Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi katika uzinduzi huo.
Rais
Dkt. John Magufuli amesema Tanzania imeamua na ina uwezo mkubwa wa
kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini pasipo kutegemea fedha
zenye masharti zinazotolewa kutoka kwa wafadhili na wadau wa kimataifa
wa maendeleo.
Akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa Jengo la 3 la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi (Agosti 1, 2019),
Rais Magufuli alisema uzinduzi wa Jengo la Uwanja huo ni ushahidi wa
wazi wa usimamizi na nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali
zinazotokana na kodi ya wananchi.
Aliongeza
Jengo la Uwanja huo limejengwa kwa asilimia 100 kutokana na kodi za
Watanzania, na hivyo kuiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
pamoja na Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD) kusimamia vyema
miundombinu ya Uwanja huo kwa kuhakikisha kuwa inatunzwa ili kuakisi
vyema taswira ya Jiji la Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla.
Kwa
mujibu wa Rais Magufuli alisema jengo hilo litakalokuwa na uwezo wa
kuhudumia jumla ya abiria Milioni 6 kwa mwaka limeigharimu Serikali
kiasi cha Tsh Bilioni 722 ambazo ni fedha zilizotolewa na Serikali,
limeweza kuifanya Serikali kuaminika na kuwa na udhubutu wa kutekeleza
miradi ya Maendeleo kupitia fedha za ndani.
“Ipo
miradi mingi ya Maendeleo tunayoisimamia kwa fedha zetu za ndani
ikiwemo Ujenzi wa reli ya kisasa, mradi wa kufua umeme Mto Rufiji,
Barabara za Juu Ubungo, Daraja la Kigongo-Busisi, Daraja la Salender,
Ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya ndege 15, kujenga rada 4 katika
Viwanja vya Ndege vya Dar Salaam, Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro, huu ni
ushahidi wa usimamizi imara wa fedha zetu za ndani” alisema Rais
Magufuli.
Aidha
Rais Magufuli alisema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu
ya sekta ya anga nchini, kwa kuwa sekta hiyo imekuwa kiungo muhimu
katika maendeleo ya sekta ya Utalii, kwani kila siku takribani watu
Milioni 12 duniani hutumia usafiri wa anga kutokana na kuwa njia ya
haraka na ya uhakika kwa ajili ya usafirishaji wa abiria na mizigo.
Akifafanua
zaidi Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
kutoa kipaumbele kwa makampuni ya kitanzania yanapewa nafasi katika
maduka yatakayofunguliwa ndani ya Uwanja huo ili kuwawezesha kufaidi
matunda ya kodi yao sambamba na kuweza kuchangia kikamilifu katika
maendeleo ya uchumi.
Akitoa
taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS,
Mhandisi Patrick Mfugale alisema tangu mwaka 2004-2011 Serikali
imechukua hatua mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya
majengo ya Uwanja wa ndege vyaJulius Nyerere ikiwemo ujenzi wa Jengo
jipya la tatu la abiria katika uwanja huo, kutokana na majengo ya sasa
ya jengo la I na II kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uwezo
mdogo wa kuhudumia abiria.
Anaongeza
kuwa ujenzi wa Jengo hilo la tatu la abiria lilisimama ujenzi wake
mwaka 2016 kutokana na mkandarasi kudai Tsh Bilioni 29, ambapo awali
alishapokea kiasi cha Tsh Bilioni 380 kati ya Tsh Bilioni 560
zilizohitajika kwa ajili ya ukamlishaji wa jengo hilo hapo awali, lakini
mwaka 2017 Serikali ilitoa zabuni ya ujenzi wa mradi huo kwa mkandarasi
mwingine kutokana mkandarasi aliyepita kuwa na kasi ndogo ya
utekelezaji wa mradi.
Kwa
mujibu wa Mhandisi Mfugale alisema kutokana na kasoro zilizojitokeza,
shughuli za ujenzi wa jengo hilo zilipelekwa kwa kampuni ya TECU na
mshauri mwelekezi kampuni ya Arab Contractor ambapo hadi kufikia Mei 29
mwaka huu zilikamilisha ujenzi wa jengo hilo na kusubiri kukabidhiwa kwa
Serikali kwa ajili ya kuanza kutumika kwake.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Mhandisi
Julius Ndyamukama alisema hadi kufikia sasa jumla ya makampuni 18 kati
ya 23 ya kimataifa tayari yamehamishia shughuli zao katika Uwanja huo
kwa ajili ya kuanza kutoa huduma za usafiri kwa abiria wanaosafiri
kwenda nje ya nchi.
Aliongeza
kuwa katika kuimarisha usimamizi bora wa Jengo la Uwanja huo, Mamlaka
hiyo pia imewapatia mafunzo watumishi wake kwa ajili ya kupata uelewa wa
pamoja wa namna bora ya kulinda miundombinu ya Uwanja huo na hadi sasa
imepokea Tsh Milioni 500 kutoka Serikalini ilizozilipa kwa mkandarasi wa
ujenzi wa mradi huo kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment