Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango |
MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA NAMIPANGO
KWA MWAKA 2020/21
1.0
TANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na taarifa
iliyowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Bajeti, iliyochambua bajeti za
mafungu ya Wizara ya Fedha na Mipango
pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa
mwaka 2020/21, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na
kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha na
Mipango kwa mwaka 2019/20 na kuidhinisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya mafungu saba (7) ya Wizara pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa
mwaka 2020/21.
2.
Mheshimiwa Spika, awali ya
yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia afya njema pamoja na kutuwezesha kuendelea kutekeleza
majukumu yetu kwa Taifa na leo amenipa kibali kusimama mbele ya Bunge lako
Tukufu kuwasilisha Mpango na Bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka ujao wa fedha.
3.
Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa dhati kabisa, napenda kutoa shukrani zangu
kwa kiongozi wetu, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kusimamia Wizara ya
Fedha na Mipango kwa kipindi chote cha muhula wa kwanza wa Serikali yake. Ni
heshima kubwa kwangu kufanya kazi chini ya Kiongozi Mkuu wa nchi huyu ambaye
ana upeo mkubwa sana, mchapa kazi, mwenye uzalendo wa kweli na ambaye
ameistaajabisha dunia kwa kutekeleza mambo makubwa ya kimaendeleo kwa kipindi
kifupi. Itoshe tu kusema namshukuru sana, naendelea kumuombea afya njema yeye
na familia yake ili kazi kubwa aliyoianza ya kuwaletea maendeleo makubwa wananchi wa Tanzania iweze kukamilika.
Ahadi yangu kwa Mheshimiwa Rais na Watanzania ni kuwa, nitaendelea kuchapa kazi
katika kipindi chote cha utumishi wangu ili kuenzi nafasi hii adhimu
niliyokabidhiwa ya kutoa mchango wangu kwa mama Tanzania.
4.
Mheshimiwa Spika, vilevile, napenda
nitumie jukwaa hili kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati kabisa, Mhe. Samia
Suluhu Hassan, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Kassim M. Majaliwa (Mb.),
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna walivyojitoa katika
kuwahudumia Watanzania. Nimefurahi kufanya kazi chini yao na ninawasihi
Watanzania kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia wasaidizi hawa waandamizi wa
Mheshimiwa Rais ambao ni makini na wenye mapenzi ya dhati kwa nchi yao. Tuendelee
kwa pamoja kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili waendelee kuwa na afya njema na pia hekima na busara katika
kazi zao za kumsaidia Kiongozi Mkuu wa Nchi.
5.
Mheshimiwa
Spika, napenda
kukupongeza wewe binafsi, kwa kusimamia mhimili huu wa Bunge kwa umahiri mkubwa
sana. Aidha, ninakupongeza pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote
wa Bunge kwa kuongoza vyema majadiliano ya Bajeti za Wizara mbalimbali. Naomba pia nitumie fursa hii
kuishukuru kipekee Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake
Mhe.
Mashimba Mashauri Ndaki (Mb.), kwa maoni,
ushauri na mapendekezo mazuri waliyotupatia wakati wa kuchambua mapendekezo ya
Bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka 2020/21. Nakiri kwamba mimi binafsi, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb.), Naibu Waziri na Watendaji wa Wizara yetu na taasisi zake
tumejifunza mambo mengi mazuri kutokana na hoja na ushauri wa Kamati hii nyeti.
Vile vile, napenda
nitumie fursa hii, kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wote wa Serikali ya
Awamu ya Tano kwa kusimamia majukumu ya Wizara zao vizuri na kupelekea
kupatikana kwa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi 2015 - 2020.
6.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie pia nafasi
hii kumpongeza sana Comred Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.) kwa kuteuliwa
kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Aidha, natoa pole kwa Bunge lako Tukufu kwa
kumpoteza Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga aliyekuwa Mbunge wa
Kuteuliwa - CCM na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Rashid Ajali Akbar,
aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini-CCM, Mhe. Mchungaji Dkt. Getrude
Pangalile Rwakatare, aliyekuwa Mbunge Viti Maalum – CCM na Mhe. Richard Mganga
Ndassa (Senator) aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumve-CCM. Tunawaombea ili wapate
rehema kwa Mungu, wapumzike kwa amani. Amina.
