Wananchi washangilia, waishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma
Changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama iliyokuwa
inawakabili wananchi wa vijiji vya Nandagala ‘B’ na Ingawali wilayani
Ruangwa imekuwa historia baada ya Ubalozi wa Uturiki kupitia taasisi
yake ya Diyanet kuwachimbia visima virefu.
Visima hivyo viwili vimekabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo
(Jumatatu, Juni 3, 2019) na Muambata wa Ubalozi wa Uturuki
anayeshughulikia masuala ya jamii nchini, Muhammed Cicek. Hafla hiyo
imefanyika katika kijiji cha Nandagala ‘B’.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania na Uturuki
ni nchi rafiki na kwamba Serikali ya Uturuki imekuwa ikishirikiana na
Serikali ya Tanzania katika uboreshaji wa huduma za jamii zikiwemo za
afya, elimu na maji.
Waziri Mkuu baada ya kuvipokea visima hivyo amewataka wananchi wa
vijiji hivyo kupitia kamati zao za maji zihakikishe zinaisimamia
vizuri miradi hiyo na pia wawe wanatoa taarifa za mapato na matumizi
ya kila mwezi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) wilaya ya Ruangwa, Samwel Pyuza ahakikishe huduma
ya umeme inafikishwa katika mradi huo kwa ajili ya kusukuma maji
badala ya kutumia jenereta.
Kwa upande wake, Muambata wa Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia
masuala za jamii nchini, Muhammed Cicek amesema Watanzania na Waturuki
ni ndugu, hivyo amefurahi baada ya wananchi wa vijiji hivyo kupokea
zawadi ya visima hivyo walivyowakabidhi.
Wakizungumza baada ya makabidhiano hayo, baadhi ya wakazi wa kijiji
cha Nandagala ‘B’ wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwasogezea huduma ya maji karibu na
makazi yao.
Mmoja wa wakazi hao Safina Angulupele (63) amesema awali kabla ya
kisima hicho walikuwa wanapata maji kutoka katika kijiji kingine na
pia hayakuwa na uhakika, hivyo uwepo wa kisima kwenye kijiji chao ni
mkombozi kwao.
Naye mkazi mwingine wa kijiji hicho Zainab Issa amesema huduma ya maji
safi na salama ni muhimu kwa maendeleo ya jamii, hivyo anaipongeza
Serikali kwa kuwafikishia huduma karibu na makazi. “Sasa hata sisi
wazee tunaweza kwenda kisimani na kuchota maji.”
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli
ya kumtua mama ndoo, imedhamiria kuwafikishia wananchi wote huduma ya
maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye
makazi yao.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua maji baada ya kukabidhiwa kisima cha
maji cha kijiji cha Nandagala ‘B’ kilichojengwa kwa ufadhili wa Ubalozi
wa Uturuki nchini Juni 3, 2019. Kulia ni Muambata wa Ubalozi wa Uturuki
anayeshughulikia masuala ya jamii nchini, Muhammed Cicek na kushoto ni
Mkurugenzi Mkazi wa Turkish Maarif Foundation, Oguz Hamza Yilmaz. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment