Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amezindua huduma ya ulipaji kodi ya pango
la ardhi kwa kutumia mtandao wa simu ya mkononi kupitia Airtel Money.
Uzinduzi wa ulipaji kodi
ya pango la ardhi kwa njia ya Airtel Money unarahisisha huduma hiyo ambapo wamiliki
wa ardhi wataweza kufanya malipo kupitia mtandao huo wa simu bila kwenda ofisi
za Ardhi.
Akizungumza jijini
Dodoma leo tarehe 9 Septemba 2019 wakati wa kuzindua huduma hiyo, Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema ubunifu wa serikali
kufanya malipo ya Ankara za serikali kwa kutumia mfumo wa GePG umerahisisha
malipo ya tozo mbalimbali za serikali ikiwemo kodi ya pango la ardhi.
Alisema mfumo huo wa
malipo ya serikali umekuja na faida nyingi kama vile kuweka kumbukumbu vizuri,
kulipa kwa muda, kupunguza upotevu wa mapato ya serikali, kuondoa mianya ya
rushwa pamoja na kuongeza mapato ya serikali.
‘’Tunayo furaha kubwa
kwa mara nyingine kutangaza kuwa kampuni ya simu ya Mkononi ya Airtel
imerahisisha malipo ya kodi ya pango la ardhi kupitia Airtel Money. Hii ni
huduma rahisi na itapunguza kero nyingi wakati wa kufanya malipo’’ alisema
Lukuvi.
Aliitaka kampuni ya simu
ya Airel kusaidia kuhimiza wananchi wanaotumia mtandao wa simu wa kampuni hiyo
kulipia tozo mbalimbali za serikali ikiwemo kodi ya pango la ardhi kwa airtel
money kwa kuwa inarahisisha kufanya malipo mahali popote.
Waziri Lukuvi amesema
lengo la wizara yake kwa sasa ni kutaka kutumia makampuni ya simu kuwakumbusha
wananchi kulipia kodi ya pango la ardhi kupitia jumbe za simu badala ya
utaratibu uliopo sasa wa kwa kuwafuata wadaiwa.
‘’Sasa ofisi za ardhi
za kulipia kodi ya pango la ardhi ziko viganjani mwenu mnaweza kulipia bila
kwenda katika ofisi za ardhi’’alisema Lukuvi.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Beatrice Singano alisema, kuunga mkono
juhudi za serikali ni moja ya ajenda kubwa ya kampuni ya Airtel na kubainisha
kuwa kampuni hiyo inaelewa umuhimu wa kukusanya kodi na kulipa malipo ya
serikali kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuleta maendeleo.
Kwa mujibu wa Singano,
Airtel itaendelea kushirikiana na taasisi pamoja na mashirika mengine ya
serikali kwa ajili ya kutimiza azma ya Serikali katika kukusanya mapato na
kutoa wito kwa watanzania kuendelea kutumia huduma za kielektroniki kwa kuwa zina
ubunifu mkubwa na kusisitiza kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na watanzania kwa
asilimi 49 na matumizi ya mtandao huo ni
kutumia kilicho cha watanzania.
No comments:
Post a Comment