Matokeo chanyA+ online




Tuesday, April 28, 2020

TANZANIA NA KUWAIT ZAAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akizungumza na Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Mubarak Mohammed Faleh Alsehaijan alipomtembelea katika ofisi za wizara Jijini Dodoma tarehe 28 Aprili 2020.

Mazungumzo yao yalijikita katika kujadili namna bora ya kuuenzi na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia iliopo baina ya mataifa yao ili uweze kuleta tija na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Kuwait.

Vilevile wawili hao walipata fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya utekelezezaji katika sekta ya afya, na utawala ambapo kwa pamoja wamekubaliana kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha mambo yaliyokubaliwa kwa nyakati tofauti katika sekta hizo yanakamilika kwa wakati.

Tanzania na Kuwait zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya kilimo, afya, biashara, maji, pamoja na ujenzi wa miundombinu wezeshe katika sekta hizo kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa diplomasia ya uchumi unafikiwa kwa wakati. 

Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Mubarak Mohammed Faleh Alsehaijan akifafanua jambo kwa Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Ndumbaro ambapo pamoja na mambo mengine walipata nafasi ya kushirikishana hatua mbalimbali zinazochukuliwa na mataifa yao katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa Corona unaoikabili dunia kwa sasa.

Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Ayoub Mndeme na Msaidizi wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Charles Faini wakifatilia mazungumzo.

Mazungumzo yakiendelea.

No comments:

Post a Comment