Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewatoa
hofu wananchi kufuatia zoezi linaloendelea la kupanga matumizi bora ya
ardhi katika wilaya kumi nchini hasa katika maeneo yanayopakana na
Hifadhi za Taifa kuwa zoezi hilo halina mpango wowote wa kunyang'anya
ardhi ya wananchi kwa ajili ya kuanzisha Jumuiya ya Hifadhi ya
Wanyamapori.
Rai hiyo imetolewa leo na Mhe. Constantine Kanyasu kufuatia hofu
kubwa iliyokuwa imetanda miongoni mwa wananchi wa vijiji 8
vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wilayani Bunda mkoani
Mara ambapo moja ya madai yao ni kwamba zoezi hilo limelenga kuchukua
maeneo yao ya malisho kwa ajili ya kuanzisha Hifadhi ya Jumuiya ya
Wanyamapori jambo ambalo sio kweli.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Sarakwa kinachotenganishwa kati
ya mto Rubana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti , Mhe.Kanyasu
amewaeleza wakazi hao kuwa zoezi la kupanga matumizi bora ya ardhi
katika maeneo hayo lina faida kubwa ikiwemo kuepusha migogoro wa ardhi
inayotokea mara kwa mara miongoni mwao.
Amesema mpango wa matumizi bora ya ardhi ni zoezi la kitaifa ambalo
limelenga kutenga maeneo maalum kwa ajili ya malisho, kilimo pamoja na
shughuli za maendeleo kwa malengo yakuepusha migongano inayotokea
sehemu mbalimbali nchini na si kunyang'anya ardhi mpya kama
inavyodaiwa.
"Nataka niwahakikishie Wizara yangu haina mpango wa kuanzisha msitu wa
Hifadhi wala Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika kijiji chenu,
Huu ni uzushi upuuzeni" Alisisitiza Kanyasu.
Aidha, Mhe.Kanyasu amewaeleza wananchi hao kuwa mpango wa matumizi
bora ya ardhi utasaidia kuepusha watu wachache kujimilikishia eneo
kubwa,"kinachofanyika kwa sasa ni kuweka rekodi na nyaraka kwa ajili
ya vizazi vyenu" Alisisitiza.
Amesema katika zoezi hilo la mpango wa matumizi bora ya ardhi
wanachoweza kufanya ni kutenga eneo la msitu asili wa kijiji kwa ajili
ya manufaa yao ikiwemo kuokota kumi na eneo litakuwa chini ya umiliki
wa kijiji na sio serikali kuu.
Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewatoa wasiwasi wananchi hao kuwa
licha ya kijiji hicho kuingia katika zoezi la mpango wa matumizi bora
ya ardhi mifugo yao haitazuiliwa kwenda kunyweshwa maji katika mto
Rubana.
"Nimesikia baadhi ya watu wakieneza uzushi kuwa baada ya mpango wa
matumizi bora ya ardhi kukamilika hakuna mtu yeyote kupeleka mifugo
katika mto Rubana, huu ni uwongo" alisema Kanyasu
Hata hivyo amewaeleza kuwa mita 500 kutoka katika mto huo ni eneo la
kijiji kwa ajili ya malisho ya mifugo isipokuwa vitu ambavyo
havitaruhusiwa kufanywa na mtu yeyote ni kulima pamoja na kujenga
nyumba kwa vile eneo hilo ni shirikishi kwa Wanyamapori pamoja na
mifugo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bunda vijijini, Boniface Getere amewataka
wananchi kuwa watulivu kwani serikali haina mpango wowote wa
kunyang'anya ardhi badala yake mpango huo utakuwa mkombozi kwa ajili
ya kizazi cha sasa na cha badae.
" Mimi ni Mbunge wenu nisingeweza kukubali hata kidogo kama mpango huu
wa matumizi bora ya ardhi umelenga kunyang'anya ardhi yenu."
Alisisitiza Getere.
Naye, Mwenyekiti wa kijiji cha Sara, Samson Kapeta amekiri mbele ya
Naibu Waziri kuwa mpango wa matumizi bora ni mpango mzuri isipokuwa
kumejitokeza vikundi vya watu vilivyolenga kupotosha malengo mazuri
ya serikali kwa ajili ya ardhi yao.
Mpango wa matumizi bora ya Ardhi ni mpango unaotekelezwa katika wilaya
kumi nchini kwa ushirikiano katika ya Wizara ya Maliasili na Utalii na
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi kwa kugharamiwa na
Hifadhi ya Taifa ( TANAPA)
NA LUSUNGU HELELA-MARA
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza na
wananchi wa kijiji cha Sarakwa kuhusu umuhimu wa zoezi la mpango wa
matumizi bora wa ardhi unaofanywa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Ardhi katika wilaya
kumi katika wilaya kumi nchini kuwa haujikiti kupokonya maeneo mapya ya
wananchi kwa ajili ya kuanzisha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori kama
inavyodaiwa.
Baadhi
ya wananchi wa kijiji cha Sarakwa wakimsikiliza Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii,Mhe, Constantine Kanyasu akiwaeleza kuwa serikali
inaendesha zoezi la mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya
manufaa ya wananchi.
Mbunge
wa Bunda vijijini, Mhe, Boniface Getere akizungumza na wananchi wa
Sarakwa kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe,
Constantine Kanyasu kuzungumza na wananchi hao kuhusu nia ya serikali ya
kuendesha zoezi la mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kijiji
hicho.
Mratibu wa mipango wa matumizi bora ya ardhi, Rose Mdendemi akitoa
ufafanuzi kwa wananchi wa kijiji cha Sarakwa wilayani Bunda mkoani
Mara kuhusu zoezi linaloendelea la mpango wa matumizi bora ya ardhi
(Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii)
No comments:
Post a Comment