Kwa mara ya kwanza hapa nchini umefanyika upasuaji
wa moyo wa kukamilisha kuunganisha mfumo
wa mzunguko wa damu iliyokwisha kutumika mwilini kwa kuunganisha mishipa hiyo
ya damu kwenda moja kwa moja kwenye
mapafu ili ikasafishwe bila kupitia mfumo wa usukumaji wa upande wa kulia wa
moyo (Fontan operation).
Upasuaji huo ambao ulichukuwa muda wa masaa sita ulifanyika
kwa mafanikio makubwa umefanywa jana katika
kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa na madaktari bingwa wa
magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikia na
wenzao wa shirika la Mending’s Kids International lenye wataalamu wa afya
kutoka nchini Italia na Marekani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Anjela Mhozya alisema mtoto
aliyefanyiwa upasuaji huo anaumri wa miaka minne alikuwa na tatizo la kutokuwepo
kwa valvu ya kulia ya tricuspid na mfumo wa moyo wa kulia ambao ulikuwa mdogo
kuliko kawaida (tricuspid atresia).
“Tangu kuanza kwa kambi hii siku ya jumatatu jumla ya watoto
35 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu
ya moyo kutokuwa katika mpangilio maalum wamefanyiwa upasuaji wa kufungua na
bila kufungua kifua ambapo hali zao zinaendelea vizuri na wengine
wamesharuhusiwa kutoka katika chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi
maalum (ICU) na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na dawa pamoja na
mazoezi”,.
“Kati ya watoto 35 waliofanyiwa upasuaji watoto 20
wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab na 15
wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua”, alisema Dkt. Anjela
ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa walioko ICU.
Dkt. Anjela alisema ujio wa madaktari hao kutoka nchini Italia na Marekani umekuwa ni neema kwao kwani kumewasaidia kuongeza ujuzi wa kazi na mara baada ya
kumalizika kwa kambi hiyo watautumia ujuzi huo katika kazi zao za kila siku.
Kwa upande wake Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni
ambaye alitembelea Taasisi hiyo ili kuangalia maendeleo ya kambi hiyo
aliipongeza JKCI kwa huduma za matibabu ya moyo inazozitoa hasa kwa watoto
ambao ni taifa la kesho.
“Nafahamu kuwa Taasisi hii inategemewa na watanzania pamoja
na nchi jirani na ndiyo maana katika kambi hii kuna watoto kutoka nchini
Ethiopia na Malawi ambao wamekuja kutibiwa na kama nilivyowaona hali zao
zinaendelea vizuri baada ya kupata matibabu”,.
“Hongereni sana kwa kazi mnayoifanya ya kuokoa maisha ya
watanzania wenye matatizo ya moyo. Tanzania inafanya vizuri katika sekta ya
afya nampongeza Waziri wenu Mhe. Ummy Mwalimu mara kwa mara nimekuwa nikimuona
akifanya kazi mbalimbali za kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora za afya”,
alisema Mhe. Mengoni.
Nao wazazi ambao watoto wao wametibiwa katika kambi hiyo waliishukuru
Serikali kwa Kuboresha huduma za matibabu ya moyo hapa nchini na kuwataka
wazazi wengine ambao watoto wao wanamatatizo ya moyo kwenda kutibiwa katika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)ambako kuna wataalamu wa kutosha.
Upendo Samweli kutoka Iringa ambaye mtoto wake amefanyiwa
upasuaji wa bila kufungua kifua alisema mtoto wake alikuwa anapata tabu ya kupumua
vizuri, kukohoa mara kwa mara na
kupungua uzito lakini baada ya kufika
JKCI na kufanyiwa vipimo alikutwa na tundu kwenye moyo.
Upendo aliomba, “Ninawaomba madaktari walioko mikoani wanaowatibu
watoto kama wataona wanamtibu mtoto kwa muda mrefu hapati naafuu wampe rufaa
ili aweze kutibiwa katika Hospitali zenye utaalamu wa juu zaidi. Mimi mwanangu
kabla hajagundulika kuwa na matatizo ya moyo niliambiwa mtoto hapati lishe ya
kutosha, kanywa maji ya uzazi lakini baada ya kuona anatibiwa muda mrefu bila
ya kupata naafuu niliomba rufaa ya kuja kutibiwa JKCI”,.
Naye Rachel Anton
mkazi wa Kibaha ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji mkubwa wa kuziba tundu
kwenye moyo na kurekebishwa mishipa ya damu ya moyo alishukuru kwa huduma ya
matibabu aliyoipata na kuwasihi wazazi wanapoona mtoto hakui vizuri na anaumwa
mara kwa mara wawahi Hospitali mapema ili aweze kutibiwa kwa wakati.
Habari hizi siyo tu zinasisimua bali zinadhihirisha ubingwa wa madaktari wetu,imani ya nchi jirani na mrengo sahihi wa sera na uongoziimara wa Ras wetu Magufuli. Viva Tanzania 👏
ReplyDeleteNifaraja kubwa kuyaona maendeleo hata naamini mbeleni kama juhudi za kupanua zaidi uelewa wa madaktari waliopo na wanaoendelea kufundishwa, sambamba na ununuzi wa vifaatiba vya kisasa badala ya India watu watakuja Tanzania. Big up Magufuli, big up Ummy Mwalimu big up wataalam wetu
ReplyDelete