7.
Mheshimiwa
Spika, namshukuru sana Mheshimiwa
Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge makini wa Kondoa na Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango, kwa msaada mkubwa anaonipatia katika kutekeleza majukumu ya Wizara.
Nampongeza sana kwa uchapakazi na kujitoa kwake na napenda niwaombe Wananchi wa
Jimbo la Kondoa wamrejeshe kwa kishindo mama huyu Hodari katika Bunge lijalo.
Aidha, nawashukuru sana watumishi wote wa Wizara ya Fedha na Mipango
wakiongozwa na Katibu Mkuu ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto M.
James, Naibu Makatibu Wakuu Bi. Amina Kh. Shaaban, Bw. Adolf H. Ndunguru na Bi.
Mary N. Maganga kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekeleza majukumu ya
Wizara. Vile vile, nawashukuru Wakuu wa Mashirika na Taasisi zilizo chini ya
Wizara ya Fedha na Mipango (CAG, BOT, TRA, NBS, TR, TRAT, TRAB, Benki za Serikali, Taasisi 5 za mafunzo ya Elimu ya
Juu na Bodi za Kitaaluma na Kitaalam) pamoja na watumishi wote wa taasisi hizo
kwa ushirikiano walionipatia katika kipindi chote cha utumishi wangu kama
Waziri wa Fedha na Mipango.
8.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye hoja
yangu. Nitaanza kwa kuelezea mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya
Wizara kwa mwaka 2019/20, maeneo ya kipaumbele pamoja na mikakati mbalimbali
ambayo itatekelezwa na Wizara kwa mwaka 2020/21. Aidha, nitawasilisha Mpango na
Bajeti ya mwaka 2020/21 kwa mafungu saba (7) ya Wizara ambayo ni Fungu 7 –
Ofisi ya Msajili wa Hazina, Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha, Fungu 13 –
Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu, Fungu 21 – HAZINA, Fungu 22 – Deni la Taifa
na Huduma Nyingine, Fungu 23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali na Fungu 50 –
Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Fungu 45 - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
2.0. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA
WIZARA KWA MWAKA 2019/20 NA MALENGO YA MWAKA 2020/21
Mapitio ya Mapato na Matumizi
9.
Mheshimiwa Spika,
mapitio ya mapato na matumizi ya Wizara
kwa mwaka wa fedha 2019/20 ni kama inavyooneshwa katika hotuba yangu
kuanzia ukurasa wa 5 hadi ukurasa wa 8.
Utekelezaji wa Majukumu kwa mwaka 2019/20 na Mpango wa Mwaka 2020/21
10.
Mheshimiwa
Spika, naomba kulielekeza Bunge
lako Tukufu kwa ufupi juu ya utekelezaji wa majukumu ya
Wizara kwa kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi Machi 2020 pamoja na Mpango na
Bajeti ya mwaka 2020/21. Maelezo ya kina yapo katika hotuba yangu ukurasa wa 8
hadi wa 33.
(i) Kubuni na Kusimamia Utekelezaji wa Sera za Uchumi Jumla
11.
Mheshimiwa
Spika, Pato la Taifa limekua kwa
asilimia 7.0 mwaka 2019, kama ilivyokuwa mwaka 2018. Sekta zilizoongoza katika
ukuaji ni pamoja na Uchimbaji wa Madini na Mawe asilimia 17.7, Ujenzi asilimia
14.1, Sanaa na Burudani asilimia 11.2 na Usafirishaji na Uhifadhi wa Mizigo
asilimia 8.7. Sekta zilizokuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa kwa mwaka
2019 ni: Kilimo (asilimia 26.6); Ujenzi (asilimia 14.3); Biashara na
Matengenezo (asilimia 8.8); Viwanda (asilimia 8.5) na Usafirishaji na Uhifadhi
mizigo (asilimia 6.9). Aidha, mfumuko wa bei umeendelea kubaki katika wigo wa
tarakimu moja ambapo kwa mwezi Machi 2020, ulikuwa asilimia 3.4.
12.
