Rais wa Kwanza wa Tanganyika na Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Baba
wa Taifa, aliyetuletea Uhuru, anatimiza miaka 20 tangu alipoiaga dunia
tarehe 14 Oktoba mwaka 1999.
Mara baada ya Uhuru Mwalimu Nyerere
aliwaandaa Watanzania wakati ule Watanganyika kisaikolojia kuwa ni
lazima wajitegemee. Kwa kuwa aliona viashiria vya utegemezi, ambapo
wananchi walio wengi wakidhani Uhuru maana yake ni kubweteka na kuletewa
vitu vya bure bila kufanya kazi.
Kama hiyo haitoshi Mwalimu akaja rasmi na
Azimio la Arusha tarehe 05 Februari 1967 baada ya kuona viashiria vya
ubwanyenye, unyonyaji, rushwa na upendeleo kwa baadhi ya viongozi. Moja
ya mikakati yake katika azimio hili ni kufanya kazi kwa bidii ndipo
alipozindua Elimu ya Kujitegema Shuleni.
Wakati wa uzinduzi huo Mwalimu Nyerere
alisema maneno haya; “Tumieni kikamilifu uwezo wetu wa ndani
kujitegemea, tumieni watu wetu na ushirikiano katika ngazi mbalimbali
fanyeni hivyo na muone utegemezi kuwa ni adui wa nchi”. Tujenge nchi
yetu tutumie uwezo wetu wa ndani kwa ajili ya maendeleo yetu.
Kitendo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere
kuamua kuja na sera za kujitegemea na kukataa utegemezi kwa kiasi
kikubwa kiliwachefua mabeberu, ambao walitumia silaha ya misaada katika
suala zima la kulazimisha nchi kufuata masharti na itikadi wanazizitaka
wao.
Tuna haki ya kumwambia Mwalimu Nyerere
maneno haya kuwa leo hii Tanzania inatembea kifua mbele kwa kufanya
mambo mengi ya maendeleo kwa kutumia fedha zake za ndani. Msingi na
muongozo wa kutumia fedha hizo za ndani umeuweka wewe Mwalimu Nyerere.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt John Pombe Magufuli leo ni kielelezo cha matamshi yako uliyoyasema
wakati unazindua Elimu ya Kujitegemea mara baada ya kutangaza Azimio la
Arusha.
Nanukuu maneno yako Mwalimu “Tumieni
kikamilifu uwezo wetu wa ndani kujitegemea, tumieni watu wetu na
ushirikiano katika ngazi mbalimbali fanyeni hivyo na muone utegemezi
kuwa ni adui wa nchi”.
Akihutubia Mkutano wa hadhara pale Mkoa
wa Katavi Rais Magufuli amesema Mtaji wa Msikini ni nguvu zake mwenyewe.
Tunajitegemea kwa fedha zetu. Mradi wa Barabara wa Kaliuwa –
Mpandafedha zetu, SGR, (reli ya kisasa), fedha zetu, vituo vya afya na
hospitali fedha zetu. Tembeeni kifua mbele.
Fedha za Elimu bure darasa la kwanza hadi
kidato cha nne, shilingi Bilioni 23.6 kila mwezi fedha zetu, Hata Ulaya
hawawezi hili amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa
mabeberu hawaoni raha kuiona Tanzania ikitekeleza miradi yake kwa fedha
zake ndio maana wanaizushia mabaya yakiwemo magonjwa hatari.
Amesisitiza kwa kusema Mabeberu hawaoni
raha kutuona tunafanya mambo makubwa ka fedha fedha zetu wenyewe . Ndio
maana wanafanya mbinu zao wanadai kuna ugonjwa. Wapuuzeni!!!!!.
Utabiri na uhalisia wa maono na uwezo wa
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere umetimia. Hakika Tanzania inajitegemea kwa
kutumia fedha zetu za ndani . Mwalimu tumeona utegemezi ni adui wa
nchi.
