Waziri
wa Madini, Doto Biteko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na
kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Geita mara baada ya hafla ya
uzinduzi na makabidhiano ya kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Katente na
Lwamgasa Mkoani Geita. Kiwanda hicho kimekabidhiwa kwa Shirika la
Madini la Taifa (Stamico) ili kukisimamia na kukiendesha.
Waziri
wa Madini, Doto Biteko amelitaka Shirika la Madini la Taifa (Stamico)
kusimamia ipasavyo Viwanda vya Mfano vya Uchenjuaji wa madini ya dhahabu
vya Katente-Bukombe na Lwamgasa-Geita alivyovizindua leo APRIL 26 na
kuvikabidhi rasmi kwa shirika la Stamico..
Ujenzi
wa viwanda hivyo visivyotumia kemikali hatari ya zebaki ulifanywa na
kampuni ya Tan Discovery MineralConsaltancy Limited inayosimamiwa na
Rogers Sezigwa iliyoanza ujenzi wa mradi mwezi Disemba, 2016
ikianziaLwamgasanakufuatianaKatentenaItungi- Chunya.
Akizungumza
wakati wa hafla ya uzinduzi wa viwanda hivyo vya Mfano,Waziri Biteko
amesema, itakuwa aibu kubwa kwa Stamico endapo Viwanda hivyo vitafia
mikononi mwao kwani Serikali imetumia gharama kubwa katika ujenzi wa
viwanda hivyo.
Mtaalamu
wa kuendesha mitambo ya uchenjuaji wa dhahabu kwa kutumia teknolojia ya
Kisasa Gabriel Masanyiwa akitoa maelezo ya hatua zinazopitiwa mpaka
kupata dhahabu.
“Afe Kipa, afe beki ni lazima viwanda hivi vifanye kazi” Biteko alisisitiza.
Aidha,Waziri
Biteko amewahakikishia wananchi na wachimbaji wadogo wa madini nchini
kuwa, serikali ya Rais John Magufuli inawajali na itawahudumia kwa
gharama nafuu hivyo wasisite kupeleka mawe kiwandani hapo ili waweze
kuchenjuliwa dhahabu kwa kutumia teknolojia mpya na ya kisasa na hivyo
kuepuka kutumia zebaki na kuachana na utumiaji wa matimba kwenye
mashapo.
Amesema
matumizi ya matimba wakati wa uchimbaji yanasababisha uharibifu wa
mazingira wakati zebaki huathiri afya za wachimbaji hivyo waitikie na
kuvitumia viwanda hivyo kwa faida zao.
Waziri
wa Madini, Doto Biteko akisaini kitabu cha wageni mara baada ya
kuwasili kilipojegwa kiwanda cha kuchenjua dhahabu bila kutumia kemikali
ya zebaki cha Katente wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho uliofanyika
tarehe 26 Aprili, 2020
“Tumetengeneza viwanda hivi kuwavutia ninyi fanyebiashara” Biteko alisisitiza.
Pamoja
na hayo, Waziri Biteko alimtaka Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico
kuhakikisha wanasimamia ipasavyo miradi hii pasipo kucheka na watu
wasiotimiza wajibu wao kwenye viwanda hivyo.
Sambamba na hayo amewataka Bodi pamoja na Stamico kuhakikisha
wananchi wanaozunguka viwanda hivyo wananufaika na uwepo wa viwanda
katika maeneo yao kwa kupata ajira ndogo ndogo kwa kufanya hivyo
kutainua uchumi wao.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila akiongea jambo wakati wa
hafla ya uzinduzi wa viwanda vya kuchenjua dhahabu vya Katente na
Lwamgasa uliofanyika Katente mkoani Geita tarehe 26 Aprili 2020.
Akizungumzia faida zitokanazo na uwepo wa viwanda hivyo vya mfano,
Waziri Biteko alisema ni pamoja na utoaji wa mafunzo na maarifa kuhusu
sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali kwa wachimbaji wadogo,
kutolewa elimu ya mfumo wa kuthamini mashapo ya madini yaliyopo
ilikufanya uchimbaji wenye tija, kuchenjua dhahabu pamoja na kukodishwa
vifaa vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji kwa gharama nafuu
pamoja na kutolewa elimu juu ya uongezaji thamani madini na upatikanaji
wa masoko.
