Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Ruvuma uendelee
kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo na kuondoa vikwazo vyote ili
kuvutia wawekezaji zaidi.
“Mkoa
wa Ruvuma kama ilivyo mikoa mingine, unazo fursa ambazo zikiendelezwa,
zitaleta tija na kusaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa
letu. Nitoe rai kwa mkoa uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo
sambamba na kuondoa vikwazo vyovyote vya uwekezaji na biashara ili
kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje,” amesema.
Ametoa
wito huo leo mchana (Alhamisi, Julai 25, 2019) wakati akifungua
Kongamano la Biashara na Uwekezaji mkoani Ruvuma linaloendelea kwenye
uwanja wa Majimaji, Manispaa ya Songea. Pia amezindua Mwongozo wa
Uwekezaji wa mkoa huo.
Amesema
katika ustawi wa uchumi, nchi nyingi hapa duniani zimeweza kukuza
uchumi wao kupitia ujenzi wa viwanda na zikafanikiwa kupunguza umasikini
katika jamii zao. Amezitaja nchi hizo kuwa ni Marekani, China, Japani,
Korea ya Kusini na Ujerumani.
“Tunapaswa
kuiga kutoka wa wenzetu. Ndiyo maana Tanzania pia tunahamasisha ujenzi
wa viwanda kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mikoa ili tulete mageuzi ya
kiuchumi yatakayowezesha upatikanaji wa ajira na hatimaye kuondoa
umaskini,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza:
“Kongamano
hili ambalo kaulimbiu yake ni “Ruvuma itavuma kwa uchumi wa viwanda,
wekeza sasa,” imelenga kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo
mkoani humu, na inajipambanua vema na kuendana na azma ya Serikali ya
awamu ya tano ya kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo
2025.”
Amesema
mchango wa sekta ya viwanda kiuchumi na kijamii nchini ni pamoja na
kuongeza pato la Taifa na kupandisha hali ya maisha ya wananchi;
kusaidia nchi isiyumbe kiuchumi ikizingatiwa kuwa viwanda vingi
havitegemei hali ya hewa kama kilimo; kuboresha urari wa biashara
(improve balance of trade) kwa sababu tija yake ni kubwa na hasa
zikiuzwa bidhaa nyingi nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa
kutoka nje ya nchi.
Amezitaja
faida nyingine kuwa ni kuchangia maendeleo ya sekta nyingine kama za
kilimo, uvuvi, elimu na madini; kutengeneza ajira kwa wananchi;
kuchagiza na kuharakisha maendeleo ya teknolojia na rasilimali watu na
kuwezesha matumizi mazuri ya maliasili zilizopo kwa faida zaidi.
Nyingine
ni kuleta uhakika wa soko la mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na
madini kwa sababu hutumika kama malighafi na kuwepo kwa uhakika wa
kuingiza fedha za kigeni nchini kupitia mauzo ya bidhaa nje ambapo
husaidia kuagiza mitambo, malighafi na bidhaa nyingine ambazo
hazizalishwi nchini.
Mapema,
akitoa salamu kwa niaba mabalozi wengine, Mwakilishi wa Balozi wa
China, Bw. Xian Bing alisema ana uhakika kuwa kongamano hilo
litafanikiwa kuleta mabadiliko mkoani humo kwa sababu wana bidii ya
kazi.
“Ninaahidi
kuleta wawekezaji kutoka China kwa sababu tunataka waje kuleta
teknolojia mpya, wafanye kazi pamoja na Watanzania na wawafundishe
teknolojia hizo mpya. Tunataka hapa Ruvuma iwe model (mfano) kwa mikoa
mingine,” alisema.
Akielezea
kwa kifupi kuhusu mwongozo uliozinduliwa na Waziri Mkuu, mtafiti kutoka
Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Hoseana Lunogelo
alisema walitumia mfumo shirikishi ili kupata mwongozo unahusisha
wawekezaji wa ndani.
“Mwongozo
huu umezingatia Dira ya Taifa ya 2025 katika kutimiza azma ya Serikali
ya kuwa nchi ya uchumi na viwanda, tumeshirikisha wananchi wa mkoa wa
Ruvuma ili wasibakie kuwa watazamaji,” alisema.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi, baada ya kufungua
maonesho ya viwanda na kongamano la uwekezaji mkoani Ruvuma, Julai
25.2019.. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akimsikiliza Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa
China Tanzania, Bwana Xian Ding, wakati alipoipongeza Serikali ya awamu
ya tano katika kuwaletea wananchi wake maendeleo, kwenye maonesho ya
viwanda na kongamano la uwekezaji,yaliyofanyika katika Mkoa wa Ruvuma,
Julai 25.2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akizindua kitabu cha muongozo wa uwekezaji katika
Mkoa wa Ruvuma, kwenye maonesho ya viwanda na kongamano la uwekezaji
mkoani Ruvuma. Julai 25.2019. Tokea kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje John Ndumbalo na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa amebeba mkaa wa mawe, wakati akikagua
mabanda kwenye banda la TANCOAL, katika maonesho ya viwanda na
kongamano la uwekezaji mkoani Ruvuma, Julai 25.2019. Tokea kushoto ni
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme na kulia ni Mkuu wa Jiolojia
TANCOAL.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia mkaa wa mawe, uliyotengenezwa kwa
ajili ya matumizi ya nyumbani na wajasiriamali wa kikundi cha Mbalawala
Women Group, wakati akikagua mabanda kwenye maonesho ya viwanda na
kongamano la uwekezaji mkoani Ruvuma, Julai 25.2019. Tokea kulia ni
Meneja wa Fedha wa kikundi hicho, Esta Silas na Msimamizi wa Mradi,
Hajra Yakub.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Christina Mndeme (kushoto), akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya
Mbinga Coffee Curing Company, kabla ya kufungua maonesho ya viwanda na
kongamano la uwekezaji mkoani Ruvuma, Julai 25.2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Christina Mndeme, akiangalia na vikundi vya ngoma, kwenye maonesho ya
viwanda na kongamano la uwekezaji mkoani Ruvuma, Julai 25.2019.(Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment