Matokeo chanyA+ online




Wednesday, May 29, 2019

VIONGOZI NA WATUMISHI WA WIZARA YA MADINI WATAKIWA KUWA WAADILIFU KATIKA UTENDAJI KAZI WAO

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akifungua mafunzo ya viongozi wa Wizara ya Madini katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma.
 Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya viongozi wa Wizara ya Madini wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) (hayupopichani) katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akikabidhi cheti cha ufanyakazi bora kwa mmoja wa wafanyakazi bora wa Wizara ya Madini, Bi. Asteria Muhozya baada ya ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi wa Wizara ya Madini katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Madini, Dotto Biteko (Mb) (kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila (wa pili kutoka kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu Wizara ya Madini  Bw. Issa Nchasi (kulia).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) na Waziri wa Madini, Dotto Biteko (Mb) wakifurahia jambo baada ya ufunguzi mafunzo kwa viongozi wa Wizara ya Madini katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma.Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu Wizara ya Madini  Bw. Issa Nchasi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) amewataka viongozi na watumishi wa Wizara ya Madini kuwa waadilifu katika utendaji kazi wao ili Tanzania iweze kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. 
Mhe. Mkuchika ametoa wito huo alipokuwa akifungua mafunzo kwa viongozi wa Wizara ya Madini katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma.

Mhe. Mkuchika amesema kuwa, katika kulenga dira ya pamoja ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 ni lazima viongozi na watumishi wa Wizara ya Madini kufuata misingi ya maadili kama inavyoelezwa katika Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za mwaka 2005.
Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, kutozingatia viapo vya maadili ni kosa kwa mujibu wa sheria.
Mhe. Mkuchika amewataka viongozi wa Wizara ya Madini kuwa mfano wa kuigwa katika kutekeleza kiapo cha uadillifu. 

“Kiongozi unapaswa kuwa mfano katika kutekeleza kiapo chako cha uadilifu, na kama utakuwa umesahau kiapo chako, si vibaya ukaichukua nakala ya kiapo ofisini kwako na kujikumbusha mara kwa mara,” Mhe. Mkuchika amesisitiza.

Mhe. Mkuchika amesema kuwa ni vema watumishi wa Wizara ya Madini hasa wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya uchimbaji madini wawe waadilifu pia ili kuongeza tija na utendaji kazi mzuri.
“Watumishi mlioko kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji, muwe waadilifu na mtangulize uzalendo wa nchi mnapotekeleza majukumu yenu” Mhe. Mkuchika amesema.

Aidha, Mhe. Mkuchika amewataka viongozi na watumishi wa Wizara ya Madini kuepuka vitendo vya rushwa huku akinukuu maneno ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Hayati Koffi Annan.

“Rushwa ni ugonjwa ambao unatafuna taratibu na wenye kuleta madhara katika jamii. Unadhoofisha demokrasia na utawala wa sheria, unaleta uvunjifu wa haki za binadamu, unaharibu hali ya maisha, na kusababisha kuwepo kwa mauaji na mambo mengine yanayotishia usalama wa binadamu” Mhe. Mkuchika amesema.

Katika tukio la ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Mkuchika amekabidhi vyeti vya ufanyakazi bora kwa watumishi 12 wa Wizara ya Madini.
Mafunzo ya viongozi wa Wizara ya Madini yamefanyika lengo ikiwa ni kukumbushana stadi muhimu za kazi, kuwajengea uwezo wa utendaji kazi na kuongeza ari ya utekelezaji wa majukumu yao.

IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 29 MEI, 2019

No comments:

Post a Comment