Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy
Mwalimu amewataka Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa
nchini kuhakikisha wanakua na vifaa vya muhimu vya kutolea huduma za
afya kwa wagonjwa wanaofika Hospitalini kupata matibabu.
Waziri Ummy amesema hayo wakati akifungua mkutano wa viongozi wa
Hospitali za Rufaa za Mikoa unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
chuo cha Mipango Jijini Dodoma.
Waziri Ummy amewataka Waganga Wafawidhi hao kubainisha aina ya vifaa
vya matibabu vinavyotakiwa kupelekwa katika Hospitali zao ili
kuhakikisha mgonjwa anapofika Hospitalini hakosi huduma wakati
anapoenda kupata matibabu.
“Mganga Mfawidhi unatakiwa useme vifaa gani ukivipata utaboresha
huduma, hatutaki mgonjwa afike Hospitali halafu akose huduma, boresha
kwanza kupata vifaa vya msingi kabla ya vile vikubwa kama CT-Scan”.
Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema lengo la Wizara ya Afya chini ya Serikali
ya awamu ya tano ni kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa ili
mwananchi akifika katika Hospitali za Rufaa aseme kweli huduma
zimeboreshwa.
“Lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kila Hospitali ya
Rufaa inakua na huduma za kipaumbele 13 zikiwepo huduma za mama na
mtoto ili kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na magonjwa
mengine ambayo yanaweza kutibiwa bila kumpa rufaa mgonjwa”. Ameongeza
Waziri Ummy.
Kwa upande wake, Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewataka Waganga Wafawidhi wa
Hospitali za Rufaa za mikoa kuhakikisha wanasimamia vizuri ukusanyaji
wa mapato kwa kufunga mfumo utakaotumika kukusanya mapato na kuachana
na makaratasi.
“Tuendelee kuboresha huduma za afya na kusimamia ubora wa huduma
tunazozitoa na kuboresha upatikanaji wa vifaa na kuwa wabunifu
japokuwa tuna changamoto za rasilimali watu ila huduma za kibingwa
ziboreshwe ili kupunguza rufaa za nje”. Amesema Dkt. Ndugulile.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula amewataka
Waganga Wafawidhi hao kuhakikisha wanaripoti taarifa za maendeleo ya
Hospitali na atakayeshindwa kufanya hivyo hataendelea na uongozi. Pia
amewataka Waganga Wafawidhi hao kuwa na ushirikiano ili kufanya sekta
ya afya kuwa ya mfano.
“Tuhakikishe tunaweka mifumo vizuri ya kutoa huduma kwa wahitaji
kuanzia ngazi ya chini kwa kufuata miongozo na mikataba iliyotolewa,
na tufanye kazi kwa ushirikiano bila kujali cheo au nafasi ya mtu”.
Amesema Dkt. Chaula.
Pamoja na hayo katika Mkutano huo Waziri Ummy alizindua muongozo wa
uendeshaji wa Hospitali za Rufaa za Mikoa pamoja na jarida la afya ya
jamii toleo la kwanza.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu
(katikati) akizndua muongozo wa uendeshaji wa Hospitali za Rufaa za
mikoa wakati wa uzinduzi wa mkutano wa Waganga Wafawidhi wa Mikoa
unaoendelea jijini Dodoma. Kushoto Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Grace
Maghembe na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile na kulia ni
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula na Mganga Mkuu wa Serikali
Dkt. Muhammad Kambi.
Waziri
wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alifurahia muongozo wa uendeshaji wa
Hospitali za Rufaa aliouzindua mapema leo, kulia ni Mkurugenzi wa Tiba
Dkt. Grace Maghembe, akipokea muongozo huo kutoka kwa katibu Mkuu Dkt.
Zainab Chaula na katikati ni Naibu waziri Dkt. Faustine Ndugulile
akishuhudia.
Waziri
wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
akionesha jarida la afya ya jamii toleo la kwanza alilozindua wakati wa
ufunguzi wa mkutano wa Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa
unaoendelea jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri Dkt. Faustine
Ndugulile na Kulia ni Katibu wa Afya Dkt. Zainab Chaula.
Viongozi
mbalimbali wa Wizara ya Afya na TAMISEMI wakiongozwa na Waziri wa Afya
Mhe. Ummy Mwalimu wakionesha jarida la afya ya jamii toleo la kwanza
lililozinduliwa leo na Waziri Ummy.
Waziri wa Afya, Mhe Ummy Mwalimu akihutubia Waganga Wafawidhi wa
Hospitali za Rufaa za Mikoa waliofika katika Mkutano unaoanza leo
jijini Dodoma. NA WAMJW-DOM
No comments:
Post a Comment