Matokeo chanyA+ online




Friday, March 20, 2020

UKARABATI WA MELI YA MV VICTORIA UMEFIKIA ASILIMIA 75

Serikali imekamilisha ujenzi wa meli mpya ya MV Mbeya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 katika Ziwa Nyasa mkoani Mbeya.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango wakati akiwasilisha mapendekezo ya  serikali ya mpango wa maendeleo wa taifa 
na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya  serikali kwa mwaka 2020/21 mjini Dodoma

Waziri Mpango amesema kuwa kwa sasa ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria utekelezaji wake  umefikia asilimia 52 na ujenzi wa chelezo umefikia asilimia 80.

Aidha, amesema kuwa ukarabati wa meli ya MV Victoria umefikia asilimia 75 na MV Butiama asilimia 70 ambapo  awamu ya kwanza ya upanuzi wa maegesho ya Magogoni - Kigamboni umekamilika.

Akizungumzia  jengo la abiria na ofisi ya kivuko cha Lindi – Kitunda amesema umekamilika na kukabidhiwa.

Aidha, Waziri Mpango amesema kuwa  vivuko vya MV Kigamboni, Kigongo – Busisi na MV Utete pia vimekamilika ambapo kwa sasa ujenzi wa vivuko vipya vya Nyamisati - Mafia umefikia asilimia 28, Bugolora - Ukara (asilimia 40), Chato - Nkome na Kayenze Bezi umefikia asilimia 98.

Akitaja  shughuli nyingine ni kununuliwa kwa kivuko kipya chenye uwezo wa kubeba tani 170 Magogoni - Kigamboni kuendelea na ukarabati wa vivuko vya MV Sengerema ambao umefikia asilimia 70 na MV Misungwi umefikia asilimia 20.

Ambapo  jumla ya shilingi bilioni 81.5 zimetumika kugharamia ujenzi na ukarabati wa meli na vivuko ikijumuisha shilingi bilioni 38.8 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020.

No comments:

Post a Comment