Naibu Waziri wa
Nishati, Subira Mgalu, ametoa Wiki Moja kwa wasimamizi wa mradi wa usambazaji
umeme vijijini mkoani Morogoro kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) na TANESCO kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto ya nguzo za
umeme mkoani Morogoro.
Naibu Waziri alitoa
agizo hilo, tarehe 23 Mei, 2019 mkoani Morogoro wakati alipofanya ziara ya
kukagua kazi ya usambazaji umeme vijijini wilayani Mvomero na Gairo na kuwasha
umeme katika Kijiji cha Dibamba wilayani Mvomero na Kijiji cha Sanganjeru
wilayani Gairo.
Agizo la Naibu Waziri
limekuja baada ya sampuli ya nguzo za mkandarasi wa umeme mkoani Morogoro
kupimwa na wataalam wa TANESCO na kuonekana kuwa hazina vigezo huku mkandarasi huyo akidai kuwa sehemu ya
nguzo zake zinafaa kwa matumizi ya umeme.
Aidha alitoa agizo
kwa wazalishaji wa vifaa vya umeme, wasambazaji na wakandarasi wa umeme
vijijini kutatua changamoto zao kwa haraka mara zinapojitokeza ili kutochelewesha
miradi ya umeme vijijini.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akikata utepe kuashia uwashaji umeme katika Kijiji cha Sanganjeru wilayani Gairo Mkoa wa Morogoro. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe. |
Akieleza kuhusu hatua
zilizofikiwa na Serikali katika kazi ya usambazaji umeme vijijini, alibainisha
kuwa hadi sasa asilimia 57 ya vijiji nchini tayari vimesambaziwa umeme kati ya
Vijiji 12,268 huku kazi hiyo ikiendelea na kwamba Tanzania ndiyo inayoongoza
katika nchi za Afrika Mashariki kwa usambazaji umeme vijijini.
" Wakati
Serikali ya Awamu ya Tano, inaingia madarakani ilikuta vijiji 8783 havina umeme kati ya Vijiji 12,268, ndio
ikaanza safari ya kufikisha umeme kwenye vijiji hivyo kupitia miradi mbalimbali
ikiwemo huu wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza, mradi wa ujazilizi Awamu
ya Pili mzunguko wa kwanza na miradi mingine," alisema Mgalu
Kuhusu bei ya umeme
aliendelea kusisitiza agizo la Serikali kuwa ni elfu 27,000 tu, awe anasambaza
mkandarasi wa umeme vijijini au TANESCO ili kuleta usawa wa utoaji huduma kwa
wananchi. Na Teresia Mhagama
No comments:
Post a Comment