Maafisa
wa Serikali kutoka Wizara ya Maji, Wizara ya Ujenzi, miundombinu na
Mawasiliano, wakiongozwa na Wizara ya Fedha na Mipango, wakipata maelezo
ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya
Bariadi hadi Maswa, (km50) wakati wa ziara ya ufuatiliaji wa utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Simiyu, ili kujua mafanikio,
changamoto na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.
Mchumi
kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Jordan Matonya, akitaka kupata
ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango
cha lami kutoka Bariadi hadi Maswa, mkoani Simiyu, yenye urefu wa km 50,
kutoka kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara mkoani humo, Mhandisi
Mohamedi Athumani (Hayuko pichani).
Na Benny Mwaipaja, WFM, Simiyu
UJENZI
wa barabara yenye urefu wa kilometa 50 kati ya mji wa Bariadi na Maswa
mkoani Simiyu kwa kiwango cha lami, inayojengwa kwa gharama ya shilingi
bilioni 88, unaendelea kwa kasi ambapo hivi sasa umefikia asilimia 34.
Kaimu
Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini-TANROADS, mkoa wa Simiyu, Mhandisi
Mohamedi Athumani, ameiambia timu ya maafisa wa Serikali inayoongozwa na
Wizara ya Fedha na Mipango, inayofuatilia utekelezaji wa miradi ya
maendeleo mkoani humo kwamba mradi huo utakapo kamilika mwezi Oktoba
mwakani, utafungua fursa za kibiashara na kiuchumi kwenye mkoa huo na
mikoa jirani ya Mwanza, Shinyanga, Singida na nchi jirani ya Kenya.
Amesema
kuwa kazi zilizofanywa na mkandarasi anayejenga barabara hiyo, Kampuni
ya CHICO ya China, ni kuanza kwa ujenzi wa madaraja makubwa mawili ya
Simiyu na Banhya na uinuaji wa tuta la barabara maeneo mbalimbli ya
mradi.
“Kuna
madaraja mengine madogo madogo (Pipe culverts 57) pamoja na makalvati
madogo (Box culverts 12), kwenye kipande hiki cha Barabara chenye urefu
wa kilometa 50 na mkandarasi, Kampuni ya CHICO inafanyakazi vizuri na
tuna imani kwamba ujenzi wa barabara hii utakamilika ifikapo mwezi
Oktoba, 2019 kama mkataba unavyoonesha” alifafanua Mhandisi Athumani.
Kwa
upande wake, Mhandisi Mshauri Mkazi wa mradi huo, Mhandisi Swalihi
Kazuvi amesema kuwa barabara ya Mwigumbi-Maswa-Bariadi na Lamadi,
inayojengwa kwa kiwango cha lami, yenye urefu wa kilometa 172,
itakapokamilika, italeta chachu ya maendeleo yanayopitiwa na barabara
hiyo.
“Kipande
cha barabara ya lami kutoka Mwigumbi mpaka Maswa na kile cha Bariadi
hadi Lamadi vimekamilika kwa hiyo kipande kilichobaki ni hiki
(Bariadi-Maswa), ndio maana unaona magari yanayopita barabara hii ni
mengi licha ya kwamba kipande hiki cha kilometa 50 hakijakamilika,
madereva wanaona afadhali wapite huku kwenda Musoma kuliko kupitia njia
ya Mwanza” aliongeza Mhandisi Swalihi Kazuvi
Lengo
la ziara hiyo ya maafisa wa Serikali ni kufuatilia utekelezaji wa
miradi ya maendeleo inayotekelezawa katika Mkoa huo ili kujua
mafanikio, changamoto na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.
No comments:
Post a Comment