Ili kuhakikisha kuwa kazi ya usambazaji umeme mijini na vijijini
inafanyika kwa kasi na ufanisi katika mwaka wa fedha 2019/20, viongozi
wa Wizara ya Nishati wakiongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani wamefanya Mkutano wa siku moja na watendaji wa TANESCO na
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kujadili masuala mbalimbali
yatakayowezesha lengo hilo linafanikiwa.
Mkutano huo, uliofanyika tarehe 16 Juni, 2019, ulihudhuriwa na Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt.
Hamisi Mwinyimvua, Menejimenti ya TANESCO, REA na Bodi ya REA,
ulijadili kazi zilizofanyika katika mwaka 2018/19 na kujipanga katika
utekelezaji wa majukumu kwa mwaka wa fedha wa 2019/20 unaoanza mwezi
Julai.
Watendaji
kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO wakiwa katika kikao baina ya Wizara
ya Nishati, TANESCO na REA kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Baadhi ya masuala yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho ni upelekaji umeme
viwandani, kuimarisha hali ya umeme katika maeneo yaliyounganishwa na
gridi, kuunganishia umeme Taasisi za umma, kuunganishia umeme maeneo
yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme, bei ya kupeleka umeme vijijini,
ununuzi vifaa vya umeme, utambuzi wa wateja wanaohitaji umeme
viwandani na utambuzi wa wazalishaji wadogo wa umeme.
“ Kimsingi lazima tuhakikishe tunaimarisha huduma za umeme kwa kutatua
kero mbalimbali kama za kukatika kwa umeme na kutowaunganishia umeme
wateja ndani ya muda uliopangwa hivyo lazima tujipange sasa
kukamilisha shughuli zetu kwa ukamilifu ili kuwezesha nchi kuingia
kwenye uchumi wa viwanda.” Alisema Dkt Kalemani
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza wakati wakati wa kikao
baina ya Wizara ya Nishati, TANESCO na REA kilichofanyika jijini Dodoma
na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Suala la upelekaji umeme viwandani, Waziri wa Nishati, amesema kuwa ni
la kipaumbele na ametoa miezi mitatu kwa Mameneja wa TANESCO wa Wilaya
kuwasilisha takwimu ya viwanda walivyoviunganishia umeme kwenye maeneo
yao.
Aidha, amewaagiza kuhakikisha kuwa, wanafanya jitihada za kuunganishia
umeme viwanda vinavyoanzishwa kwenye maeneo yao kabla havijakamilika
kwa kupeleka bili stahiki kwa wenye viwanda ili waweze kufanya malipo
mapema hivyo TANESCO kutoonekana kuwa ni chanzo cha kukwamisha
ufanyaji kazi wa kiwanda.
Watendaji
kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO wakiwa katika kikao baina ya Wizara
ya Nishati, TANESCO na REA kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Kuhusu upelekaji umeme vijijini, Dkt Kalemani amesema kuwa kila
mtumishi wa Wizara, TANESCO na REA lazima atambue kuwa, lengo la
Serikali ni kupeleka umeme katika Vijiji vyote ifikapo Juni 2021 hivyo
ni lazima kila mmoja ahakikishe kuwa hilo linafanikiwa na bei ya
kuunganisha umeme ni 27,000 na Meneja asiyetaka kutekeleza hilo aachie
ngazi.
Aidha, kuhusu Wazalishaji wadogo wa umeme ameelekeza Mameneja wa
TANESCO wilayani kuhakikisha kuwa, wanawatambua wazalishaji hao,
wanawapa elimu, miongozo, wanawasimamia na kuwaingiza katika programu
za uzalishaji umeme.
Watendaji
kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na TANESCO
wakiwa katika kikao baina ya Wizara ya Nishati, TANESCO na REA
kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt.
Medard Kalemani.
Suala jingine lililojadiliwa ni ununuzi wa vifaa vya umeme, ambapo Dkt
Kalemani amesema kuwa mtendaji anapaswa kusimamia utekelezaji wa agizo
la Serikali la kutonunua nje vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini
ili kurahisisha ufuatiliaji wa vifaa hivyo pia kuokoa muda mrefu ambao
ungetumika kusafirisha vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.
Suala la uunganishaji umeme kwa wateja wa muda mrefu pia lilijadiliwa
ambapo Waziri wa Nishati ametoa mwezi mmoja kwa TANESCO kuunganishia
umeme wateja wote waliolipia umeme kwa muda mrefu na bado
hawajaunganishwa na umeme.
Kazi ya kushusha umeme kwenye maeneo yaliyopitiwa na miundombinu ya
umeme ameagiza kuwa, kazi hiyo ianze mwezi wa Saba mwaka huu na
ikamilike ndani ya miezi Sita.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua akizungumza katika
kikao baina ya Wizara ya Nishati, TANESCO na REA kilichofanyika jijini
Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesisitiza
kuhusu upelekaji umeme kwenye Taasisi za umma kama vile Shule,
Zahanati na Visima vya Maji kutokana na umuhimu wake kwa jamii
zinazozunguka maeneo hayo na kuagiza kuwa suala hilo liwekewe mkakati
maalum.
Vilevile amempongeza Waziri wa Nishati kwa kuwa na utaratibu wa vikao
kazi ambavyo vimekuwa na tija katika uendelezaji wa Sekta ya Nishati
nchini.
Watendaji
kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na TANESCO
wakiwa katika kikao baina ya Wizara ya Nishati, TANESCO na REA
kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Nishati, Dkt.
Medard Kalemani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua amempongeza
Waziri wa Nishati kwa Mkutano huo na kuahidi kuwa changamoto
mbalimbali zilizojadiliwa kwenye Mkutano zitafanyiwa kazi.
Aidha, amegiza watendaji wa Taasisi zilizohudhuria Mkutano huo
kutekeleza ipasavyo maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Nishati na
kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga
amemshukuru Waziri wa Nishati kwa kufanya Mkutano huo ambao unasaidia
kuboresha utendaji kazi na kutoa wito kwa TANESCO kuendelea kutatua
changamoto mbalimbali kama za kukatika umeme na kutounganishia umeme
wateja ndani ya muda mfupi.
No comments:
Post a Comment