Na. Dianarose Shirima-Maelezo
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amezungumza na waandishi wa habari
kuelezea uwepo wa tamasha la utamaduni la Afrika Mashariki JAMAFEST 2019
ambalo litafanyika kuanzia tarehe 21 hadi 28 Septemba katika uwanja wa
Taifa Dar es Salaam.
Dkt. Mwakyembe amesema kuwa maonyesho
hayo yatajumuisha wasanii wanchi zote sita za Jumuiya ya Umoja wa
Afrika Mashariki ambao ni wasanii wa ufundi kama vile wachonga vinyago,
wachoraji, wabunifu wa mavazi, watengeneza bidhaa za vitenge, Batiki,
wanasanaa wa ulimbwende, wasuka mikeka.
Vilevile wasanii wa taarabu, nyimbo za
injili, wasanii wa maigizo, watungaji pamoja na wataalamu wa lugha ya
Kiswahili na watafiti wa tiba za asili na vipodozi, hayo ndiyo makundi
makubwa ambayo yatakuwepo siku hiyo pamoja na sanaa nyingine nyingi za
ubunifu.
Dkt. Mwakyembe amesema kuwa wasanii wa Muziki kama vile Peter Msechu ambaye ni mtunzi wa wimbo wa TANZANIA YA VIWANDA akiwa
amewashirikisha wasanii wengine kama Mimi Mars, Linnah, Rich Mavoko
ambao watakuwepo kwa ajili ya kuzindua wimbo huo, pia uwepo wa msanii
mkubwa wa Tanzania anayepeperusha vyema bendera ya Tanzania Kimataifa
Diamond Platnumz, “najua atakuwa na ziara yake mkoani Iringa lakini
nimemuomba kuahirisha kwa maslahi ya taifa ni matumaini yangu atakubali
kufanya hivyo”, alisema.
“Matamasha yaliyofanyika Rwanda, Kenya na
Uganda miaka ya nyuma yalikuwa ni yenye mafanikio makubwa ambapo wengi
waliohudhuria walifaidika na maonyesho hayo, na kuendana kabisa na lengo
la maonyesho hayo ambalo ni kuhifadhi, kulinda na kuendeleza urithi
wa tamaduni za watu weusi wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla”,
alisema Dkt.Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe amewahakikishia
wahudhuriaji wote wa tamasha la JAMAFEST, Wanajumuiya wa nchi za Afrika
Mashariki pamoja na watanzania kuwepo ulinzi na usalama katika tamasha
hilo huku akitolea mfano wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
waliokuja Jijini Arusha katika michezo kutoka nchi za Afrika Mashariki
waliweza kukaa kwa muda wa siku kumi na waliondoka bila tatizo lolote
hivyo hata katika maonyesho haya ya JAMAFEST yatakuwa ni yenye amani.
Mwakyembe amewataka watanzania kuwa
wabunifu, licha ya yeye kutaja vitu vitakavyokuwepo katika maonyesho
hayo amewataka watanzania kuwa na ladha tofauti kuwa ya hali ya juu
ambayo itavutia watazamaji kutoka katika jumuiya ya Afrika Mashariki,
pia maonyesho haya yanahitaji ubunifu zaidi pamoja na kuonyesha vyakula
vya asili ambavyo ni tamaduni ya watu weusi ‘vyakula vitapikwa vya aina
mbalimbali lakini pia tutakuwa na madaktari ambao watathibitisha kwa
afya za binadamu’ alisema.
Dkt. Mwakyembe amewakaribisha watanzania
wote kuhudhuria maonyesho hayo kuonesha ubunifu wao na kufaidika na
maonyesho hayo katika Nyanja mbalimbali za kijamii, kiuchumi na
kiutamaduni.
Sambamba na hilo, Katibu Mtendaji Bodi ya
Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo amesema kuwepo kwa Tuzo ya filamu
bora ambapo nchi zote za Afrika Mashariki wataleta filamu zao na kila
nchi italeta filamu tatu ambapo ziashindanishwa ili kupata filamu tatu
bora katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa upande wa Tanzania tayari
wasanii wameshaanza kupeleka fiilamu zao na tayari wameshaambiwa ni
filamu za aina gani zinazohitajika kwa ajili ya mashindano hayo,
‘nipende kuwakaribisha wasanii wote wa Tanzania kushiriki katika
maonyesho hayo.
No comments:
Post a Comment