Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia Wabunge wakati akifunga Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 16 June 2020.
HOTUBA YA RAIS MAGUFULI, WAKATI WA KULIHUTUBIA KWA MARA YA MWISHO BUNGE LA 11 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, UKUMBI WA BUNGE, DODOMA, TAREHE 16 JUNI, 2020
Mheshimiwa Spika;
Awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aliyetujalia uhai na kutuwezesha kuiona siku ya leo. Kama, Mheshimiwa Spika unavyofahamu, wapo wenzetu ambao tulikuwa nao wakati wa kuzindua Bunge hili, lakini leo hatuko nao. Wametangulia mbele za haki. Hivyo basi, kwa heshima yao naomba tusimame kwa dakika moja kuwakumbuka. Mwenyezi Mungu azipumzishe roho zao mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea zaidi, naomba kutambua uwepo wa viongozi mbalimbali kwenye Ukumbi huu. Nimefurahi kuwaona Waheshimiwa Marais wetu Wastaafu wote wapo hapa, pamoja na Makamu wa Rais Wastaafu na pia Mawaziri Wakuu wastaafu, akiwemo Mheshimiwa Lowasa na Mheshimiwa Sumaye. Hii ndiyo Tanzania.
Kwa namna ya pekee, napenda nikushukuru wewe, Mheshimiwa Spika, Job Ndugai, Mbunge wa Kongwa, kwa kunipa kibali cha kuja kulihutubia Bunge hili. Aidha, nawashukuru Naibu Spika, Mheshimiwa Tulia Ackson, pamoja na Wenyeviti wa Bunge, Mheshimiwa Andrew Chenge na Mheshimiwa Najma Giga, kwa ushirikiano wenu. Ahsanteni sana. Hiki ni kielelezo cha uhusiano mzuri uliokuwepo kati ya mihimili yetu mitatu katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita.
Nitumie fursa hii pia kueleza kuwa, tangu nimeingia ndani ya Bunge hili leo nimeshuhudia mabadiliko mengi makubwa, tofauti na ilivyokuwa wakati mimi nikiwa Mbunge. Hivi sasa nimeona hata Waheshimiwa Wabunge wanatumia vifaa vya kisasa kama vile tablets. Enzi zetu, vifaa hivyo, havikuwepo. Hivyo basi, nakupongeza sana Mheshimiwa Spika kwa ubunifu huu; na nawapongeza pia Waheshimiwa Wabunge kwa kuweza kuvitumia vifaa hivi; na hivyo kulifanya Bunge lenu kuwa la kisasa namna hii.
Mheshimiwa Spika;
Tarehe 20 Novemba 2015, nilikuja hapa kulizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Leo tena, kwa madhumuni ya kutimiza matakwa ya Katiba yetu, nimekuja kulihutubia kwa mara ya mwisho, ili hatimaye kuweza kuruhusu kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2020.
Utakumbuka, Mheshimiwa Spika, kuwa wakati nikizindua Bunge lako Tukufu, nilitumia fursa hiyo pia kutoa mwelekeo, kueleza malengo na pia kutaja vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano. Siku ile, nakumbuka, nilieleza mambo mengi sana, ambayo nafarijika kuona kuwa mengi tumefanikiwa kuyatekeleza, kama ambavyo Waheshimiwa Mawaziri mbalimbali walieleza wakati wakiwasilisha Bajeti zao. Namshukuru pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambaye naye wakati wa kuwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Serikali alitoa ufafanuzi wa mafanikio tuliyoyapata. Aidha, jana, Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelezo ya kina kuhusu mafanikio yaliyopatikana.
Kwa ujumla, naweza kusema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumeweza kutimiza wajibu wetu wa kuwatumikia Watanzania kwa kiasi kikubwa. Na tumeweza kufanya hivyo kutokana na ushirikiano mkubwa tulioupata kutoka kwa Watanzania wote. Nitumie fursa hii kuwashukuru ninyi Waheshimiwa Wabunge kwa kuishauri vyema na pia kuisimamia vizuri Serikali katika kutekeleza majukumu yake. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Madiwani kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye maeneo yao. Kama mnavyofahamu, Madiwani ni kiungo muhimu kati ya wananchi na Serikali; lakini pia kati yenu Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi. Hivyo, hatuna budi kuwashukuru Waheshimiwa Madiwani wetu.
Napenda pia nitumie fursa hii kuwashukuru watangulizi wangu - kuanzia Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Baba ya Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; Awamu ya Pili, iliyoongozwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi; Awamu ya Tatu ya Mzee Benjamin William Mkapa pamoja na Awamu ya Nne ya Mzee Jakaya Mrisho Kikwete– kwa kuweka misingi imara na kutengeneza mazingira yaliyowezesha kupatikana mafanikio hayo mbalimbali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Na katika hilo, nawashukuru pia viongozi wetu wakuu wastaafu; Mzee wetu Mwinyi (Mzee Ruksa), Mzee wetu Mkapa (Mzee wa Ukweli na Uwazi) na Mzee Kikwete (Mzee wa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya) kwa ushauri wao mbalimbali waliotupatia katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita. Nikiri tu kwamba ushauri wao umenisaidia sana mimi binafsi pamoja na Serikali ninayoingoza. Nawashukuru pia Makamu wa Rais Wastaafu, Marais wa Zanzibar Wastaafu na Mawaziri Wakuu Wastaafu kwa ushirikiano wao.
Mheshimiwa Spika;
Kama utakavyokumbuka, mojawapo ya ahadi kubwa niliyoitoa wakati wa kuzindua Bunge ilikuwa kudumisha amani, umoja, mshikamano, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na Muungano wetu; na halikadhalika kuimarisha amani, ulinzi, usalama na utulivu wa nchi yetu. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba tumeitimiza ahadi hiyo kwa vitendo.
