Jumla
ya wafanyabiashara 1,950 wa Mkoa wa Iringa wamefikiwa na kupatiwa elimu ya kodi
wakati wakampeni ya elimu kwa mlipakodi iliyofanyika kuanzia tarehe 17 hadi 27
Februari,2020.
Kampeni
hiyo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kuwafikia na
kuwaelimisha baadhi ya wafanyabiashara wa Wilaya za Kilolo, Manispaa ya Iringa
na Mufindi.
Akizungumza
mara baada ya kuhitimisha kampeni hiyo mkoani humo, Afisa Msimamizi wa Kodi Mwandamizi
wa TRA Bi. Catherine Mwakilagala amesema kuwa, zoezi hilo limekuwa na mafanikio
makubwa kwani wamefanikiwa kuwaelimisha jumla ya walipakodi 1,950.
“Mamlaka
ya Mapato Tanzania tumehitimisha kampeni ya elimu kwa mlipakodi katika mkoa huu
wa Iringa na zoezi hili limekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu tumeweza kuwafikia
jumla ya walipakodi 1,950 ambao wote tumewapatia elimu ya kodi na wamepata
nafasi ya kutoa maoni na changamoto zao ambazo tumezipokea na nyingine
tumezipatia ufumbuzi,” alisema Bi. Mwakilagala.
Kwa
upande wake Meneja wa TRA mkoani humo Bw. Lamson Tulyanje ametoa wito kwa
wafanyabiashara wote waliotembelewa na maafisa wa TRA kwenye maduka yao na wale
waliopata elimu kupitia semina wakati wa kampeni hiyo, kutumia elimu walioipata
kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati na hiari.
“Elimu
ambayo wameipata wafanyabishara mbalimbali kwenye kampeni hii ya elimu kwa
mlipakodi, ni vizuri waitumie katika kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa
wakati ili Serikali iweze kutimiza majukumu yake ya kuwapatia huduma mbalimbali
wananchi,” alieleza Bw. Tulyanje.
Na
Veronica Kazimoto
Bw.
Richard Kilawa ni mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi kutoka Halmashauri
ya Mji wa Mafinga mkoani humo ambaye ameishukuru TRA kwa kumfikishia elimu ya
kodi dukani kwake na ameahidi kuendelea kulipa kodi kwa hiari.
“Ninashukuru
sana TRA kunitembelea dukani kwangu na elimu yao imenifundisha kulipa kodi kwa
hiari. Hivyo, nitawashawishi wafanyabiashara wenzangu walipe kodi kwa hiari ili
tujenge nchi yetu,” alisema Bw. Kilawa.
Naye,
mfanyabiashara wa mbao wa Halmashauri hiyo, Bi. Maura Ng’umbi amesema kuwa, kupitia
elimu iliyotolewa na maafisa wa TRA wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi,
imewasaidia kujua umuhimu wa kulipa kodi stahiki kwa manufaa ya Taifa.
Kampeni
ya elimu kwa mlipakodi iliyomalizika mkoani Iringa ni mwendelezo wa kampeni
zilizofanyika katika Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam kwa lengo la
kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali ya kikodi, kupokea maoni
na mapendekezo yao pamoja na kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment