Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki amezitaka kampuni binafsi
nchini kuweka utaratibu maalum wa kuwasaidia wafanyakazi na familia zao pindi
wanapokabiliwa na majanga mbalimbali ya kibindamu ikiwemo ajali na vifo.
Waziri
Kairuki aliyasema hayo jana Jumatatu (Desemba 16, 2019) wakati wa ziara yake ya
kutembelea Kampuni ya vinywaji baridi ya SBC Tanzania Ltd inayozalisha vivywaji
vya Pepsi, Mirinda, Mountain Dew na 7up, na kusema utaratibu huo utasaidia
kuongeza tija, motisha na uzalishaji katika makampuni hayo.
Waziri
Kairuki alisema Kampuni ya SBC Tanzania imekuwa ni miongoni mwa makampuni
machache nchini yaliyoweka utaratibu wa kusaidia wafanyakazi wake wakati wa
majanga, ikiwemo vifo na hivyo kuwataka waajiri wa makampuni mengine kuiga
mfano huo kwani wafanyakazi ni kiungo muhimu cha mafanikio ndani ya makampuni
hayo.
‘Hapa
PESPI kuna Mtumishi alifariki akiwa kazini, na kampuni ya SBC ilimchukua mtoto
wake na kumuendeleza kielimu kuanzia degree (Shahada) ya kwanza hadi ya pili na
yupo katika Idara ya Masoko ya kampuni hii na huu ni mfano mzuri unaopaswa
kuigwa na makampuni mengine katika kuendeleza familia za wafanyakazi wao pindi
wanapofariki’ alisema Waziri Kairuki.
Aidha
Waziri Kairuki alisema kitendo cha kuweka utaratibu wa kuwasadia wafanyakazi na
familia zao wakati wa majanga utasaidia kuendeleza kizazi kinachofuata ndani ya
kampuni hizo na hivyo kuwafanya kufurahia kufanya kazi ndani ya kampuni hizo na
kuhimiza utaratibu huo kuwa endelevu ili kuzidi kuimarisha ushirikiano baina ya
kampuni hizo na familia za wafanyakazi.
Akizungumzia
kuhusu uzalishaji wa Kampuni hiyo, Waziri Kairuki aliupongeza Uongozi wa SBC
Tanzania Ltd kutokana na juhudi na jitihada kubwa inazoendelea kuzifanya katika
kukuza soko la bidhaa za vinywaji nchini sambamba na kuendelea kutoa ajira kwa
Watanzania na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi nchini.
Akitolea
mfano Waziri Kairuki alisema Kampuni hiyo yenye mtaji wa Dola Milioni 373
imeendelea kukuza mnyoyoro wa thamani wa bidhaa zake nchini, ambapo katika
kipindi cha miaka 18 tangu kuanzishwa kwake kiwanda hicho kimeonyesha uhalisia
wa kazi kubwa inayofanya, na hilo linadhihishwa na kiwango cha malipo ya kodi kwa
Serikali ya Tsh Bilioni 416 iliyolipa kuanzia mwaka 2001.
‘Kampuni
hii ilianza mwaka 2001 ikiwa wafanyakazi
76 na mtaji wa uwekezaji wenye thamani ya Tsh Bilioni 24.6, lakini kwa sasa ina
jumla ya wafanyakazi walioajiriwa katika ajira ya moja kwa moja takribani 1215,
na pia wameendelea kuhuisha mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao kila baada ya
miaka 2-3’’ alisema Waziri Kairuki.
Kwa
upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya SBC Tanzania Ltd, Avinash Jha
alisema Kampuni hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na serikali
katika kufanikisha mikakati mbalimbali ikiwemo sera ya uchumi wa viwanda, hatua
inayolenga kuleta maendeleo jumuishi kwa Watanzania wote.
Jha
aliongeza kuwa kampuni yake itaendelea kuzingatia sera, miongozo na maelekezo
mbalimbali yanayotolewa na Serikali ikiwemo kutoa ajira kwa vijana wengi wa
Kitanzania sambamba na kuwajengea uwezo na uzoefu wa kazi ili kumudu changamoto
zilizopo katika soko la ajira nchini.
No comments:
Post a Comment