Serikali imewaagiza Makamanda wa
Polisi na Wakuu wa Magereza mikoa yote nchini kuhakikisha inawapa dhamana
mahabusu wote wanaokidhi vigezo vya dhamana na kuharakisha upelekwaji haraka
wa kesi kwa watuhumiwa waliopo katika magereza mbalimbali nchini ili kuweza kuepusha
na kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya
corona(Covid 19) usiweze kuingia katika mahabusu za polisi na magereza.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati alipofanya ziara ya
kushtukiza katika Vituo mbalimbali vya Polisi mkoani Dodoma ambapo alibaini
kuwepo msongamano wa mahabusu katika vituo vya polisi huku akifanikiwa
kuzungumza na baadhi ya mahabusu ambao ilionekana kesi zao zinadhaminika huku
wengine wakiruhusiwa katika ziara hiyo.
“Maagizo ya Serikali na wataalamu wa
afya ni kuepusha misongamano sasa nimetembelea kituo hiki cha kati nimekuta
mahabusu wengine wamekaa siku kumi na nne,na wengine wanaingia wakiwa
wametoka nje huko hali iliyopelekea msongamano mkubwa katika kituo hiki, na
kuna mahabusu mmoja nimekuta wamemuweka siku tatu hapa kosa lake wamemkamata
tu anapita nje ya bunge hii sio sawa huku hana kosa lolote.
“Sasa natoa maagizo kwa Makamanda wa
Polisi nchi nzima katika kukabiliana na ugonjwa wa corona wahakikishe
mahabusu wote ambao kesi zao zinadhaminika watolewe, agizo hili pia liende
kwa wakuu wa magereza yote nchini kuhakikisha watuhumiwa wote kesi zao
zinaharakishwa kupelekwa mahakamani hii yote ikiwa ni mkakati wa kupambana na
gonjwa la Corona sasa watu wamerundikwa tu hakuna kinachoendelea hii si sawa”
alisema Masauni
Pia alipata fursa ya kuzungumza na
wananchi waliokusanyika nje ya vituo vya polisi wakija kuwaona ndugu zao huku
akisisitiza washughulikiwe haraka kwani wamekusanyana wengi huku serikali
ikiwa imepiga marufuku mkusanyiko wa watu na wataalamu wakishauri umbali kati
ya mtu na mtu uwe mita moja.
“Wananchi wamekuja kuona ndugu zao
waliopo mahabusu tunajua ni haki yao pamoja na kuwaletea chakula lakini
muwahudumie haraka waondoke hii mikusanyiko ishakatazwa ni hatari sana”
alisema Masauni.
|
No comments:
Post a Comment