Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mwenyekiti wa Kampuni ya Touchroad
Group ya China, Bw. He Liehui, ofisini kwa Waziri Mkuu, jijini Dodoma
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa Kampuni ya
Touchroad Group ya China, Bw. He Liehui, ofisini kwa Waziri Mkuu, jijini
Dodoma.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameahidi kupokea kundi la watalii wasiopungua 300
ambao wanatarajiwa kuwasili nchini Machi, mwaka huu.
Watalii
hao ni kundi la kwanza miongoni mwa watalii 10,000 wanaotarajiwa
kuwasili nchini katika mwaka 2019 chini ya mpango unaosimamiwa baina ya
Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania na kampuni ya
TouchRoad International Holding Group ya China.
Ametoa
ahadi hiyo leo (Jumamosi, Januari 19, 2019) alipokutana na Mwenyekiti
wa Touchroad Group, Bw. Liehui He na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji
Thomas Mihayo ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.
Waziri
Mkuu amefikia uamuzi huo baada ya kuelezwa na Bw. He huyo kwamba kundi
hilo la watalii likiwa Djibouti litapokelewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo
na likienda Zimbabwe, litapokelewa na Rais wa nchi hiyo.
“Tanzania
imeamua kuweka mkakati wa kuongeza idadi ya watalii nchini kwa
kuboresha miundombinu ya usafiri na kukuza utalii kupitia vivutio vya
vyakula vya asili, mavazi ya asili, wanyama, fukwe za bahari na milima.
Kwa hiyo, ujio wa kundi hili kubwa, unatoa fursa mpya ya kutangaza
vivutio vya nchi yetu,” amesema.
“Nitoe
wito kwa Watanzania wanaoishi maeneo ya jirani na vivutio vyetu,
wachangamkie fursa ya ujio wa watalii hawa katika maeneo mbalimbali.
Wakifika Dar es Salaam, wanaweza kwenda Kigoma kuona Ziwa Tanganyika,
mbuga zilizoko Nyanda za Juu Kusini, Arusha au vivutio vya Zanzibar.
Tujiandae, tuwe tayari kuwauzia bidhaa mbalimbali,” amesema.
Pia
amesema amefurahishwa na wazo lao la kuifanya Dar es Salaam iwe kitovu
cha utalii (tourist hub) kwa makundi ya watalii ambayo yatakuja Tanzania
na baadaye kutoka Tanzania kwenda Lusaka, Harare, Johannesburg na
Djibouti.
Mwenyekiti
huyo ambaye aliwasili nchini juzi, ameambatana na ujumbe wa watu 31
ambao unajumuisha waandishi wa habari, wasanii, wanamuziki na watu
mashuhuri.
Akiwa
Beijing, China, wakati akishiriki mkutano wa Jukwaa la Biashara baina ya
Tanzania na China lililofanyika Septemba mwaka jana, Waziri Mkuu
alikutana na uongozi wa kampuni ya TouchRoad ambayo ilionesha nia ya
kutangaza fursa za utalii zilizopo hapa nchini.Ziara
ya Bw. He ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano yaliyoingiwa kati ya
kampuni ya TouchRoad na Bodi ya Utalii ya Tanzania, Novemba 2018.
Mapema,
Bw. He alimweleza Waziri Mkuu nia ya kampuni hiyo kutekeleza
makubaliano yao ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika soko
la China ili kuvutia watalii wapatao 10,000 waitembelee Tanzania katika
mwaka 2019.
“Tumepanga
kuleta watalii 10,000 kwa mwaka huu wa 2019 na tumeweka lengo la
kuongeza idadi hiyo kwa asilimia 20 kila mwaka kwa muda wa miaka mitano.
Pia tuna lengo la kuitumia ndege ya ATCL ili ilete watalii moja kwa
moja kutoka Shanghai, China,” alisema.Akielezea
ujio wa kundi la kwanza la watalii, Bw. He alisema kundi hilo litakaa
Djibouti kwa siku moja, Tanzania siku nne (tatu za kulala) na Zimbabwe
siku tatu (mbili za kulala) na kisha kurejea China.
Alisema
wanapanga kila mwezi wawe na kundi kubwa la watalii ambao watakuwa
wanafikia Tanzania na kupelekwa nchi nyingine kwa sababu Wachina wengi
hupenda kufanya utalii kwa siku walau 10, lakini wapelekwe maeneo matatu
au manne tofauti kuona vivutio vya aina nyingine badala ya kukaa sehemu
moja kwa kipindi chote hicho.
“Watalii
hawa wakija kwa siku tatu au nne, wana uhakika wa kutumia dola za
Marekani zaidi 2,000, wakienda eneo jingine watatumia fedha pia, namna
hiyo tuna uhakika wa kuongeza pato la Taifa, lakini pia tuna uhakika wa
kutengeneza ajira kwa Watanzania,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA,
JUMAMOSI, JANUARI 19, 2019.
No comments:
Post a Comment