Watanzania tumebaki kuwa wamoja na tumeendelea kushirikiana licha ya tofauti zetu za dini, kabila, rangi, ufuasi vyama vya siasa au mahali tunakotoka. Muungano wetu pia umeendelea kuimarika. Tumeweza kushughulikia baadhi ya changamoto za Muungano na kufikia makubaliano, ikiwemo kuhusu suala la gharama za kushusha mizigo {landing fees) na pia kufuta kodi ya ongezeko la thamani pamoja na malimbikizo ya kodi hiyo ya shilingi bilioni 22.9 ambayo Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) lilikuwa likidaiwa na TANESCO. Tumefanikiwa pia kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Kuhusu amani, ulinzi na usalama, nchi yetu imeendelea kuwa Kisiwa cha Amani na mipaka yake imebaki kuwa salama. Utakumbuka kuwa, wakati tukiingia madarakani, kulikuwepo na wimbi kubwa la uhalifu wa kutumia silaha pamoja na vitendo vingine vya kihalifu, ikiwemo matukio ya mauaji kule Kibiti na Rufiji. Hata hivyo, kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, vitendo vyote hivyo vilikomeshwa, na nchi yetu sasa ipo salama. Na katika kuthibitisha hilo, Ripoti ya Global Peace Index ya Mwaka 2020 imeitaja Tanzania kushika nafasi ya kwanza kwa amani na utulivu kwenye eneo la Afrika Mashariki na ya saba kwa nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa niaba yenu na kwa niaba ya Watanzania wote, navipongeza sana vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kusimamia amani nchini. Nawashukuru pia Watanzania kwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumejitahidi pia kuimarisha maadili, nidhamu na utendaji kazi Serikalini. Kama tulivyoahdi, hatukuwa na mzaha kwa viongozi na watumishi wazembe, walioshindwa kufanya kazi kwa weledi, nidhamu, maarifa na uadilifu. Viongozi na watumishi wa namna hiyo walichukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwemo “kuwatumbua”, kuwashusha vyeo na mishahara, au kuwapa onyo kali.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, jumla ya watumishi 32,555 wamechukuliwa hatua mbalimbali, wakiwemo watumishi 15,508 ambao waliachishwa kazi kwa kukutwa na vyeti vya kughushi. Aidha, tulifuta ajira hewa 19,708 zilizoigharimu Serikali kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni 19.8. Hatua hii ilitoa fursa ya kuajiri watumishi wapya wenye sifa wapatao 74,173. Vilevile, kufuatia hatua tulizochukua, tuliwapandisha vyeo watumishi 306,917 na kulipa madeni ya watumishi ya mishahara na yasiyo ya mishahara yenye thamani ya shilingi bilioni 472.6 (ya kimshahara shilingi bilioni 114.5 na yasiyo ya kimshahara shilingi bilioni 358.1). Waheshimiwa Wabunge, tulifanya haya kwa lengo kulinda heshima ya wafanyakazi na kuleta nidhamu kwenye utumishi wa umma.
Sambamba na kuimarisha nidhamu Serikalini, tulizidisha mapambano dhidi ya rushwa, uhujumu uchumi na ufisadi. Utakumbuka kuwa, wakati nikizindua Bunge hili niliahidi kuanzisha Mahakama ya Uhujumu Uchumi. Mahakama hiyo ilianzishwa mwaka 2016 na mpaka sasa imepokea mashauri 407, ambapo mashauri 385 tayari yamesikilizwa. Zaidi ya hapo, katika kupambana na adui rushwa, Taasisi yetu ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeweza kufungua mashauri 2,256; ambapo mashauri 1,926 tayari yametolewa uamuzi, na Serikali imepata ushindi kwenye mashauri 1,013.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita pia TAKUKURU imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 273.38, zikiwemo fedha walizokuwa wamedhulumiwa wakulima. Aidha, TAKUKURU imetaifisha fedha taslim shilingi milioni 899, Dola za Marekani 1,191,651, EURO 4,301,399, nyumba 8 zenye thamani ya shilingi bilioni 11.6, magari matano yenye thamani ya shilingi milioni 126 pamoja na viwanja vitano (5). Aidha, tumeweza kurejesha mali za Serikali zilizochukuliwa na watu binafsi ama taasisi kinyume cha sheria, zikiwemo nyumba na majengo 98 (ikiwemo Mbeya Hotel), mashamba 23, viwanja 298, kampuni 3, maghala 69. Vile vile, kiasi cha fedha na mali zilizowekewa zuio kusubiria kukamilika kwa taratibu za kisheria za utaifishaji ni shilingi bilioni 52.7; Dola za Marekani milioni 55.8; Euro milioni 4.3, magari 75, nyumba 41; viwanja 47 na mashamba 13.
Hii, bila shaka, inaonesha dhamira yetu isiyo na mashaka ya kupambana na rushwa na ufisadi. Naupongeza Muhimili wa Mahakama, TAKUKURU, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi pamoja na wananchi kwa ujumla kwa kufanikisha mapambano haya. Lakini, nitumie fursa hii pia kuipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kufanikiwa kudhibiti na kuvunja mitandao ya biashara hiyo haramu hapa nchini. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, jumla ya tani 97.99 za bangi, tani 85.84 za mirungi, kilo 567.96 za heroin na kilo 23.383 za cocaine zimekamatwa pamoja na watuhumiwa 37,104. Hatua hizi ndizo zilifanya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), mwaka jana, kuipongeza nchi yetu kwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kwa asilimia 90. Lakini niseme, mafanikio haya yasingepatikana kama pasingekuwa na Sheria nzuri zilizopitishwa na Bunge hili. Hivyo basi, nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri mliyoifanya. Nawashukuru pia Watanzania kwa ushirikiano waliotoa katika kukabiliana na biashara hii haramu.
Mheshimiwa Spika;
Wakati nikizindua Bunge hili, nilieleza kwa kirefu sana kuhusu kutoridhishwa kwangu na hali ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Hivyo basi, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumejitahidi kushughulikia suala hilo, kwa kusimamia uadilifu kwa watumishi waliopewa dhamana ya kukusanya mapato, kuimarisha sheria za kodi, mifumo ya TEHAMA, kupanua wigo wa walipa kodi, kupunguza misamaha na kuziba mianya ya ukwepaji kodi, n.k.
Kutokana na hatua hizo, ukusanyaji wa mapato umeimarika. Mathalan, ukusanyaji wa mapato ya kodi kwa mwezi umeongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 mwaka 2015 hadi shilingi trilioni 1.3 hivi sasa; na mwezi Disemba 2019, TRA ilikusanya shilingi trilioni 1.987, kiwango ambacho ni cha juu kabisa kuwahi kukusanywa kwenye historia ya nchi yetu. Kwa upande wa mapato yasiyo ya kodi, nayo yameongezeka kutoka chini ya shilingi bilioni 688.7 mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi trilioni 2.4 mwaka 2018/2019. Halikadhalika, mapato ya ndani ya Halmashauri yameongezeka kutoka shilingi bilioni 402.66 Mwaka 2015/2016 hadi shilingi bilioni 661 Mwaka wa Fedha 2018/2019. Hii imefanya mapato ya ndani kwa ujumla, kuongezeka kutoka shilingi trilioni 11.0 mwaka 2014/2015 hadi shilingi trilioni 18.5 Mwaka wa Fedha 2018/2019.
Sambamba na kuongeza ukusanyaji wa mapato, tumedhibiti matumizi ya fedha za Serikali kwa kuzuia au kupunguza safari za nje zisizo za lazima, semina, warsha, makongamano, matamasha na udanganyifu kwenye manunuzi. Aidha, tulipitia upya muundo wa Serikali ili kuongeza ufanisi na kubana matumizi yasiyo ya lazima. Katika zoezi hilo, tuliweza kupunguza idadi ya wizara kutoka 29 hadi 22; na pia kuunganisha taasisi, idara na vitengo mbalimbali. Vilevile, tumepitia miundo ya wizara, taasisi na idara zinazojitegemea 116 na kufanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 17.4. Tumeunganisha pia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoka mitano kuwa miwili kwa lengo hilo hilo la kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji. Mabadiliko yote haya yalifanyika baada ya kupata baraka za Bunge hili Tukufu. Hivyo basi, nina haki kabisa ya kusema “ahsanteni sana Waheshimiwa Wabunge”. Bila ya ninyi, haya yote yasingefanyika.
Mheshimiwa Spika;
Kwa sababu ya kuongezeka kwa mapato na kudhibiti matumizi, Serikali iliweza kuongeza bajeti ya maendeleo kutoka wastani wa asilimia 26 hadi asilimia 40. Hii ndiyo imetuwezesha kuboresha huduma mbalimbali za jamii na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo. Kwa upande wa huduma za jamii, tumepanua wigo na kuboresha upatikanaji wa huduma za elimu, afya pamoja na maji. Kwenye elimu, kama unavyofahamu, tulianza kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ambapo mpaka mwezi Februari 2020 tulikuwa tumetumia shilingi trilioni 1.01 kugharamia.
Lakini, mbali na kutoa elimu bure, tumeongeza idadi ya shule za msingi kutoka 16,899 mwaka 2015 hadi 17,804 mwaka huu; na shule za sekondari kutoka 4,708 mwaka 2015 hadi shule 5,330 mwaka 2020. Vilevile, tumekarabati shule kongwe za sekondari 73 kati ya 89, tumejenga mabweni 253 na vyumba vya maabara ya 227. Aidha, tumetoa vifaa kwenye maabara zipatazo 2,956 na tumepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa madawati, ambapo idadi yake imeongezeka kutoka madawati 3,024,311 mwaka 2015 hadi kufikia 8,095,207; sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 200.
Kwa upande wa Vyuo vya Ualimu, tumekarabati vyuo 18, tumejenga upya vyuo viwili (Murutunguru na Kabanga) na halikadhalika tumepeleka kompyuta 1,550 kwenye vyuo vyote 35 vya ualimu kwa lengo la kuimarisha ufundishaji wa masomo ya TEHAMA. Kuhusu ngazi nyingine za elimu, tumeongeza Vyuo vya Ufundi (VETA) kutoka 672 mwaka 2015 hadi 712 mwaka 2020; na pia tumekarabati na kuboresha vifaa na miundombinu ya kufundishia katika vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi (FDC). Vilevile, tumejenga hosteli, kumbi za mihadhari, mabwalo ya chakula na maktaba kwenye vyuo vikuu. Tumeongeza pia bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 348.7 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 450 mwaka huu wa Fedha 2019/2020.
Kutokana na hatua hizo, uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza umeongozeka maradufu kutoka wastani wa wanafunzi milioni 1 mwaka 2015 hadi kufikia milioni 1.6 hivi sasa. Aidha, idadi ya wanafunzi wa kidato cha I – IV imeongezeka kutoka 1,648,359 mwaka 2015 hadi 2,185,037. Idadi ya wanafunzi wa VETA imeongezeka kutoka 117,067 mwaka 2015 hadi 226,767 mwaka 2020; na idadi ya wanafunzi wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) imeongezeka kutoka 6,693 mwaka 2016/17 hadi 9,736 mwaka 2018/19. Kwa upande wa vyuo vikuu, idadi ya wanafunzi wanaojiunga mwaka wa kwanza imeongezeka kutoka 65,064 mwaka 2015 hadi 87,813 mwaka 2020; na wenye kupata mikopo wameongezeka kutoka 98,300 mwaka 2014/2015 hadi 130,883 mwaka 2019/2020. Kwa taarifa hii Waheshimiwa Wabunge, naamini nitakuwa sijakosea nikisema, kazi kubwa imefanyika kwenye sekta ya elimu.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa sekta ya afya, tumeongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya 1,769, zikiwemo zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 71, hospitali za mikoa 10, ikiwemo Hospitali ya Mkoa wa Mara, (Mwalimu Nyerere Memorial Hospital) ambayo ujenzi wake ulikwama tangu miaka ya 1970. Vilevile, tumejenga hospitali za rufaa za kanda 3. Hii imefanya vituo vya kutolea huduma za afya kuongezeka kutoka 7,014 mwaka 2015 hadi kufikia 8,783 hivi sasa.
Zaidi ya hapo, tumeajiri watumishi wapya wa afya wapatao 14,479, wakiwemo madaktari wapya 1,000 tuliowaajiri hivi karibuni. Hii imeongeza idadi ya watumishi wa afya nchini kutoka 86,152 mwaka 2015 hadi 100,631 mwaka 2020. Tumeimarisha pia upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, ambapo tuliongeza bajeti yake kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 270 hivi sasa; na pia tumenunua na kusambaza magari ya kubeba wagonjwa (Ambulances) 117. Vilevile, tumefanikiwa kusomesha madaktari bingwa 301 ambao wamewezesha kuimarisha matibabu ya kibingwa nchini, hususan kwa magonjwa ya moyo, masikio, figo, mifupa, ubongo, kansa, n.k.
Kutokana na hatua hizo, idadi ya akinamama wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kutoka asilimia 64 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 83 hivi sasa; vifo vya watoto wachanga (wenye chini ya siku 28) vimepungua kutoka wastani wa vifo 25 hadi vifo 7 kwa kila vizazi hai 1,000; na idadi ya rufaa za kwenda nje ya nchi zimepungua kwa asilimia 95. Aidha, kutokana na kuimarishwa kwa matibabu ya kibingwa, baadhi ya wagonjwa kutoka mataifa jirani wameanza kuja kutibiwa nchini, hususan magonjwa ya moyo. Hii inadhihirisha kuwa, tumefanya kazi kubwa sana katika kuboresha na kuimarisha sekta ya afya nchini. Ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi.
Kuhusu maji, tumetekeleza miradi ya maji 1,423, ambapo miradi 1,268 ni ya vijijini na 155 ni ya mijini. Miongoni mwa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa ni wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Nzega, Tabora na Igunga; Mradi wa Maji wa Arusha pamoja na mradi wa kupeleka maji kwenye miji 28 unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi trilioni 1.2. Miradi mingine ya maji ilielezwa vizuri kwenye Hotuba ya Waziri wa Maji wakati wa kuwasilisha Bajeti. Na kutokana na jitihada zilizofanyika, upatikanaji wa majisafi na salama vijijini umeongezeka kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 70.1 mwaka 2020; na kwa mijini kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 84 mwaka 2020.
Tumeimarisha pia huduma za mawasiliano, hususan kwa kuboresha usikivu wa simu kutoka asilimia 79 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 94 mwezi Disemba 2019. Aidha, idadi ya watumiaji wa simu za mkononi pamoja na watumiaji data imeongezeka maradufu. Na hali hiyo imechangiwa zaidi na kupungua kwa gharama za kupiga simu kwa dakika moja kutoka shilingi 267 mwaka 2015 hadi shilingi 40 tu hivi sasa.
Sambamba na hayo, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kufufua Shirika letu la Simu (TTCL) ambalo lilikuwa limekufa pamoja na kuongeza hisa zetu kwenye Kampuni ya Airtel kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49. Huu ni ushahidi mwingine kwamba kazi tuliyotumwa na Watanzania tumeifanya kikamilifu.
Mheshimiwa Spika;
Mbali na kuboresha huduma za jamii, tumetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hususan katika ujenzi, uchukuzi na nishati ya umeme. Tumekamilisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa takriban kilometa 3,500 na hivyo kuifanya nchi yetu iwe na kilometa 12,964 za barabara za lami. Barabara nyingine zenye urefu wa zaidi ya kilometa 2,000 zinaendelea kujengwa. Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tumejenga barabara za juu (flyover na interchange) Dar es Salaam ili kupunguza tatizo la msongamano wa magari na pia tumekamilisha ujenzi wa madaraja makubwa 13, likiwepo Daraja la Nyerere – Kigamboni, Daraja la Magufuli katika Mto Kilombero pamoja na Daraja la Sibiti; na wakati huo huo ujenzi wa madaraja mengine makubwa unaendelea, likiwemo Daraja la Kigongo - Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2, Daraja la Salender lenye urefu wa kilometa 1.03 pamoja na Daraja la Wami lenye urefu wa meta 513.5.
Kwa ujumla, katika Awamu hii, hakuna Mkoa au Wilaya ambayo haikupatiwa fedha za kujenga barabara za lami. Makao Makuu ya Mikoa na Wilaya karibu zote sasa yanameremeta kwa lami na taa za barabarani. Na ahadi yetu ya kuunganisha Mikoa kwa barabara za lami nayo imetekelezwa kwa asilimia kubwa; na kwa Mikoa ya Rukwa-Katavi, Katavi-Tabora, Singida-Tabora, Tabora-Kigoma na Kigoma-Kagera nayo inaendelea kuunganishwa. Mathalan, barabara ya Mpanda – Tabora kilometa 359 wakandarasi wanne wanaendelea kujenga kwa kiwango cha lami; na barabara ya Manyoni – Tabora inakamilishwa kujengwa kwa lami. Vilevile, barabara ya kutoka Mpanda kwenda Kigoma na Kigoma hadi Nyakanazi zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hakika, kazi kubwa imefanyika.
Sambamba na kujenga barabara, tunakamilisha Awamu ya Kwanza ya ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa kilometa 300 na ujenzi wa Awamu ya Pili kutoka Morogoro hadi Makutupora umbali wa kilometa 422 umefikia asilimia 30. Miradi hii miwili inagharimu shilingi trilioni 7.062. Ujenzi wa sehemu ya Mwanza – Isaka – Dodoma ipo kwenye maandalizi. Tumekarabati pia reli ya zamani kutoka Dar es Salaam hadi Isaka kilometa 970 na halikadhalika tumefufua usafiri wa reli ya Dar es Salaam –Tanga – Moshi - Arusha, ambao ulisimama kwa takriban miaka 20. Lakini, katika kipindi cha miaka mitano, tumefanikiwa kurudisha tena usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga, Moshi hadi Arusha. Huu ni uthibitisho kuwa kazi kubwa imefanyika.
Kwa upande wa usafiri wa maji, hivi sasa tunafanya upanuzi wa Bandari zetu kuu za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga. Vilevile, tumeboresha usafiri wa maji kwenye Maziwa yetu Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa kuboresha bandari zake pamoja na kujenga na kukarabati meli. Kwenye Ziwa Victoria tumekarabati meli tano za Mv. Victoria, Mv. Butiama, Mv. Clarias, Mv. Umoja na Mv. Wimbi; na tunaendelea na ujenzi wa meli mpya kubwa ya “Mv. Mwanza, Hapa Kazi tu” itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo. Kwenye Ziwa Victoria pia tumejenga Chelezo kubwa kuliko zote kwenye Ziwa Victoria ili kujenga na kukarabati meli.
Kwa upande wa Ziwa Tanganyika, tumekarabati meli ya mafuta ya MT. Sangara na tupo mbioni kuanza ukarabati wa MV Liemba. Kwenye Ziwa Nyasa tumejenga meli mpya ya kubeba abiria 200 na mizigo tani 200. Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba wenzetu kule Zanzibar wamenunua meli kubwa mbili kwa ajili ya kutoa huduma katika Bahari ya Hindi. Aidha, mipango ya kujenga meli mpya kwa ajili ya kutoa huduma kati ya Bandari ya Mtwara na Comoro na kati ya Bandari ya Kalema na karemi nchini DRC, nayo inaendelea. Sambamba na hayo, tumejenga vivuko vipya na kukarabati vivuko vya zamani vipatavyo 17.
