Bodi ya ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA) imetembelea eneo la Mradi wa ujenzi wa Maghala na Vihenge vya
kisasa Mkoani Manyara na kuipongeza kampuni ya Unia Araj Realizacje Sp.o.o)
chini ya msimamizi wa utekelezaji wa mradi huo ambaye ni Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA) kwa kasi waliyoanza nayo ya ujenzi.
Kampuni hiyo ambayo imeanza ujenzi huo tarehe 15
Disemba 2018 katika Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara katika kipindi
hicho imetekeleza mradi huo kwa kasi nzuri, Imesema Bodi hiyo.
Mradi huo katika Kanda ya Arusha (Babati), pamoja
na Dodoma, Makambako, Mbozi, Shinyanga, Songea, Sumbawanga na Mpanda.
utagharimu Dola za Kimarekani Milioni 55, ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu
kutoka Serikali ya Poland ikiwa ni sehemu ya kiasi cha milioni 110
kilichotolewa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na mkandari wa mradi huo Mwenyekiti wa
Bodi ya ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Mhandisi
Eustance Kangole alisema kuwa kampuni hiyo inapaswa kuongeza kasi zaidi ya
ujenzi ili kukamilisha kwa muda uliopangwa.
Alisema kuwa Hifadhi ya Chakula inayohitajika
kukidhi mahitaji ya dharula kwa miezi mitatu ni zaidi ya tani 500,000
ukilinganisha na tani 150,000 iliyokuwa inahitajika miaka ya 1992 Wakala
ulipoanzishwa.
Pia, technologia ya vihenge itawezesha Wakala kutumia
teknolojia ya kisasa na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji, Itawezesha
Wakala kuhifadhi chakula kwa muda mrefu Zaidi, itasaidia kupunguza upotevu wa
zao la mahindi baada ya kuvuna (posthaverst loss) na kuongeza soko la mahindi
nchini na kuimarisha usalama wa nafaka inayohifadhiwa kwa kudhibiti sumukuvu
(Aflatoxin) kwa mahindi yaliyohifadhiwa.
Bodi ya ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Eustance Kangole
na katibu wake ambaye pia ni Kaimu Afisa Mtendaji mkuu wa Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bi Vumilia L. Zikankuba imefanya ziara hiyo mara
baada ya kikao kazi cha 33 cha Bodi hiyo Jijini Dodoma kilichofanyika kwa lengo
la kujadili masuala muhimu ya Wakala ikiwemo utekelezaji wa mkataba wa mauzo ya
mahindi Tani 36,000 kwa Shirika la Chakula Duniani (WFP) sambamba na kujadili
maendeleo ya Mradi wa Vihenge na Maghala ya kisasa.
Vihenge 8 vinatarajiwa kujenzgwa Kanda ya Arusha
katika eneo la (Babati) vyenye uwezo wa kuhifadhi nafaka Tani 25,000 ambapo pia
yatajengwa maghala 2 yenye uwezo wa kuhifadhi nafaka Tani 15,000 hivyo kuwa na
jumla ya Tani 40,000.
Baada ya mradi kukamilika Wakala utakuwa umeongeza
uwezo wa kuhifahi kwa Tani 250,000 zaidi (vihenge vya kisasa 190,000 MT na maghala
60,000 MT) jambo ambalo litakuwa chachu na mafanikio yenye tija katika kuunga
mkono Juhudi za utendaji wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.
Kupatikana kwa Mradi huo nchini ni jitihada za
Serikali ambazo zitapelekea ukuaji wa uchumi nchini na kuchangia kuwezesha
Tanzania ya viwanda ambapo kutawezesha maghala ya Wakala kuweza kuhifadhi akiba
ya Chakula ambayo itaendana na mahitaji halisi ya dharura kulinganisha na
ongezeko la watu nchini.
Wajumbe
wa Bodi ya ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
wakikagua eneo la Mradi wa ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa
Mkoani Manyara unaojengwa na kampuni ya Unia Araj Realizacje Sp.o.o)
chini ya msimamizi wa utekelezaji wa mradi huo ambaye ni Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA). (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
No comments:
Post a Comment