Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema
kuanzia sasa gharama za urasimishaji haitazidi shilingi 150,000 badala
ya 250,000 iliyopangwa awali na makampuni yatakayoenda kinyume
yatachukuliwa hatua ikiwemo kufutwa.
Lukuvi alitoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokutana na
Makampuni ya Upangaji na Upimaji yanayofanya kazi ya urasimishaji
katika mitaa mbalimbali nchini pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, baada ya Wizara yake kuona zoezi la urasimishaji
linasuasua wamegundua asilimia 30 pekee ndiyo iliyorasimishwa tangu
kuanza zoezi hilo na hali hiyo imechangiwa na uwezo mdogo wa wananchi
wengi kumudu gharama za urasimishaji.
Waziri Lukuvi alisema, alichotegemea kwa makampuni yaliyopewa kazi ya
urasimishaji ni kuwa na uzalendo kwa kushusha gharama lakini
yameshindwa kupunguza gharama jambo lililoifanya serikali kuona haja
ya kupitia upya gharama hizo na kubaini gharama za msingi ili
kumuwezesha mwananchi kupata hati na kusisitiza punguzo hilo
halitawahusu waliolipia gharama za urasimishaji.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameyataka makampuni
yanaoyoendesha zoezi la urasimishaji kuhakikisha kiasi cha fedha
inachowatoza wananchi kinaishia hatua ya Hati na gharama itakayolipwa
na mwananchi baada ya kurasimishwa ni kodi ya ardhi na
kuyatahadharisha kutochukua muda mrefu kukamilisha zoezi hilo.
No comments:
Post a Comment