Kuhusu usafiri wa anga, tumekamilisha ujenzi wa Jengo jipya la Abiria (Terminal III) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere na tunaendelea na upanuzi wa Viwanja vya Kimataifa vya Kilimanjaro (KIA) na Abeid Aman Karume kule Zanzibar. Vilevile, ujenzi wa viwanja vingine 11 upo katika hatua mbalimbali, na tupo mbioni kumpata Mkandarasi wa kujenga Uwanja wa Kimataifa wa Msalato hapa Dodoma.
Tumekamilisha pia ujenzi rada Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza; na kule Songwe/Mbeya ujenzi wake unakaribia kukamilika. Sambamba na hilo, tumefufua Shirika letu la Ndege (ATCL) kwa kununua ndege mpya 11, ambapo 8 tayari zimewasili. Hii imeongeza idadi ya wasafiri wa anga nchini kutoka milioni 4.8 mwaka 2015 hadi milioni 5.8 mwaka 2018. Na faida nyingine ya kuwa na ndege tumeiona katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa corona, ambapo kwa kutumia ndege zetu tumeweza kuwarejesha Watanzania wenzetu waliokwama nchi mbalimbali, ikiwemo India. Kama tusingekuwa na ndege zetu, ingekuwa vigumu kuwarejesha Watanzania hao.
Ukiachilia mbali uimarishaji wa miundombinu ya usafiri, tumeboresha upatikanaji wa nishati ya umeme. Tumekamilisha Mradi wa Kinyerezi II, ambao umetuongezea Megawati 240; na tunakaribia kukamilisha upanuzi wa mtambo wa Kinyerezi I utakaozalisha Megawati 325 kutoka Megawati 150 za sasa. Muhimu zaidi, tumeanza kutekeleza Mradi mkubwa wa Bwawa la Nyerere kwenye Bonde la Mto Rufiji. Mradi huu unagharimu shilingi trilioni 6.5 na utakapokamilika utazalisha umeme Megawati 2115, ambazo sio tu zitatuhakikishia umeme wa kutosha na wa gharama nafuu lakini pia utatusaidia kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi makubwa ya kuni na mkaa. Tunaendelea pia kutekeleza miradi mingine kwa kutumia vyanzo mbalimbali, ikiwemo maji, gesi asilia, jua, upepo, n.k. Aidha, tumekamilisha miradi mikubwa ya kusafirisha umeme, ikiwemo Mradi wa Iringa – Shinyanga; Makambako – Songea; Lindi – Mtwara; n.k.; pamoja na kuendelea kutekeleza Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini, ambapo tumeongeza idadi ya vijiji vilivyofikishiwa umeme kutoka 2,018 mwaka 2015 hadi vijiji 9,112 mwezi Aprili 2020. Nchi yetu ina vijiji 12,268; hivyo tumebakisha vijiji 3,156 tu kufikisha umeme kwenye vijiji vyote nchini.
Kutokana na hatua tulizochukua, idadi ya watumiaji wa umeme (energy access) imeongezeka kutoka asilimia 35 hadi asilimia 85. Na hii imechagizwa na ushushaji wa gharama za kuunganisha umeme kutoka shilingi 177,000 hadi shilingi 27,000. Mafanikio mengine tuliyoyapata kwenye sekta ya nishati ni kupunguza tatizo la kukatikakatika kwa umeme. Katika kipindi chote cha miaka mitano nchi yetu haikuwahi kuingia gizani. Zaidi ya hapo, tumeokoa kiasi kikubwa cha fedha kwa kuzima mitambo ya kuzalisha umeme wa mafuta. Kwa mfano, kwa kuzima mitambo ya IPTL, Aggreko na Symbion tumeokoa shilingi bilioni 719 kwa mwaka. Hii ndiyo imesaidia TANESCO sasa ianze kujiendesha yenyewe.
Mheshimiwa Spika;
Wakati nikizindua Bunge hili, nakumbuka niliahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ingeendeleza jitihada za Awamu zilizotangulia za kukuza uchumi pamoja na kukabiliana na matatizo ya umasikini na ukosefu wa ajira. Hivyo basi, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumejitahidi kutekeleza ahadi hiyo; hususan kwa kukuza sekta zetu kuu za uchumi na uzalishaji, ikiwemo viwanda, kilimo, biashara, madini pamoja na utalii. Kuhusu viwanda, tumejenga viwanda vipya 8,477, ambapo vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406, na vidogo sana 4,410. Hii imeongeza idadi ya viwanda nchini kutoka 52,633 mwaka 2015 hadi viwanda 61,110 mwaka 2020. Viwanda vipya vilivyojengwa vimeisaidia kuifanya nchi yetu kujitosheleza kwa baadhi ya bidhaa, ikiwemo saruji, nondo na bati. Aidha, viwanda vipya vimezalisha ajira 482,601.
Sambamba na kujenga viwanda, tumeendelea kuweka mkazo kwenye sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji. Kama unavyofahamu, sekta hii bado ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu. Inachangia takriban asilimia 25 ya fedha za kigeni, asilimia 30 ya Pato la Taifa, asilimia 65 ya malighafi za viwandani, asilimia 70 ya ajira zote nchini na asilimia 100 ya mahitaji yetu ya chakula.
Hivyo basi, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tumeendelea kuipa kipaumbele sekta hiyo. Tumeongeza upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo (mbegu bora, mbolea, viatilifu, matrekta), tumeongeza uzalishaji wa miche ya mazao ya kimkakati, tumejenga na kukarabati skimu za umwagiliaji, vihenge vya kuhifadhi mazao, tumetafuta masoko na kuviimarisha vyama vya ushirika. Vilevile, tumeongeza maeneo ya ufugaji kutoka hekta milioni 1.4 mwaka 2015 hadi hekta milioni 5 mwaka 2020 na hivyo kusaidia kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Tumejenga pia majosho mapya 104; tumeongeza idadi ya ng’ombe waliohamilishwa kutoka 105,000 mwaka 2015 hadi 514,700 mwaka 2020, tumetoa chanjo ya mifugo na kusambaza dawa za kuogeshea mifugo.