Mheshimiwa
Spika, kutokana
na uchambuzi wa awali, shabaha za uchumi jumla katika mwaka 2020/21 ni kama ifuatavyo: Pato halisi
la Taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 4.0 mwaka 2020; mfumuko wa bei kubaki
katika wigo wa tarakimu moja; nakisi ya bajeti ya Serikali kufikia asilimia 2.8;
mapato ya ndani asilimia 14.5 ya Pato la Taifa; na mapato ya kodi asilimia 12.5
ya Pato la Taifa. Matarajio haya yanatarajiwa kupungua kutegemea ukubwa wa
athari za mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu (unaosababishwa na Virusi
vya CORONA) kwenye sekta mbalimbali.
(ii) Uandaaji, Utekelezaji na Usimamizi wa Mikakati, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali
13.
Mheshimiwa
Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2020, Wizara ilifanikiwa kuandaa Mapendekezo ya
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21; kuandaa taarifa ya Hiari ya
Nchi Kuhusu Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs); kuunda
mfumo wa kitaasisi wa ufuatiliaji na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa
Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 pamoja na mfumo wa awali (prototype) wa Kanzidata ya Kuhifadhi na Kutoa Taarifa za Miradi ya
Maendeleo.
14.
Mheshimiwa Spika, Wizara imechukua
hatua za kimkakati za kuimarisha ukusanyaji wa mapato kama zinavyoonekana
katika hotuba yangu ukurasa wa 11 hadi wa 14. Hatua hizo zimeiwezesha Serikali
kukusanya mapato ya ndani ya jumla ya shilingi trilioni 16.06 katika kipindi
cha Julai 2019 hadi Machi 2020, sawa na asilimia 92.4 ya lengo. Mapato ya ndani
yameongezeka
kutoka shilingi trilioni 14.07 hadi shilingi trilioni 16.06, sawa na asilimia 14.2 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka
2018/19.
15.
Mheshimiwa Spika, kati ya Julai 2019 na Machi
2020, Wizara imefanikisha upatikanaji wa fedha za misaada na mikopo nafuu ya
jumla ya shilingi trilioni 2.04 sawa
na asilimia 93 ya lengo la kipindi hicho la shilingi trilioni 2.78. Aidha, Wizara imefanikisha mkopo wa kiasi cha shilingi trilioni
3.44 kutoka katika soko la
ndani, sawa na asilimia 101.5 ya lengo la kukopa shilingi trilioni 3.39 na
mkopo wa shilingi trilioni 1.82
kutoka soko la nje sawa na asilimia 78.66 ya lengo la kukopa shilingi
trilioni 2.32.
16.
Mheshimiwa Spika,
hadi kufikia mwezi Machi 2020, jumla ya shilingi
trilioni 24.65 zilitolewa
kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali. Kati ya
kiasi hicho, shilingi trilioni 1.16 zimetolewa
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kielelezo na shilingi bilioni 597.54 kwa ajili ya kulipa madai yaliyohakikiwa.
Aidha, jumla ya shilingi bilioni 33.98
sawa na asilimia 84.95 ya bajeti iliyotengwa zimetolewa kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi 18 ya kimkakati inayotekelezwa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa.
(iii) Kubuni, Kuunda na Kusimamia Mifumo ya Usimamizi wa Fedha na Mali za Umma
17. Mheshimiwa
Spika, Wizara imeboresha
Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG)
kwa kuongeza huduma kwa njia ya simu za kiganjani (GePG application mobile) na kwa kuunganisha mfumo huo na mifumo ya
Mamlaka ya Mapato Tanzania ya ukusanyaji wa mapato. Utekelezaji wa jukumu la
kubuni, kuunda na kusimamia mifumo ya usimamizi wa fedha na mali za umma
umefafanuliwa kwa kina katika hotuba yangu ukurasa wa 14 hadi wa 15.
(iv) Usimamizi wa Sekta ya Fedha
18. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2020,
Wizara imefanikiwa kukamilisha uandaaji wa Kanuni za Sheria ya Huduma
Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 ambapo zilianza kutumika rasmi mwezi Novemba 2019.
