Na Charles James, MICHUZI TV
Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa kutokomeza vitendo
vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya Wanawake na Watoto kwenye
masoko na kushauri elimu iendelee kutolewa kupitia mikutano ndani ya
Mitaa na Kata.
Hayo
ameyasema leo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi huo ambapo amesema katika
kupambana na vitendo hivyo vya kikatili Serikali imeimarisha utendaji
wa madawati 417 ya jinsia na watoto yaliyopo katika vituo vya Polisi
nchini kwa lengo la kuwezesha huduma stahiki kwa watu wanaofanyiwa
ukatili wa kijinsia.
Mama
Samia ameitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kushirikiana na Jumuiya ya
Tawala za Mitaa ambao ndio waratibu wa mradi huo katika kuhakikisha afua
zinazotekelezwa kupitia mradi huo zinakua endelevu hata pale
utekelezaji wa mradi unapofikia mwisho.
"
Ndugu zangu kila mmoja wetu ana haki ya kupinga na kutokomeza ukatili wa
kijinsia, hivi vitendo havikubaliki na wala haviruhusiwi kisheria.
Yeyote atakayethubutu kumdhalilisha mwanamke au mtoto tutamchukulia
hatua kali.
" Ni
jambo la aibu kuona tunatumia viungo vya wanawake kama matusi, huyu
mwanamke unayemdhalilisha tukumbuke ni kama mama zetu majumbani mwetu,
hatuwezi kuwa na Taifa lenye amani kama tutaruhusu vitendo hivi,
tuungane katika kupiga vita na kutokomeza ukatili wa kijinsia, " amesema
Mama Samia.
Akizungumzia
ombwe la watoto wadogo kufanya biashara kwenye masoko, Mama Samia
amezitaka kamati za masoko kuhakikisha zinashirikiana na mamlaka husika
katika kuzuia watoto kufanya biashara sokoni na badala yake wawahimize
kwenda shule na kuwaripoti wazazi wanaowatuma watoto wao kufanya
biashara.
"
Serikali yenu ya awamu ya tano iliwaahidi elimu bure kwa shule ya msingi
hadi kidato cha nne. Tunapoona watoto wetu hawaendi shule na wanafanya
biashara sokoni tunakua hatumtendei haki Rais wetu Dk John Magufuli kwa
zawadi ya elimu bure aliyotuletea. Tuwazuie watoto kufanya biashara
sokoni na tushirikiane kuwapeleka shule," amesema Mama Samia.
Aidha
katika kutekeleza mradi huo, Mhe Makamu wa Rais amekabidhi Pikipiki 14
kwa ajili ya wataalam wa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Dodoma kwa Kata
za Halmashauri ya Chamwino na kuielekeza Wizara kuendeleza utaratibu huo
wa kupatia wataalamu hao usafiri ili iwe rahisi kwao kuwafikia wanawake
wengi hususani wa vijijini na kuwaunganisha na fursa za kiuchumi.
Kwa
upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Mhe Ummy Mwalimu amemshukuru Makamu wa Rais kwa kuzindua mradi huo
ambao utakua msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya ukatili wa
kijinsia.
" Mhe
Makamu wa Rais kama Wizara tumejipanga katika kuhakikisha tunaongeza
elimu zaidi kwa wananchi iki tuzidi kupunguza wimbi la vitendo hivi,
lengo letu ni kutokomeza kabisa vitendo hivi ili kuwa na Taifa imara
ambalo litakua na mshikamano na amani baina yetu bila kujali huyu ni
Mwanaume au Mwanamke," amesema Waziri Ummy.
Nae
Mwenyekiti wa ALAT Mhe Gulamhafeez Mukadam amesema kuna changamoto
kwenye dira ya pamoja juu ya utokomezaji wa vitendo vya ukatili wa
kijinsia jambo ambalo linaleta athari ya maendeleo ya wanawake na hivyo
kuzorotesha uchumi wa Nchi.
"
Nimpongeze Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Mhe Godwin Kunambi kwa namna
ambavyo amekua msaada kwa akina Mama wa Jiji hili kwa kuwapatia mikopo
inayowawezesha kufanya biashara zao. Serikali za Mitaa jukumu lao ni
kuwawezesha wananchi wao kuzipata fursa.
"
Lakini pia kuna changamoto ya masoko, lugha chafu kwa wanawake sokoni
hizi changamoto zinapaswa kushughulikiwa na kutokomezwa kabisa.
Tukiwawezesha wanawake na kuwaepusha na vitendo vya unyanyasaji tutakua
tunatengeneza Taifa imara na madhubuti na kuweza kufikia azma ya Mhe
Rais ya uchumi wa kati kupitia viwanda," amesema Mhe Mukadam.
Makamu
wa Rais Mhe Mama Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria ufunguzi
wa mradi wa kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya
wanawake na watoto katika maeneo ya masoko. Uzinduzi huo umefnyika
jijini Dodoma.
Wananchi
waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa kutokomeza vitendo vya kikatili
dhidi ya wanawake wakimsikiliza mgeni rasmi ambaye ni Makamu wa Rais Mhe
Mama Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) jijini Dodoma.
Maafisa
Maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino wakiwa na
pikipiki walizokabidhiwa na Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan
jijini Dodoma. Pikipiki hizo zimelenga kuwasaidia katika kuwafikia kundi
kubwa la wanawake ambao wanafanyiwa unyanyasaji wa kijinsia.
No comments:
Post a Comment