Na Lusungu Helela-WMU
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Mhe.
Constantine Kanyasu amewahakikishia wamiliki wa viwanda vya misitu
Tanzania kuwa atashughulikia ombi lao la kutaka kuongezewa muda wa
mikataba yao kutoka miaka miwili hadi mitano ya kupewa mgao wa vitalu
vya miti
Pia ameahidi kuyafanyia kazi malalamiko
mbalimbali yaliyowasilishwa ofisini kwake na wamiliki hao yakiwemo ya
gharama za tozo ya ushuru wa mazao ya misitu (Cess) inayotozwa
na Halmashauri za wilaya ya Mufindi ambayo licha Serikali kutoa
maagizo ya kuzuia tozo hiyo bado wadau hao wanaendelea kutozwa.
Mhe. Kanyasu ameyasema hayo alipokuwa
akizungumza na Rais wa Shirikisho la Viwanda vya Misitu Tanzania
(SHIVIMITA) na Wanachama wa Shirikisho hilo waliomtembelea ofisini
kwake jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Rais wa
SHIVIMITA, Ben Sulus amemuomba Naibu Waziri aangalie namna ya
kuwasaidia wadau hao waongezewe muda wa mikataba kutoka miaka miwili
hadi mitano ya kupewa mgao wa vitalu vya misitu ili waweze kupata mikopo
kutoka kwenye Taasisi za Kifedha kwa ajili ya kuendeshea viwanda vyao
Rais huyo ameeleza kuwa Taasisi za
Kifedha zimekuwa zikiwanyima mikopo kwa kuhofia fedha zao kupotea
kutokana na wadau hao kutokuwa na uhakika wa kuongezewa mikataba mara
baada ya mikataba yao ya kuvuna magogo ya miaka miwili waliyopewa na
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS).
Amesema endapo watapewa mikataba ya
miaka mitano watakuwa na uhakika wa kuweza kuendeleza viwanda vyao kwa
vile Taasisi hizo za Kifedha zitaweza kuwapa mikopo watakayoomba na
zitakuwa na uhakika wa kurudishiwa fedha hizo.
Katika hatua nyingine, Wadau hao
wamemuomba awe mlezi wao katika jitihada wanazozichukua za kuhakikisha
wanakuwa wazalishaji wa bidhaa za mwisho kama vile milango pamoja na
meza zitokanazo na mbao badala ya kujikita kuuza mbao tu.
No comments:
Post a Comment