Tumeimarisha pia ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi kwa kuanzisha Kanda Kuu tatu: Ziwa Victoria, Tanganyika na Pwani; pamoja na kudhibiti matumizi ya zana haramu. (Nakumbuka kuna wakati Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Mhe. Mpina alikuwa akitembea na rula hadi kwenye migahawa). Zaidi ya hapo, tumehamasisha na kufanikiwa kuongeza idadi wafugaji samaki kutoka 18,843 mwaka 2015 hadi 26,474 mwaka 2020; tumeongeza idadi ya mabwawa kutoka 22,545 hadi 26,445; vizimba vya kufugia samaki (fish cages) kutoka 109 hadi 431; na uzalishaji wa vifaranga kutoka 8,090,000 hadi 14,531,487.
Sambamba na hayo, mwaka 2017, tulizindua Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP – II) wenye malengo wa kukifanya kilimo chetu kuwa cha kisasa, cha kibiashara na chenye tija. Vilevile, tumeiongezea mtaji Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) wa shilingi bilioni 208 kupitia mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika. Serikali pia imeipatia TADB Dola za Marekani milioni 25.0 (sawa na shilingi bilioni 57.8) ili kuendesha Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (SCGS) wenye lengo la kuchagiza mabenki na taasisi za fedha kuongeza utoaji wa mikopo kwa wakulima wadogo na makampuni madogo na ya kati ya kilimo (SMEs). Hii ina maana kuwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imeipa TADB shilingi bilioni 324.8 na hivyo kuiwezesha Benki hiyo kutoa mikopo ya moja kwa moja kwa wakulima, wafugaji na wavuvi yenye thamani ya shilingi bilioni 166.9 kwa riba nafuu.
Kutokana na hatua hizi, mafanikio makubwa yamepatikana. Mathalan, uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 15,528,820 mwaka 2015/2016 hadi tani 16,891,974 mwaka 2018/2019. Mahitaji yetu ya chakula kwa mwaka ni chini ya tani milioni 14. Kwa upande wa mazao ya biashara, uzalishaji umeongezeka kutoka tani 796,502 hadi tani 1,144,1631. Kwenye uvuvi, sangara kwenye Ziwa Victoria wameongezeka kutoka tani 417,936 mwaka 2016 hadi tani 816,964 mwaka 2020, na urefu wa sangara umeongezeka kutoka wastani wa sentimeta 16 hadi sentimeta 25.2. Vilevile, mauzo ya samaki wetu nje ya nchi yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 379 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 692 mwaka 2019. Haya sio mambo madogo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa lengo la kukuza uchumi pia tumeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ikiwemo kuanza kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini (Blueprint) na kuanzisha Wizara Maalum ya Uwekezaji iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tumefanya marekebisho ya sheria mbalimbali na kupunguza urasimu katika kutoa vibali na pia kufuta tozo kero 173 ambapo tozo 114 zinahusu sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo; tozo 54 za sekta nyingine mbalimbali; na tozo 5 zilikuwa zinatozwa na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa Kazi.
Kutokana na hatua hizo, mafanikio makubwa yamepatikana kwenye nyanja za biashara na uwekezaji. Biashara yetu ya nje imeongezeka kutoka shilingi trilioni 11.5 mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi trilioni 16.6 mwaka 2018/2019. Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba, Tanzania imekuwa na urari chanya wa mauzo ya bidhaa kwenye masoko ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Mfano, kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kutoka mwaka 2015 hadi mwaka 2018, Tanzania imekuwa na urari chanya wa mauzo ya bidhaa kwa wastani wa Dola za Marekani milioni 288.04. Kuhusu uwekezaji, Kituo chetu cha Uwekezaji kimesajili miradi mipya 1,307 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 14.607, zaidi ya shilingi trilioni 30, na itakapokamilika itatoa ajira 183,503.
Mheshimiwa Spika;
Kwenye sekta ya madini, mageuzi makubwa sana yamefanyika, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Wizara mahsusi ya Madini, kudhibiti utoroshaji na usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi, kuanzisha masoko ya madini kwenye kila Mkoa, kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wetu wadogo kwenye mnyororo wa uchumi wa madini na kuwafutia ama kuwapunguzia viwango vya kodi. Zaidi ya hapo na muhimu zaidi, mwezi Julai 2017, tulipitisha Sheria ya Kulinda Rasilimali za Taifa (The Natural Wealth and Resources – Permanent Sovereignty - Act 2017), ikiwemo madini. Nakushukuru sana wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupitisha Sheria hii muhimu sana kwa Taifa letu. Kwa hakika, mmeingia kwenye vitabu vya historia vya nchi yetu na naamini vizazi hadi vizazi vitawakumbuka.
Kupitishwa kwa Sheria hiyo ndiko kumewezesha kwa mara ya kwanza Watanzania kumiliki rasilimali zao kwa nguvu za kisheria. Na Sheria hiyo pia ndiyo imefanikisha kuanzishwa kwa Kampuni ya Twiga Minerals Company, ambayo Serikali yetu inamiliki hisa asilimia 16 na Kampuni ya Barrick asilimia 84 ya Hisa, na halikadhalika kutolewa kwa malipo ya fidia ya Dola za Marekani milioni 100 kati ya Dola za Marekani 300 ambazo Kampuni ya Barrick ilikubali kutulipa kufuatia majadiliano tuliyofanya. Napenda pia nikushukuru wewe, Mheshimiwa Spika, kwa Kuunda Kamati Maalum ya Bunge ya Kuchunguza Utoroshaji wa Madini ya Tanzanite, ambayo ilitoa ushauri wa kujenga Ukuta wa kilometa 25 katika Mgodi wa Mirerani, ambao Serikali iliutekeleza.
Kutokana na hatua mbalimbali tulizochukua, sekta ya madini sasa imeanza kukua kwa kasi kubwa, ambapo mwaka jana (2019) iliongoza kwa ukuaji (kwa asilimia 17.7), ikifuatiwa na ujenzi asilimia 14.1. Aidha, mapato yatokanayo na madini nayo yameongezeka. Mathalan, kwenye mwaka wa Fedha 2018/2019 zilikusanywa shilingi bilioni 346 kutoka shilingi bilioni 194 mwaka 2016/2017. Kwenye Mwaka huu wa fedha (2019/2020) tunatarajia tukusanye shilingi bilioni 470, ambapo mwezi Aprili 2020 pekee, licha ya kuwepo kwa tatizo la ugonjwa wa corona, tumekusanya shilingi bilioni 58. Haijawahi kutokea. Kiwango cha juu kabisa tulichowahi kukikusanya kwa mwezi ilikuwa shilingi bilioni 43.