Aidha, Wizara imeanza kutekeleza Mpango Maalum wa Elimu kwa Umma kuhusu sekta
hii ili kujenga uelewa kwa wananchi. Vile vile, Wizara imekamilisha kuandaa Mpango Kabambe wa
Maendeleo ya Sekta ya Fedha pamoja na Kanuni za Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za
Fedha. Ukurasa wa 16
-17 wa hotuba yangu unaainisha kwa kina kazi nyingine zilizofanyika
katika kutekeleza jukumu hili muhimu kwa uchumi wetu kati ya Julai 2019 na
Machi 2020.
(v) Usimamizi wa Deni la Serikali
19.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2020, Serikali ilifanikiwa
kulipa deni lake lote lililoiva lenye thamani ya shilingi trilioni 6.19. Kati ya kiasi hicho, Deni la Ndani ni shilingi trilioni 4.06
ikijumuisha riba shilingi trilioni 1.09
na mtaji shilingi trilioni 2.98. Aidha, Deni la Nje ni shilingi trilioni 2.13
ikijumuisha riba ya shilingi bilioni 636.75 na mtaji shilingi trilioni 1.49.
(vi) Ubia kati ya Sekta ya umma na sekta binafsi
20. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2020, Wizara imefanikisha
kutungwa kwa Kanuni za Sheria ya Ubia za Mwaka 2020 na
kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na.37. Aidha, Wizara imeendelea kupokea, kuchambua na kutoa ushauri kwa Mamlaka za Serikali
zinazotekeleza miradi ya PPP ipatayo 10 ambayo ipo katika hatua za awali za
kutafuta wabia, washauri elekezi, kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
21. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2020/21, Wizara inatarajia kukamilisha taratibu za kuanzisha kituo cha
ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi - PPP Center.
(vii) Usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma
22.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea kutekeleza
jukumu lake la Usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kama inavyooneka katika hotuba yangu ukurasa wa 23 -24. Aidha, hadi kufikia mwezi Machi 2020, Mfuko
Mkuu wa Serikali umepokea jumla ya shilingi bilioni 612.87 kutoka kwenye
Taasisi na Mashirika ya Umma kama gawio na michango ya Mashirika.
(viii) Taasisi za Mafunzo ya Elimu ya Juu na Bodi za Kitaaluma na Kitaalamu
23.
Mheshimiwa
Spika, Wizara
inasimamia Taasisi tano (5) za mafunzo ya elimu ya juu na Bodi mbili (2) za
kitaaluma na kitaalamu ambazo ni: Chuo cha Usimamizi wa Fedha -IFM; Chuo cha
Mipango ya Maendeleo Vijijini – IRDP; Taasisi ya Uhasibu Tanzania –
TIA; Chuo cha Uhasibu Arusha –IAA; Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika – EASTC;
Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi – PSPTB na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na
Wakaguzi wa Hesabu – NBAA. Utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo na mpango wa
utekelezaji kwa mwaka 2020/21 ni kama inavyoonekana katika kitabu cha hotuba
yangu ukurasa wa 24 -27.
(ix) Mafao ya Wastaafu na Mirathi
24.
Mheshimiwa Spika, kati ya
mwezi Julai 2019 na Machi 2020, Wizara imelipa mafao na pensheni kwa wastaafu wa
Serikali 57,605, mirathi kwa warithi 1,006 na malipo ya kiinua
mgongo kwa watumishi 457 wa Serikali walio kwenye mikataba. Aidha,
Wizara imeandaa vitambulisho vipya vya wastaafu vya kielektroniki katika mfumo
wa “smart cards” na kuboresha Mfumo wa unaotumika kutoa huduma kwa
njia ya mtandao na kudhibiti fedha za mirathi zinazotoka HAZINA kwenda moja kwa
moja kwenye akaunti za warithi (Tanzania Pensioners Payment System – TPPS).
(x) Tume ya Pamoja ya Fedha
25.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20,
Tume ya Pamoja ya Fedha imefanya stadi
maalum kuhusu Mfumo wa Biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar na Mwenendo
wa Mapato ya Muungano. Aidha, Tume imefanya uchambuzi wa taarifa na takwimu halisi za
Mapato na Matumizi ya Muungano kwa mwaka 2017/18, mwaka 2018/19 na 2019/20. Taarifa ya uchambuzi wa takwimu hizo
ilijadiliwa na Sekretarieti ya Tume mwezi Februari, 2020 na Serikali za pande
zote zinaendelea kufanyia kazi mapendekezo yaliyomo katika taarifa hiyo.
