 |
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa apokea hundi ya Sh. 500,000,000/= kutoka kwa
Kampuni ya Export Trading Group, ukiwa ni mchango wa Kampuni hiyo kwa
ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za mapambano dhidi ya ugonjwa
wa homa kali ya mapafu- COVID - 19. Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye
Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 14, 2020. ( Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amepokea hundi ya mfano ya sh. milioni 500 kutoka
kampuni ya Export Trading Group (ETG) zikiwa ni msaada kwa ajili ya
kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaotokana na maambukizi ya
virusi vya corona (COVID-19) nchini.
Waziri Mkuu amepokea msaada huo leo (Jumanne, Aprili 14, 2020) ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma, kutoka kwa Mkurugenzi mkazi wa ETG, Bw. Nilladri Chowdhury aliyefuatana na maafisa uhusiano wa kampuni hiyo, Bw. Frank Mtui na Bi. Fatma Salum Ally.
Akizungumza
mara baada ya kupokea kupokea msaada huo, Waziri Mkuu amewashukuru
watendaji wa kampuni ya ETG kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika
mapambano dhidi ya virusi vya corona, ambapo hadi sasa kesi 49
zimeripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huo nchini na wagonjwa saba
wameshapona.
“Kwa
niaba ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tunawashukuru kwa
msaada huu ambao utaisadia Serikali kupunguza makali ya kuwahudumia
wananchi wetu. Tunahitaji kuungwa mkono na wadau wengine kama ninyi,”
amesema.
| |
 |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na uongozi wa Kampuni ya Export Trading Group, baada ya kupokea hundi ya Sh. 500,000,000/= , ikiwa ni mchango wa Kampuni hiyo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu- COVID - 19. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 14, 2020. Kutoka kushoto ni Afisa Uhusiano, Fatma Ally, Afisa Uhusiano, Frank Mtui na Kiongozi wa Kampuni (Tanzania) Niladri Choudhury. |
Waziri
Mkuu amewataka wananchi wote wazidishe kuchukua tahadhari dhidi ya
ugonjwa huo hasa katika kipindi hiki. “Hatua tuliyofikia hivi sasa,
maambukizi yameanza kuongezeka hasa kwa Dar es Salaam na Zanzibar.
Tunajua kule kuna watu wengi na shughuli zote za kiuchumi zinaanzia
pale, lakini hatuna budi kufuata masharti tuliyopewa ili kuzuia ugonjwa
huu usisambae,” amesema.
“Serikali
inatoa msisitizo kwa wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa kuhusu
kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ikiwemo kunawa mikono kwa
sabuni na maji tiririka pamoja na kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya
lazima.”
“Muhimu zaidi sote tuendelee kumuomba Mwenyezi Mkungu ili atupunguzie makali ya ugonjwa huu,” amesisitiza.
Mapema, akizungumza
kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kampuni ya ETG, Bw. Mahesh Patel, Mkurugenzi
Mkazi wa ETG, Bw. Nilladri Chowdhury alisema wameamua kuchangia ili
kuunga mkono juhudi za Serikali katika vita ya kupambana na ugonjwa huo.
“Mwenyekiti
wetu amesafiri lakini kama kampuni, tumeamua kuungana na Serikali
katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu, na ametutuma tutoe mchango wa
shilingi milioni 500. Tuna imani na tunaendelea kumuomba Mungu ili
atuvushe katika kipindi hiki,” alisema.
Alisema
kampuni yao inashughulika na masuala ya kilimo zikiwemo kusambaza
pembejeo na kuongeza thamani mazao kupitia kampuni yao ya Kapunga
iliyoko Mbeya, viwanda vitatu vya kubangua korosho vilivyoko Mtwara,
Newala na Tunduru na viwanda vya kusindika mbegu za mafuta.
Pia wanatoa soko kwa wakulima kwa kununua mazao kama vile korosho, mbaazi, kokoa, mahindi, choroko na ufuta.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMANNE, APRILI 14, 2020.
No comments:
Post a Comment