Akizungumzia mchakato wa ujenzi wa viwanda hivi vya mfano, Mkurugenzi
wa Idara ya Sera na Mipango, Augustine Ollal amesema, ujenzi huo
nimatokeo ya Utekelezaji wa Sera ya Madini ya mwaka 2009 iliyosisitiza
zaidi juu ya uendelezaji wa sekta ya madini hususani wachimbaji wadogo.
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Profesa Idrisa Kikula akizungumza jambo wakati wa
hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Katente wilayani
Bukombe mkoani Geita tarehe 26 Aprili, 2020.
Amesema katika kutimiza azma hiyo, Serikali ilianzisha mradi wa
Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) uliokuwa na awamu mbili,
ya kwanza ni kuanzia 2009 hadi 2014 na awamu ya pili mwaka 2015 hadi
2018 ambapo awamuya pili ya mradi ndipo viwanda vitatu vya mfano vya
uchenjuaji wa dhahabu vya Katente- Bukombe, Lwamgasa- Geita na Itumbi
–Chunya vilipoanza kujengwa baada ya kufanyika kwa utafiti wa kijiolojia
chini ya ushirikiano baina ya uongozi wa mradi, Stamico, Taasisi ya
Utafiti na Jiolojia Tanzania (GST) na wachimbaji wadogo.
Akizungumzia gharama ya ujenzi wa viwanda hivyo Ollal alisema mradi
wa Katente umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.7 na Lwamgasa
umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.3 wakati mradi wa Itumba
Uligharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.7 na hivyo kufanya miradi yote
kutekelezwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 4.7.
Mwakilishi
wa Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico Lucas Seleli akizungumza jambo mara
baada ya uzinduzi na makabidhiano ya Viwanda viwili vya uchenjuaji wa
Madini ya dhahabu kisichotumia kemikali ya zebaki vilivyoko Katente na
Lwamgasa mkoani Geita.
Ollal ameongeza kuwa, uwepo wa tekinolojia hii kwa wachimbaji wadogo
itakuwa na manufaa kama vile; kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali migodini
kwa kutumia sementi katika kuimarisha kuta, kurahisisha utoaji wa mbale
mgodini(Haulage system) kupunguza athari za kimazingira kwa kutokata
miti hovyo na kurahisisha ufungaji wa migodi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara y aMadini, Prof. Simon Msanjila
amelitaka Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuisaidia jamii
inayozunguka viwanda hivyo vya mfano kuondokana na changamoto ya maji
kwa kuchimba kisima kiwandani hapo na kuiruhusu jamii kunufaika na
huduma hiyo.
Aidha, Prof. Msanjila amewataka Stamico kutoa nafasi za ajira kwa
wananchi kutokana na ukweli kwamba wao ndio walinzi wa viwanda hivyo.
“Nitashangaa sana kuona wafanyakazi wakawaida wanatoka km 200 kutoka
hapa wakati kijiji kimezungukwa na vijana mahiri na wachapa kazi”
alisistiza Prof. Msanjila.
Viongozi
wa Serikali kuanzia kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel
akifuatiwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Madini, Profesa Simon Msanjila na mwisho ni Mshauri mwelekezi
aliyesimamia ujenzi wa viwanda vya kuchenjua dhahabu Rogers Sezigwa
wakiendelea na ukaguzi wa kiwanda hicho kabla ya kukikabidhi rasmi kwa
Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert
Gabriel ametoa wito kwa watendaji na wasimamizi wa vituo hivyo kuwa
wazalendo katika usimamizi wa Viwanda hivyo vya uchenjuaji wa dhahabu.
Sanjari na hilo, ameelezea mikakati ya mkoa wake kuelekea maonesho ya
Tekinolojia ya uchimbaji wa madini kwa mwaka huu kuwa ni pamoja na mkoa
wake kuandaa uwanja maalum kwa ajili ya maonesho hayo ambapo tayari
ujenzi wa jengo la ofisi mbalimbali ikiwepo ya wataalamu wa Sekta ya
madini umefanyika.
Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wataalamu na timu nzima ya Ujenzi wa
viwanda hivi kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo ili kuachilia
utaalamu wao kwa watanzania wengine wenye nia ya kujiendeleza kupitia
sekta ya Madini.
No comments:
Post a Comment