(xi) Sekta ya Michezo ya kubahatisha
26. Mheshimiwa Spika,
hadi kufikia mwezi Machi 2020, Wizara imewezesha marekebisho ya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha SURA 41 ili
kuipa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha mamlaka ya kuratibu, kusimamia na
kudhibiti matangazo ya michezo ya kubahatisha. Aidha, Bodi inaendelea kuunda na kuunganisha
mifumo ya TEHAMA ili kuimarisha udhibiti wa michezo ya kubahatisha.
(xii) Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi
27. Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwenye matumizi ya rasilimali
za umma, hadi kufikia Machi 2020, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imefanya ukaguzi
kwa mafungu 66 ya Wizara na Idara za Serikali; Wakala 33; Taasisi
48; Balozi 42; Vyama vya Siasa 19; Bodi za Mabonde ya Maji
14; Hospital za Rufaa 27, Mashirika ya Umma 150; Mamlaka za Serikali za Mitaa 185;
Mikoa 26; na Mifuko Maalumu 16. Aidha, ofisi imefanikiwa kufanya ukaguzi wa usimamizi wa
mikataba ya ujenzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 19. Vile vile,
ukaguzi umefanyika kwa miradi ya maendeleo 435 ikijumuisha miradi 65
ya Serikali Kuu na miradi 370 ya Serikali za Mitaa.
28. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2020/21, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imepanga kuimarisha ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo hadi ngazi za Tarafa, Kata na Vijiji; kufanya
ukaguzi wa miradi mikubwa ya maendeleo (Reli ya Kisasa, Vivuko, Bomba la Gesi Mtwara na Ukarabati
wa Reli ya Kati); kupanua mawanda ya ukaguzi katika eneo la uchimbaji wa
madini, mafuta na gesi ikiwemo kuimarisha ukaguzi wa kiuchunguzi na
kiufundi; na kuendelea kufanya ukaguzi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa,
Mashirika ya Umma pamoja na kufanya ukaguzi wa ufanisi.
Changamoto
29.
Mheshimiwa
Spika, utekelezaji wa majukumu ya Wizara unakabiliwa na changamoto mbalimbali
ambazo tunaendelea kukabiliana nazo kwa kushirikiana na
wadau wengine ili zisilete athari hasi katika malengo tuliyojiwekea. Baadhi ya
changamoto hizo ni:
(i) Kasi
ndogo ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu za maendeleo katika
Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Taasisi za Umma, Sekretarieti za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
(ii) Mabadiliko
ya mara kwa mara ya teknolojia ya mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato
yanayoleta uhitaji wa upatikanaji wa teknolojia mpya na kuboresha na kuhuisha
teknolojia ya mifumo iliyopo ili kuongeza ufanisi;
(iii) Kuongezeka kwa gharama za mikopo kwenye masoko ya fedha duniani kutokana na mabadiliko ya sera za fedha katika nchi zilizoendelea (hususan Marekani na Nchi za
Ulaya);
(iv) Uharibifu
wa miundombinu ya barabara na madaraja kutokana na mafuriko; na
(v) Mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na
virusi vya corona (COVID-19).
Mikakati ya Kukabiliana na Changamoto
30.
Mheshimiwa Spika, Baadhi ya hatua zinazochukuliwa na Wizara katika kukabiliana na
changamoto za utekelezaji wa majukumu yake ni pamoja na:
(i)
Kuanza
mchakato wa kutunga sera na mkakati wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na
programu za maendeleo;
(ii)
Kujenga
uwezo wa wataalam wa ndani katika kubuni, kuunda na kuhuisha teknolojia ya
mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato;
(iii)
Kuhamasisha
wadau wa ndani kuendelea kushiriki katika minada ya dhamana za Serikali pamoja na
kutafuta vyanzo vingine vya mikopo ya nje vyenye riba nafuu; na
(iv) Wizara imekamilisha uchambuzi wa taarifa mbalimbali za
kisekta ili kubaini kiwango cha athari zitokanazo na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu
inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) katika uchumi na kuainisha mikakati
ya muda mfupi, wa kati na mrefu ya kukabiliana nazo. Taarifa jumuishi ya
mikakati ya kupambana na CORONA imewasilishwa kwenye ngazi za maamuzi
Serikalini.
