMbele
#KataaDawaZaKulevyaTimiza

Wednesday, August 20, 2025

 Mradi wa kilimo na usimamizi wa maji “New Delta” Misri,sisi kama Tanzania Tunajifunza nini?


Image
Mradi huu unakadiriwa kugharimu dola za Kimarekani bilioni 9.7. Unalenga kurejesha na kuendeleza kilomita za mraba 9,200 za jangwa kwa ajili ya kilimo. Hii ni sawa na kuongeza takribani asilimia 30 ya ardhi ya kilimo iliyopo sasa nchini Misri.
2. Miundombinu Mikuu
  • Mto bandia wenye urefu wa km 114: Utakuwa kama njia kuu ya kusafirisha maji kwenda kwenye maeneo mapya ya kilimo.
  • Vyanzo vya maji: Mradi unategemea mchanganyiko wa maji ya Mto Nile pamoja na teknolojia za matibabu ya maji taka (wastewater treatment) ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji ya umwagiliaji.
  • Mashamba ya kisasa: Sehemu kubwa itatumia umwagiliaji wa kisasa, ikiwemo drip irrigation, ili kupunguza upotevu wa maji.
Image
3. Malengo ya Mradi
Image
  1. Kuongeza uzalishaji wa chakula: Kupunguza utegemezi wa uagizaji chakula kutoka nje, hasa nafaka, mboga na matunda.
  2. Kukuza uchumi: Kuwezesha ajira mpya kwa mamilioni ya watu kupitia kilimo, ufugaji na viwanda vinavyohusiana.
  3. Kuhakikisha usalama wa chakula: Misri ni moja ya waagizaji wakubwa wa ngano duniani, na mradi huu unalenga kupunguza shinikizo hilo.
  4. Kupanua makazi na uwekezaji: Sehemu za jangwa zilizokuwa hazitumiki sasa zitabadilishwa kuwa vitalu vya kilimo, viwanda vya chakula, na hata makazi mapya.
4. Changamoto na Muktadha wa Kisiasa
  • Mto Nile na Ethiopia: Mradi huu unakuja wakati ambapo kuna mvutano wa kidiplomasia kuhusu Bwawa la Renaissance (GERD) nchini Ethiopia, ambalo Misri inahofia litapunguza kiwango cha maji yanayofika kwake.
  • Mahitaji makubwa ya maji: Mradi huu unahitaji matumizi makubwa ya maji katika taifa ambalo tayari linakabiliwa na changamoto za upungufu wa rasilimali hiyo.
Image
5. Faida Zinazotarajiwa
  • Kuongeza pato la taifa kupitia kilimo na mauzo ya nje.
  • Kutoa ajira kwa vijana na kupunguza msongamano wa idadi ya watu katika miji mikubwa kama Cairo.
  • Kuendeleza teknolojia za matumizi bora ya maji na kilimo cha kisasa.
  • Kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje na hivyo kuimarisha uhuru wa kiuchumi.
Image