Rais
wa Taasisi inayosimamia mazingira ya Umoja wa Mataifa Bwana Siim Valmar
Kiislar amesema wakati umefika kwa Mataifa yote Ulimwenguni kuwa na
mfumo Mmoja unaoeleweka wa utunzaji wa Mazingira utakaosaidia kuifanya
Dunia iendelee kubakia salama.
Alisema
tabia ya baadhi ya Mataifa kuendelea kukwepa mikataba na baadhi ya
kanuni zinazowekwa Kimataifa pamoja na kuweka vikwazo vyenye nia ya
kulinda maslahi yao binafsi vitapelekea kuongezeka kwa wasi wasi
utakaoifanya Dunia hii ibakie katika mazingira hatarishi.
Bwana
Siim Valmar Kiislar alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Ofisi yake iliyomo
ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi liliopo Chukwani nje kidogo ya
Mji wa Zanzibar.
Rais
huyo akiuongoza Ujumbe mzito wa Taasisi hiyo ya Mazingira ya Umoja wa
Mataifa amekuja kushuhudia uzinduzi wa Kampeni ya Kidunia ya uzinduzi wa
usafi wa Mazingira katika Fukwe ya Forodhani Visiwani Zanzibar
ulioambatana na ujio la Mashua ya Mazingira iliyotengenezwa kutokana na
malighafi ya Plastiki kutoka Nchini Kenya.
Bwana
Siim Valmar ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na Wananchi wake kwa umakini wao wa kusimamia masuala ya
Mazingia katika kuitikia kampeni ya Kimataifa ya kupambana na mabadiliko
ya Tabia Nchi.
Alisema
kitendo cha Zanzibar kufanikiwa katika mapambano yake ya kupiga
marufuku matumizi ya mifuko ya Plastiki mbali ya kuwa mfano kwa Mataifa
ya Ukanda wa Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika, lakini pia kimeleta
faraja kwa Umoja wa Mataifa kupitia Taasisi yake hiyo inayosimamia
masuala ya Mazingira.
Naye
Mratibu Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayofanya kazi Nchini
Tanzania Bwana Alvaro Rodriguez alisema bado Mataifa Ulimwenguni yana
wajibu wa kushirikiana katika mapambano yake dhidi ya uchafuzi wa
Mazingira.
Bwana
Alvaro alisema ustawi wa Jamii pamoja na viumbe vilivyomo ndani ya
Dunia vitaendelea kuishi kwa amani bila ya vikwao endapo ushirikiano huo
utaimarishwa na kuendelea kuwa wa kudumu kama inavyoonekana katika
baadhi ya maeneo.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alisema Zanzibar bado inaendelea kuathirika na mabadiliko ya Tabia Nchi
akatolea mfano ufukwe wa Bahari ya Msuka uliopo kaskazini mwa Kisiwa cha
Pemba ambao tayari umeshaliwa na mawimbi ya Bahari kwa sehemu kubwa.
Balozi
Seif aliueleza Ujumbe huo wa Taasisi ya Umoja wa Mataifa unaosimamia
Mazingira kwamba Zanzibar imeanza mikakati ya kupiga marufuku matumizi
na uingizwaji wa Mifuko ya Plastiki tokea mwanzoni mwa Miaka ya 90 na
kufanikiwa vyema katika azma yake ya kulinda mazingira.
Rais
wa Taasisi inayosimamia mazingira ya Umoja wa Mataifa Bwana Siim Valmar
Kiislar kiipongeza Zanzibar kwa mapambano yake ya kusimamia vyema
mazingira alipokuwa akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi kwenye Jengo la Baraza la Wawakilishi Chukwani.
Balozi
Seif Ali Iddi Kulia akisisitiza jambo wakati akizaungumza na Bwana
Siim Valmar Kiislar aliyewasili Zanzibar kushuhudia Uzinduzi wa usafi wa
mazingira Kidunia katika Fukwe ya Forodhani.
Balozi
Seif Kulia na Mgeni wake Rais wa Taasisi inayosimamia mazingira ya
Umoja wa Mataifa Bwana Siim Valmar Kiislar wakitoa nje ya Ofisi baada ya
kumaliza mazungumzo yao.
Bwana
Siim Valmar Kiislar kati kati akibadilishana mawazo na Balozi Seif
baada ya mazungumzo yao huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akishuhudia.
Balozi
Seif wa Nne kutoka Kulia akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya
Uongozi wa Juu wa Taasisi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Mazingira nje
ya Jengo la Baraza la Wawakilishi baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Kulia ya Balozi Seif ni Rais wa Taasisi hiyo Bwana Siim Valmar Kiislar,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed
Aboud Mohamed, Mratibu Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mtaifa Nchini
Tanzania Bw. Bwana Alvaro Rodriguez na Ofisa wa Uratibu katika masuala
ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Bibi Clara Makenya.
Kutoka Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Zanzibar Bibi Farhat
Farhat Ali Mbarouk na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki Balozi Mohamed Haji Hamza. Picha na – OMPR – ZNZ.
No comments:
Post a Comment