Mawaziri
saba wametembelea Kijiji cha Kimotorok Wilayani Simanjiro Mkoani
Manyara kwa ajili ya kutatua mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa eneo
hilo na hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero.
Pia mawaziri hao wamesikiliza mgogoro wa ardhi wa kijiji cha Irkushbor
cha wilayani Kiteto na hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la
Mkungunero.
Mwenyekiti
wa mawaziri hao, William Lukuvi ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema wametumwa na Rais John
Magufuli kusikiliza mgogoro huo.
Waziri
Lukuvi alisema baada ya kupokea mapendekezo ya namna ya kumaliza
mgogoro huo kutoka pande zote watafikisha suala hilo kwa Rais Magufuli
ili atoe maamuzi.
Alisema
wamepokea maoni kutoka kwa wananchi wa vijiji hivyo, viongozi wa
serikali ngazi ya mkoa na wilaya, wabunge, hifadhi ya Taifa ya Tarangire
na pori la akiba la Mkungunero.
"Baada
ya kupokea mapendekezo haya kwa njia ya maandishi na maoni ya mdomo
tumeandika na tutayapeleka kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri na kisha
aliyetutuma atayatolea maamuzi," alisema Lukuvi.
Mawaziri
saba waliofika Simanjiro ni Lukuvi, Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo,
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Luhaga Mpina, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein
Mwinyi, Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba na Naibu Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Sima.
Akizungumza
mbele ya Mawaziri hao saba, Mnyeti alisema amekagua nyaraka zote
zilizopo kwenye mkoa huo lakini hajakuta sehemu inatamkwa kuwa pori la
akiba la Mkungunero lipo Manyara.
Mnyeti
alisema baadhi ya wafugaji wa kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro
na Irkushbor wilayani Kiteto wanafukuzwa mara kwa mara na
wakanyang'anywa mifugo yao zaidi ya 600.
Mbunge
wa jimbo la Simanjiro, James Ole Millya alisema wananchi hao
wamenyanyasika vya kutosha kwani kila wakati wanafukuzwa na kuambiwa
wapo hifadhini.
Ole
Millya alisema ni wakati sahihi wa kuweka mpaka ili ijulikane mwisho wa
wafugaji hao na hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la
Mkungunero, kuliko mpaka wao kusogezwa kila wakati.
"Kwa
sababu mmekuja na helkopta mnaweza kupita juu na kuona mifugo yetu
ng'ombe na mbuzi zinachungwa pamoja na wanyamapori wakiwemo tembo,
pumbamilia, swala na nyumbu sisi wamasai ni wahifadhi wazuri," alisema
Ole Millya.
Diwani
wa kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga (Mardad) alimshukuru Rais John
Magufuli kwa kuwajali na kuwatetea wafugaji na wakulima nchini.
Mardad
alisema hivi sasa wafugaji na wakulima wa eneo hilo wanalishia mifugo
yao na kulima sehemu ambazo walikuwa wanazitumia miaka iliyopita kabla
ya kuondolewa kwa kudaiwa wapo sehemu ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire
na pori la akiba la Mkungunero.
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akizungumza na
wananchi wa Kijiji cha Kimotorok Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara baada
ya kufika eneo hilo.
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akizungumza mbele ya Mawaziri saba
waliofika kusikiliza mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa Vijiji vya
Kimotorok Wilayani Simanjiro na Irkushbor Wilayani Kiteto na hifadhi ya
Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero.
Mbunge
wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya akizungumza huku
amefunga shuka ya kimasai juu ya manyanyaso waliopata wananchi wa
Kijiji cha Kimotorok kutokana na mgogoro wa ardhi na hifadhi.
No comments:
Post a Comment