Serikali
imesema itawajengea uwezo makandarasi wadogo wanaotumia teknolojia ya
nguvukazi (Labor Based Technology) katika ujenzi na ukarabati wa
matengenezo ya barabara, madaraja na majengo ili kuhakikisha kuwa
wanapata fursa zaidi za kushiriki na kushindana katika kazi zilizotengwa
mahsusi kwa ajili makandarasi hao.
Hayo
yalibainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga,
kwenye kongamano la uhamasishaji na uanzishwaji wa umoja wa makandarasi
na vikundi vinavyotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika ujenzi,
ukarabati wa matengenezo ya barabara uliofanyika mkoani Mbeya katika
Chuo cha Teknolojia Stahiki ya Nguvu Kazi (ATTI) na kuhudhuriwa na
wakandarasi wadogo wadogo zaidi ya 150.
Arch.
Mwakalinga, alisema kuwa Wizara kupitia taasisi zake zinazotekeleza
miradi ya ujenzi itaendelea kutumia sheria na kanuni zilizowekwa ili
kuhakikisha kazi zilizoainishwa kwenye miradi ya ujenzi ikiwemo
ukarabati na matengenezo ya barabara, madaraja na majengo zinafanywa na
makandarasi hao.
"Wizara
imeteua timu ya wataalam kupitia nyaraka mbalimbali za miradi ya ujenzi
ili kuhakikisha asilimia 30 ya fedha zinazolipwa kwenye mikataba
mbalimbali ya ujenzi zinaelekezwa kwa makandarasi wanaotumia teknolojia
ya nguvu kazi", alisema Mwakalinga.
Aliongeza
kuwa upitiaji utafanyika kwa haraka chini ya wataalam hao ambapo
anaamini watafanya kazi hiyo vizuri ili kubainisha vigezo ambavyo
makandarasi hao wamekuwa wakivilalamikia kila siku katika utekelezaji wa
kazi zao ili vifanyiwe kazi.
Aidha
Arch. Mwakalinga, alibainisha kuwa Serikali inatambua makandarasi hao
ni chachu kubwa katika kutatua tatizo la ajira kwa wananchi hususani
maeneo ya vijijini kwani mara nyingi wakandarasi hao hutumia vifaa na
vibarua wanaopatikana katika eneo la mradi.
"Mbali
na kuongeza ajira na kuimarisha usafiri hususani maeneo ya vijijini,
serikali inaelewa fika mnachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi kwa
kodi mnayolipa kupitia kazi mnazozifanya" alisisitiza Mwakalinga.
Alisema
ni jukumu la wakandarasi hao kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na
kuwa na sauti moja katika kufuatilia fursa mbalimbali na maslahi yao na
kupata ufumbuzi wa pamoja wa changamoto zinazowakabili.
Awali
akimkaribisha Katibu Mkuu huyo Mkurugenzi wa Barabara, Mhandisi
Rogatius Mativila, alisema madhumuni ya kikao kazi hicho ni kujadili kwa
pamoja masuala muhimu katika Sekta ya Ujenzi ili kuendeleza na
kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Nguvukazi katika kutekeleza
matengenezo ya barabara, madaraja na majengo bila kusahau sekta nyingine
nchini.
Akiongea
kwa niaba ya makandarasi hao, Bi Aurelia Mtui, alitoa shukrani za dhati
kwa Serikali kwani amekuwa kwenye taaluma hiyo kwa miaka 18 na kwa mara
ya kwanza wamekutana na Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi kuzungumzia
changamoto zao na kuomba maazimio waliyokubaliana katika kikao hicho
yafanyiwe kazi.
Serikali
ilianzisha mpango wa kuendeleza matumizi ya teknolojia ya Nguvukazi
tangu mwaka 2004 na kulingana na takwimu zilizopo hadi kufikia mwezi
Juni 2019 jumla ya Makandarasi 267 walikuwa wamesajiliwa na bodi ya
Usajili wa Makandarasi (CRB) katika madaraja ya kutumia teknolojia ya
nguvukazi.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi),
Arch. Elius Mwakalinga, akifungua kongamano la uhamasishaji na
uanzishwaji wa umoja wa makandarasi na vikundi vinavyotumia teknolojia
stahiki ya nguvu kazi katika ujenzi, ukarabati wa matengenezo ya
barabara lililofanyika katika Chuo cha Teknolojia Stahiki ya Nguvu Kazi
(ATTI) mkoani Mbeya.
Mshiriki
wa kikao kazi cha Makandarasi wanaotumia teknolojia stahiki ya
nguvukazi katika ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara, Bw.
Ambakisye Mwakipesile, akiwasilisha hoja zake kwa Katibu Mkuu Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch.Elius Mwakalinga
(hayupo pichani) katika kongamano lililofanyika katika Chuo cha ATTI
Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya na kushirikisha wakandarasi hao kutoka nchi
nzima.
Mkandarasi
Boniface Mambya, akitoa maoni yake kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch.Elius Mwakalinga (hayupo
pichani) wakati wa kongamano la umoja kwa makandarasi na vikundi
vinavyotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika Ujenzi ukarabati wa
Matengezo ya barabara lililofanyika katika chuo ATTI, Mkoani Mbeya.
Washiriki
wa kongamano la uhamasishwaji wa uanzishwaji wa umoja wa makandarasi na
Vikundi vinavyotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika ujenzi,
ukarabati wa matengezo ya barabara wakipitia baadhi ya makabrasha na
kumsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta
ya Ujenzi), Arch.Elius Mwakalinga (hayupo pichani) lililofanyika katika
Chuo cha ATTI, Mkoani Mbeya.
No comments:
Post a Comment