Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amevitaka vyombo ya habari
vya Nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania kutangaza na kuandika habari za
kweli ili kujitofautisha na vyombo vya Nje ya Bara hilo ambavyo upotosha na
kubeza kwa makusudi mambo mazuri yanayotekelezwa na yaliyotekelezwa na Nchi za
Afrika.
Akizungumza katika
kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Mawasiliano Barani Afrika leo Ijumaa (Mei 24,
2019) Jijini Dar es Salaam, Dkt. Mwakyembe alisema vyombo vya Habari vya Afrika
havina budi kuonyesha udhubuti kwa kuweka sera zinazoakisi maendeleo na kuyatangaza
kwa Wananchi wake na wote waliopo nje ya Bara hilo.
Dkt. Mwakyembe
alisema sehemu kubwa ya maudhui ya Vyombo vya Habari vilivyopo nje ya Bara la
Afrika vinavyoongozwa na Wakoloni waliowahi kutawala katika Bara la Afrika
hawapendi kuona Nchi za Afrika zinapiga hatua za Maendeleo kwa wananchi wake na
badala yake hupenda kuripoti na kutangaza mambo mabaya yanayohusu Afrika
ikiwemo njaa, magonjwa, vurugu za kisiasa, vita n.k.
Aidha Dkt. Mwakyembe
alisema yapo mambo mazuri ya Maendeleo yanayofanyika katika Nchi za Bara la
Afrika ikiwemo Tanzania ambayo zimepiga katika kipindi cha miaka minne imepiga
hatua kubwa katika Maendeleo ya kiuchumi, na miundombinu, jambo ambalo baadhi
ya vyombo vya habari vya Mataifa ya Nje ya Afrika yamekuwa hayapendi
kuyatangaza, hivyo ni wajibu wa vyombo
vya habari kutumia majukwaa yao kutetea na kutangaza mafanikio hayo.
“Wakati Hayati
Mwalimu Julius Nyerere na Kenneth Kaunda wa Zambia walipoamua kujenga Reli ya
Tazara, walipingwa vikali sana Wakoloni waliotuwala na wengine waliita reli ile
kuwa ni bamboo (mianzi) lakini ni taifa moja tu la Serikali ya Jamhuri ya Watu
wa China walitusaidia na leo hii reli ile ndiyo ndefu zaidi katika Bara la
Afrika yenye urefu wa kilometa 1860” alisema Dkt. Mwakyembe.
Kwa mujibu wa Waziri
Mwakyembe alisema Maendeleo ya Bara la Afrika yatatetewa na kupiganiwa na Wafrika
wenyewe, hivyo ni wajibu wa vyombo vya habari vya Bara hilo kujitokeza na
kutetea Maendeleo hayo na kamwe haitatokea siku moja chombo cha habari cha BBC
au CNN vikatangaza mafanikio hayo kwani hawapendi kuona Mataifa waliyoyatawala
yakifikia hatua kubwa za kimaendeleo.
Akifafanua zaidi Dkt.
Mwakyembe aliwataka Vijana wa Nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania kujifunza
historia ya Bara lao ili kuweza kufahamu wapi walipotoka na wapi wanapoelekea badala
ya kupenda kulalamika pasipo na kuweka mikakati ya namna bora ya kupiga hatua
za kujietea Maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.
Waziri Mwakyembe
alisema ni wajibu wa Taasisi mbalimbali za Habari na Mawasiliano zilizopo
katika Bara la Afrika kujenga mifumo imara ya mawasiliano ikiwemo kutumia vyema
mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuchapisha habari zinazohusu masuala ya maendeleo
badala ya kutumia majukwaa hayo kuandika mambo yasiyo na faida wala tija kwa mataifa
yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, alisema
Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za mawasiliano katika
sekta binafsi ili kuhakikisha kuwa wanajenga daraja moja katika kusukuma mbele
gurudumu la Maendeleo ya sekta ya habari na Mawasiliano nchini.
Naye Rais wa Chama
cha Maafisa Uhusiano wa Sekta binafsi Tanzania (PRST) Loth Makuza alisema, taasisi
hiyo ni jukwaa huru linalotoa fursa na nafasi ya kujadili masuala mbalimbali ya
mawasiliano nchini ikiwemo changamoto na utatuzi wa masuala mbalimbali
yanayohusu sekta ya habari na mawasiliano nchini.
Anaongeza kuwa
Taasisi hiyo kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano imeweza kutengeneza
majukwaa mbalimbali yanayotangaza masuala mbalimbali ya kimaendeleo
yaliyofikiwa katika Nchi za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania, lengo likiwa ni
kubadili mtazamo hasi wa Bara la Afrika katika nyanja za kiuchumi, kijamii kupitia
ngazi ya kimataifa na duniani kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment