Na Mwandishi Maalum
Wananchi 1776 wamepata huduma za
ushauri, vipimo na tiba za magonjwa ya moyo bila malipo zinazotolewa na
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwenye maonesho ya 43 ya biashara
ya kimataifa ya Dar es Salaam yanayofanyika katika uwanja wa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere uliopo barabara ya Kilwa.
Wananchi hao waliotembelea banda la
Taasisi hiyo kwa ajili ya kupima afya zao walifanyiwa vipimo vya
magonjwa ya moyo ambapo 448 walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echocardiography), na 1097 walifanyiwa kipimo cha
kuangalia umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiogram – ECG).
Asilimia 60
ya watu waliofanyiwa vipimo walikutwa na uzito mkubwa, asilimia 40
walikutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na asilimia 20
walikutwa na tatizo la kuwa na sukari kwenye damu.
Aidha Taasisi hiyo hadi sasa imetoa rufaa
ya moja kwa moja kwa watu 73 wakiwemo watoto 2 ambao baada ya
kuwafanyia vipimo walikutwa na matatizo ya moyo yanayohitaji kufanyiwa
uchunguzi wa kina na matibabu ya kibingwa .
Akizungumzia mara baada ya kupata huduma
ya matibabu katika banda hilo mkazi wa Shekilango jijini Dar es Salaam
Rehema Abdalah aliipongeza Taasisi hiyo kwa kutoa huduma ya matibabu ya
moyo kwa wananchi bila malipo pamoja na kuwapa kipaumbele wazee
waliojitokeza kwenda kupima afya zao.
“Nawashukuru wafanyakazi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete wanaotoa huduma katika maonesho haya, kutokana na
umri wangu wamenipa kipaumbele cha kufanyiwa vipimo kwa haraka.
Nimekutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na tayari nimepatiwa
dawa kwa ajili ya matibabu,” alishukuru Rehema.
Naye mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es
Salaam Hatibu Rashid ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuwafikiria wananchi
wenye uwezo wa chini kupata nafasi ya kufanyiwa vipimo vya magonjwa ya
moyo na wafanyakazi wa Taasisi hiyo pindi watakapopata nafasi watoe
huduma kama hiyo kwa wananchi waliopo maeneo mbalimbali hapa nchini
hasa vijijini.
Rashid alisema, “Zamani vipimo kama hivi
vilikuwa vinafanyika nje ya nchi tena kwa watu wenye hela. Lakini leo
hii vipimo hivi vinafanyika hapa nchini na tunafanyiwa wananchi wa
kawaida kabisa. Ninaishukuru sana Serikali kwa kuimarisha huduma ya
matibabu ya moyo na ninawaomba wananchi wenzangu watumie maonesho haya
kufika katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya
kupima afya zao bila malipo”,.
Katika maonesho hayo Taasisi hiyo inatoa
bila malipo huduma za ushauri wa lishe bora kwa afya ya moyo, umuhimu wa
kufanya mazoezi, vipimo na tiba za magonjwa ya moyo.
No comments:
Post a Comment