Kutokana na utabiri uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu
kutokea kwa Kimbunga kikali (KENNETH) na mvua kubwa leo tarehe 25 Aprili
2019 kitakachoathiri maeneo ya Pwani ya Kusini mwa nchi na kusababisha
madhara mbalimbali. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatoa rai kwa Wananchi
wote waishio katika maeneo hatarishi, maeneo yaliyopo pembezoni mwa bahari
na kandokando ya Mito, kuchukua tahadhari katika kipindi hiki kwa kuyahama
maeneo hayo haraka.
Wananchi wanatahadharishwa kuchukua tahadhari katika kipindi hiki na
kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka Hali ya Hewa Tanzania na
kusikiliza vyombo vya habari pamoja na kuzingatia tahadhari zinazotolewa,
ushauri na miongozo ya kitaalam ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Tuchukue tahadhari kwa kuepuka kukaa au kuegesha vyombo vya Usafiri na
Usafirishaji chini ya miti mikubwa, maana matawi au mti vyaweza kuangukia
chombo na kusababisha uharibifu mkubwa wa Mali hata kudhuru Maisha.
Kutokana na Kimbunga hiki kikali kinachoambatana na mvua kubwa kuna
uwezekano wa mawe makubwa au udongo kuporomoka kutoka milimani au miti
kuanguka na kuziba barabara, hivyo madereva wanapaswa kuwa makini kwa
kuendesha vyombo kwa mwendo unaokubalika ili kuepuka ajali zisizo za lazima.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limejipanga na liko imara kuhakikisha linatoa
huduma bora, sahihi na kwa wakati.
Imetolewa na;
Billy Mwakatage
Kamishna wa Operesheni
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
No comments:
Post a Comment