Yapo mambo mengi sana mbayo Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere alilazimishwa kuyafuata na hao mabeberu, mfano
kuchaguliwa marafiki na kutakiwa kufata mrengo wa kushoto au kulia ili
kupata misaada. Lakini Mwalimu alishinda vita hiyo kwa sababu wa msimamo
wake na hoja alizokuwa anawasilisha mezani wakati akiongea na mabeberu
hao na hakika walisalimu amri kwa Mwalimu.
Sio mara moja au mbili kwa Mwalimu
kufanyiwa hila na mabeberu hao Aidha, kwa kutumia Watanzania wenye
fikira za kujineemesha wao wenyewe na familia zao kwa kudiriki kuwa
wasaliti wa nchi yao. Hivyo Rais Magufuli hilo la hila limeanza kwa
Mwalimu Nyerere usistajabu kutokea sasa.
Pia, Mwalimu Nyerere alipolazimishwa
kufuata mpango wa Benki ya Dunia baada ya kutumia hila nyingi ikiwemo
vibaraka wao na mabeberu kutumiwa kuvunja Jumuiya ya Afrika Mashariki,
kumshabikia Rais wa Uganda Idi Amin Dadah kuichokoza Tanzania na Jumuiya
ya Kimataifa kukaa kimya bila kumkemea ili kukuza mgogoro na Tanzania
kusababisha vita.
Hali hiyo ilidhoofisha uchumi wa Tanzania
kwa kiasi kikubwa ambapo Mabeberu wakafurahia hali hiyo wakidhani
Mwalimu atasalim amri kwao. Kwa kuwa hali ya uchumi ilikuwa ngumu,
Wahijumu uchumi wakapata kiburi cha kuficha mali kuendlea kumdhoofisha
uchumi wa nchi.
Serikali ya Awamu ya Tano ipokee ushuzi
wowote wanaouanzisha, kusema wazi na kuwaambia mabeberu hao kuwa tunajua
njama zao na kuelezea Jumuiya ya Kimataifa kuwa hizo ni njama. Hiyo,
ndio silaha pekee ambayo Tanzania iendelee kuitumia kama alivyofanya
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Mwalimu Nyerere ataendelea kukumbukwa na
Watanzania katika maisha yao yote kwa kuwa mambo aliyowafanyia ni ya
kipekee ambayo hayawezi kufanywa na kiongozi yeyote yule ajaye. Tunasema
hivyo kwa sababu kuna mambo yanafanyika mara moja katika historia ya
nchi hayawezi kurejelewa tena . Mfano yeye ndiye aliyetuletea Uhuru
tarehe 09 Desemba mwaka 1961, hivyo hakuna awezaye kutulletea tena Uhuru
itabaki kuwa hivyo milele katika taifa hili.
Lakini Tukatae, tukubali penye ukweli
uongo hujitenga Uongozi wa Awamu ya Tano unavaa ipasavyo viatu vya Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kadiri siku zinavyosonga
mbele ndivyo anavyozidi kumuenzi, wewe usiyekubali sio rahisi
kuwashawishi watanzania wote wakubaliane na wewe kwa kuwa wanaona,
wanasikia na vitendo vinaonekana kwa macho.
Kwa kuwa Mwalimu Nyerere alitumia Elimu
Bure kuwafunza na kuwaandaa Watumishi Mashujaa wa kuja kuitumikia
Tanzania. Ni wajibu wa uongozi kuona alichokifanya Baba wa Taifa
kinaendelezwa ili kuzalisha Watumishi wengi watakaoitumikia nchi kwa
moyo wao wote.
Mwalimu Baba wa Taifa la Tanzania hakika
kazi uliyoifanya hapa Tanzania ni ya kutukuka ikiwemo ya kuwaandaa
vijana wako ambao sasa wapo madarakani. Uliwafunza wakaelimika, na sasa
wanatenda kwa vitendo na Tanzania inang’ara Mashasriki, Magharibi
Kaskazini na Kusini mwa Dunia. PUMZIKA KWA AMANI MWALIMU.
Na Judith Mhina-Maelezo
No comments:
Post a Comment