Mafanikio mengine tuliyoyapa kwenye sekta ya madini ni kutolewa kwa leseni 221 za uchenjuaji madini, leseni 4 za uyeyushaji madini (smelting) na leseni 4 za usafishaji madini (refining). Vilevile, tumetenga hekta 38,567 kwa ajili ya uchimbaji mdogo na kuwapatia mafunzo wachimbaji wadogo 10,338. Kwa ujumla, hivi sasa wachimbaji wadogo hawabughudhiwi. Mtakumbuka, zamani wachimbaji wadogo waliendesha shughuli zao kama wakimbizi. Sisi tukasema, hatutaki kuona wananchi wetu wakiwa wakimbizi ndani ya Taifa lao. Na kweli, kwa hatua tulizochukua, tumeweza kujenga heshima kwa wananchi kwa kuwawezesha kutengeneza maisha yao bila bugudha.
Kuhusu utalii, tumechukua hatua mbalimbali za kukuza sekta hiyo ikiwemo kuanza kutekeleza Mpango wa Uendelezaji Utalii Nyanda za Kusini, kuanzisha hifadhi mpya 5 (Hifadhi ya Nyerere, Chato – Burigi, Ibanda-Kyerwa, na Rumanyika-Karagwe) na kuongeza jitihada za kutangaza vivutio tulivyonavyo kimataifa, ikiwemo kuanzisha Chaneli Maalum ya Utalii ya Televisheni ya Taifa. Aidha, kama tulivyoahidi, tumezidisha mapambano dhidi ya ujangili kwa kuanzisha Jeshi Usu na hivyo kusaidia kuongezeka kwa idadi ya wanyama waliokuwa kwenye hatari ya kutoweka kama vile faru na tembo. Mathalan, idadi ya faru imeongezeka kutoka 162 mwaka 2015 hadi 190 mwaka 2019; na tembo wameongezeka kutoka 43,330 mwaka 2014 hadi 51,299 mwaka 2019.
Kufuatia hatua hizo, idadi ya watalii na mapato yameongezeka. Kwa mfano, mwaka 2019 tulipokea watalii 1,510,151 kutoka watalii 1,137,182 mwaka 2015. Aidha, mapato yaliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2019. Kama isingekuwa tatizo la kuibuka kwa janga la korona, naamini mwaka huu pia idadi ya watalii na mapato yake yangeongezeka.
Sekta nyingine, ambayo haijasemwa sana lakini kwa sasa ina mchango mkubwa kwenye uchumi wetu ni sanaa na utamaduni. Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2018, shughuli za Sanaa na Burudani ziliongoza kwa ukuaji mwaka 2018 ambapo ilikua kwa asilimia 13.7 na mwaka 2019 ilishika nafasi ya tatu kwa ukuaji wa asilimia 11.2. Hongereni sana wasanii wetu mbalimbali, hususan wa Bongo Fleva na Filamu. Kazi zenu sio tu zinaburudisha na kuchangia ukuaji uchumi, lakini pia zinaitangaza nchi yetu kimataifa. Na katika hilo, naipongeza Timu yetu Taifa ya Soka, ambayo baada ya takriban miaka 39 kupita, hatimaye mwaka jana (2019) ilifanikiwa kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Afrika. Nawapongeza pia wanamichezo wengine waliopeperusha vyema bendera yetu katika miaka mitano iliyopita, hususan katika ndondi na riadha. Mheshimiwa Spika, kutokana na mchango mkubwa unatolewa na wasanii na wanamichezo nchini, Serikali imejipanga, katika miaka mitano ijayo, kuweka mkazo mkubwa zaidi kwenye sekta hii ambayo imewaajiri vijana wetu wengi.
Sekta nyingine tulizoshughulikia na kutoa mchango kwenye ukuaji uchumi ni ulinzi, sayansi na teknolojia, habari, misitu, ufugaji nyuki, mazingira; n.k. Kwenye ulinzi, mathalan, tumeviimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi, Polisi, Idara ya Usalama, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto, TAKUKURU na Mamlaka ya Kudhibiti Madawa Kulevya, kwa kuvipatia vifaa na zana za kisasa). Kwa upande wa sayansi na teknolojia, tumeanzisha vituo mahiri vya mafunzo kwa taasisi za elimu ili kuzalisha vijana wenye uwezo unaohitajika Kitaifa, Kikanda na Kimataifa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 75. Taasisi hizo ni: Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam itakayobobea katika TEHAMA na Taasisi ya Teknolojia Mwanza itakayobobea kwenye masuala ya Ngozi), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kitakachobobea katika taaluma za anga na Chuo cha Ufundi Arusha kitabobea katika nishati. Kwa sababu ya ufinyu wa muda sitoweza kuzielezea sekta zote. Itoshe tu kusema, Serikali imejitahidi kuimarisha sekta zote ili kukuza uchumi nchini.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na hatua tulizochukua za kuimarisha sekta mbalimbali, uchumi wa nchi yetu umeendelea kukua vizuri, ambapo kwa wastani, katika miaka mitano iliyopita, umekua kwa asilimia 6.9 kutoka ukuaji wa asilimia 6.2 mwaka 2015. Pato ghafi la Taifa limeongezeka kutoka shilingi trilioni 94.349 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 139.9 mwaka 2019; kwa bei ya miaka husika (yaani current prices). Hii sio tu imetufanya tuwe miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi lakini imeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 zenye uchumi mkubwa zaidi Barani Afrika.
Tumefanikiwa pia kudhibiti mfumuko wa bei, kutoka asilimia 6.1 mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa asilimia 4.4. Sambamba na hilo, akiba ya fedha ya kigeni imeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 4.4 zilizokuwa zikitosheleza kununua bidhaa na huduma kwa miezi 4.3 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 5.3 mwezi Aprili, 2020 ambazo zinatowezesha kununua bidhaa na huduma kwa miezi 6.2. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo lililowekwa kwenye EAC (miezi 4.5) na SADC (miezi 6).