3.0 MAKADIRIO
YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2020/21
(i)
Makadirio
ya Mapato
31. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Wizara inakadiria kukusanya
maduhuli ya kiasi cha shilingi bilioni
973.02 kutoka katika vyanzo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na gawio, kodi za
pango, marejesho ya mikopo, michango kutoka katika taasisi na mashirika ya
umma, mauzo ya leseni za udalali na nyaraka za zabuni. Mchanganuo wa maduhuli
yanayokadiriwa kukusanywa umeoneshwa katika kitabu cha hotuba ukurasa wa 34 katika
Jedwali Na. 4.
(ii)
Makadirio ya Matumizi
32.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2020/21, Wizara ya Fedha na Mipango
inaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi trilioni 12.39 kwa
mafungu yote
saba (7) kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 11.73 ni
kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 659 kwa
ajili ya matumizi ya maendeleo. Kati ya matumizi ya kawaida, shilingi trilioni 10.48 kwa ajili ya deni la Serikali, shilingi bilioni 750.29 matumizi
mengineyo na shilingi bilioni 510 kwa ajili ya mishahara na marekebisho
ya mishahara. Aidha, matumizi ya maendeleo yanajumuisha shilingi bilioni
624.7 fedha za ndani na shilingi bilioni 34.61 fedha za nje.
33.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2020/21, Fungu 45 – Ofisi ya Taifa
ya Ukaguzi inaomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 80.5 kwa
ajili ya matumizi ya kawaida na ya
maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 68.87 ni kwa ajili ya
matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 11.66 matumizi ya
maendeleo. Matumizi ya kawaida yanajumuisha shilingi bilioni 14.88 kwa
ajili ya mishahara na shilingi bilioni 53.99 matumizi mengineyo. Aidha,
matumizi ya maendeleo yanajumuisha shilingi bilioni 6.70 fedha za ndani
na shilingi bilioni 4.96 fedha za nje. Mchanganuo wa kiasi
kinachoombwa kwa kila fungu umeainishwa katika Jedwali Na. 5 lililopo katika
hotuba yangu ukurasa wa 35.
34.
Mheshimiwa
Spika, kama nilivyotangulia kusema awali, Mkutano huu wa
Bunge ni wa mwisho katika muhula huu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Napenda kutumia fursa hii kukiri kuwa, katika kipindi chote cha muhula huu,
Wizara imenufaika sana na maoni na ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao umesaidia
kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha uchumi wa nchi yetu.
35.
Mheshimiwa
Spika, kwa mara nyingine, naomba nirudie kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa
kuniwezesha kufanya kazi yake hii ya Waziri wa Fedha na Mipango aliyonipa
kupitia Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Aidha, namshukuru tena Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuniamini
katika nafasi hii ngumu kwa miaka mitano mfululizo. Vilevile, napenda kuwashukuru wananchi wote wa
Tanzania hususan kwa kufanya kazi na kulipa kodi ili kujenga uchumi wa nchi yetu.
Nawaomba Watanzania tuendelee kuchapa kazi kama anavyotuasa Mheshimiwa Rais
wetu na kuitekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya “HAPA KAZI TU”.
36.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na janga la mlipuko wa ugonjwa
wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19), napenda kuchukua fursa
hii kutoa pole kwa wananchi wote waliopatwa na madhara yanayotokana janga hili na kuwaasa kuendelea
kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huu kama inavyoelekezwa na wataalamu wa
afya. Aidha, napenda kuwapongeza kwa dhati madaktari na watumishi wote wa Afya
walio mstari wa mbele siku zote katika kutoa huduma kwa wananchi hasa wanyonge
na hususan katika kipindi hiki cha mlipuko wa COVID-19 nchini.
37.
Mheshimiwa
Spika, mwisho kabisa, napenda nikushukuru tena kwa kunipa nafasi ya
kuwasilisha hoja hii pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.
Aidha, nawashukuru wote walioshiriki katika maandalizi ya hotuba hii
na kuhakikisha inakamilika kwa wakati. Hotuba hii inapatikana katika tovuti ya
Wizara kwa anuani ya www.mof.go.tz.
38.
Mheshimiwa
Spika, naomba
kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment