Jumla ya wagonjwa 28,876 wenye matatizo
ya moyo wametibiwa kwa kipindi cha miezi mitatu ya Julai hadi Septemba
mwaka huu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Hayo yamesemwa jana na Kaimu Mkurugenzi
wa Kurugenzi ya Magonjwa ya Moyo Dkt. Peter Kisenge wakati akieleza
taarifa ya kazi zilizofanywa na Kurugenzi yake katika kikao cha
menejimenti kilichofanyika jana katika Taasisi hiyo.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa
wa magonjwa ya moyo alisema wagonjwa waliotibiwa katika Taasisi hiyo
wanaume walikuwa 12,566 na wanawake 16,310 ambapo 6,590 sawa na asilimia
22.8 walikuwa wagonjwa wapya.
“Tumeona wagonjwa kutoka mikoa yote ya
Tanzania Bara na Visiwani pamoja na nchi za Ethiopia, Malawi, Zimbabwe,
Visiwa vya Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Wagonjwa
waliotibiwa na kurudi nyumbani walikuwa 27,882 na wagonjwa 994 walilazwa
kati ya hao 500 ni wanawake na 494 ni wanaume idadi ya vifo vikiwa ni
asilimia 6”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge aliendelea kusema kuwa
watoto waliotibiwa katika Taasisi hiyo walikuwa 1,516 ambapo wa kike
walikuwa 800 na wavulana 716 kati ya hao wagonjwa 374 walikuwa wapya.
Dkt. Kisenge alisema, “Wagonjwa wengi
tuliowaona walikuwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, kutanuka
kwa moyo,valvu, matundu, mishipa ya damu ya moyo na magonjwa ya moyo ya
kuambukizwa yanayosababisha makovu katika valvu za moyo kutokana na
kupata mafindofindo kwenye tezi za koo (Rheumatic Heart disease) ”,.
Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa bila
kufungua kifua na kuzibuliwa mishipa ya damu ya moyo pamoja na kuwekewa
vifaa vinavyousaidia moyo kufanya kazi vizuri walikuwa 352 kati ya hao
watoto 87 sawa na asilimia 24.7 na hakukuwa na mgonjwa aliyepoteza
maisha.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa
Kurugenzi ya Upasuaji Dkt. Anjela Muhozya alisema wamefanya upasuaji
kwa wagonjwa 153 kati ya hawa wagonjwa 122 walifanyiwa upasuaji wa
moyo wa kufungua kifua, wagonjwa 23 walifanyiwa upasuaji wa mishipa ya
damu na nane walifanyiwa upasuaji wa mapafu.
“Tumefanya upasuaji wa kubadilisha valvu
kwa wagonjwa ambao valvu zao zilikuwa na shida, kurekebisha mishipa ya
damu ya moyo na kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery
Bypass Graft – CABG). Wagonjwa waliopoteza maisha ni watatu sawa na
asilimia 2.5”, alisema Dkt. Anjela.
Dkt. Anjela alisema changamoto kubwa
wanayokutana nayo katika matibabu ya wagonjwa wa moyo ni wagonjwa wengi
kufika katika Taasisi hiyo huku mioyo yao ikiwa imechoka. Na kuwaomba
wagonjwa kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kujuwa kama
wanamatatizo ya moyo au la na kama watakuwa nayo waweze kupata matibabu
kwa wakati.
Naye Cecilia Nthala kutoka nchini Malawi
ambaye mtoto wake anatibiwa katika Taasisi hiyo alishukuru kwa huduma ya
matibabu ya moyo aliyoipata .
“Nilipata taarifa ya Taasisi hii kupitia
tovuti na mitandao ya kijamii, kwa kuwa mtoto wangu ana matatizo ya
moyo nikawa nafuatilia kwa ukaribu huduma mbalimbali wanazozitoa baada
ya kuridhika nazo nikaamua kumleta mwanangu ili naye apate huduma ya
matibabu”, alisema Cecilia.
“Kwa kipekee ninawashukuru wauguzi na
madaktari kwani muda wote wako karibu na mimi najiona kama vile niko
nchini kwetu Malawi. Ninawaomba muendelee kutoa huduma kama hii
mliyoitoa kwangu kwa wagonjwa wengine mnaowatibu”, alishukuru Cecilia.
No comments:
Post a Comment