Kwa upande wa mapambano dhidi ya umasikini, umasikini wa kipato umepungua hadi kufikia asilimia 26.4 mwaka 2017/2018. Na kwa lengo la kuendelea kupambana na umaskini, mwezi Februari 2020, tumezindua Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF III), ambao utagharimu shilingi trilioni 2.032. Kuhusu kukabiliana na tatizo la ajira, kupitia jitihada zilizofanyika, ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, tumefanikiwa kutengeneza ajira zipatazo 6,032,299. Kati ya ajira hizo, 1,975,723 zimezalishwa na sekta rasmi na ajira 4,056,576 zimezalishwa na sekta isiyo rasmi.
Mheshimiwa Spika;
Mafanikio mengine tumeyapata kwenye nyanja za sheria na utoaji haki. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumejitahidi kupunguza vitendo vya rushwa, ucheleweshaji na ubambikaji kesi, pamoja na tatizo la mlundikano wa wafungwa. Mathalan, ili kukabiliana na tatizo la ucheleweshaji wa kesi, Serikali iliteua Majaji wapya 17 wa Mahakama ya Rufani, Majaji 52 wa Mahakama Kuu na kuajiri watumishi wa mahakama 859, wakiwemo mahakimu 396. Aidha, tumejenga Mahakama Kuu mpya 2 (Mara na Kigoma); na kukarabati nyingine nne Dar es Salaam, Mbeya, Shinyanga na Sumbawanga. Tumejenga pia Mahakama za Hakimu Mkazi 5, za Wilaya 15 pamoja na Mahakama za Mwanzo 18, na halikadhalika tumeanzisha Mahakama ya Kutembea (mobile court), ambayo imeanza kufanya kazi kwenye Mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza na mpaka mwezi Machi 2020 ilishasajili mashauri 337 na kusikiliza mashauri 274. Naipongeza Mahakama kwa kuchukua hatua za kupunguza mrundikano wa kesi, ikiwemo kuimarisha matumizi ya TEHAMA ambayo sio tu imeharakisha uendeshaji wa mashauri lakini pia imepunguza tatizo la rushwa kwa watumishi wa Mahakama.
Vilevile, katika jitihada za kukabiliana na tatizo la ucheleweshaji kesi, nilisaini Hati ya kuiimarisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na pia kuanzisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Uwekaji saini Hati hiyo umeongeza tija na kuleta ufanisi mkubwa katika usimamizi na uendeshaji wa mashauri Mahakamani na pia kwenye Mabaraza ya Usuluhishi ndani na nje ya nchi. Zaidi ya hapo, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumewasamehe wafungwa 42,774 waliokuwa wakitumikia vifungo mbalimbali na hivyo kupunguza mlundikano magerezani. Aidha, katika zoezi la ukaguzi na kusikiliza changamoto za wafungwa na mahabusu, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imewafutia kesi mahabusu 2,812.
Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi, Waheshimiwa Majaji wengine, Mahakimu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuimarisha mfumo wa utoaji haki nchini.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumeshughulikia pia kero mbalimbali za wananchi, hususan wakulima, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara, wafanyakazi, wajasiliamali; na bila kusahau migogoro ya ardhi. Kwa upande wa wakulima, wavuvi, wafugaji na wafanyabiashara; kama nilivyosema awali, tumefuta takriban tozo 114 zilizokuwa zikikwamisha shughuli zao. Kwa wafanyakazi, tayari nimeshaeleza kuhusu upandishaji vyeo na malipo ya madeni mbalimbali. Zaidi ya hapo, tumepunguza kodi ya mapato kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9 na kulipa deni la shilingi trilioni 1.2 ambalo Serikali ilikuwa ikidaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii; na hivyo kuwezesha wastaafu kuendelea kulipwa mafao yao.
Kwa upande wa wajasiliamali wadogo, wakiwemo machinga, mama lishe, waendesha bodaboda na bajaji, tumejitahidi kuwawekea utaratibu mzuri wa kuendesha shughuli bila ya kubughudhiwa kwa kuwapatia vitambulisho maalum vilivyotolewa kwa gharama nafuu. Mwaka jana (2019) jumla ya wajasiliamali wadogo 1,591,085 walipatiwa vitambulisho na hivyo kuwafanya waondokane na usumbufu uliokuwepo. Mtakumbuka, zamani, kabla ya utaratibu huo kuanza, wajasiliamali wadogo walikuwa wakibugudhiwa sana na mgambo, ikiwemo kunyang’anywa mali zao. Hivyo, kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa vitambulisho hivyo, tumedhihirisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo kwa ajili ya wanyonge.
Sambamba na kutoa vitambulisho kwa wajasiliamali wadogo, tumetunga Sheria yenye kuzitaka halmashauri zote kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake (asilimia 4), vijana (asilimia 4) na wenye ulemavu (asilimia 2), ambapo hadi mwezi Machi kiasi cha shilingi bilioni 93.2 kilikuwa kimetolewa.
Kero nyingine tuliyoshughulikia ni ya migogoro ya ardhi. Baadhi ya hatua tulizochukua ni kuanzisha Ofisi za Ardhi kwenye Mikoa yote, ambapo sasa huduma zote za upangaji, upimaji, umilikishaji, utathmini pamoja na usajili wa hati, nyaraka, ramani na michoro zinapatikana. Hii imeongeza kasi ya urasimishaji makazi ya wananchi na pia utoaji hati. Jumla ya maeneo ya viwanja yaliyorasimishwa ni 764,158 na tumetoa hatimiliki za kimila 515,474. Kubwa zaidi, ni uamuzi uliofanywa na Serikali wa kuvirasimisha vijiji 920 kati ya 975 vilivyokuwa kwenye maeneo ya hifadhi.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumeimarisha pia uhusiano na ushirikiano na mataifa ya nje pamoja na taasisi za kimataifa. Hii ndiyo sababu tuliweza kuwapokea viongozi wa nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa, ikiwemo Vietnam, India, uturuki, Afrika Kusini, DRC, Ethiopia, Misri, Rwanda, Zambia, Zimbabwe, Uganda, IMF, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, IFAD, n.k.
Katika kipindi hicho pia tumefungua Balozi mpya 8 (Algeria, Cuba, Israel, Korea, Qatar, Namibia, Sudan na Uturuki). Aidha, nchi mbili, Ethiopia na Poland, nazo zimefungua Balozi zao hapa nchini. Sambamba na hayo, tumeendelea kushiriki katika shughuli na mipango mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo ulinzi wa amani, ambapo kwa sasa tuna askari wapatao 2,303 katika nchi za DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Sudan na Sudan Kusini. Zaidi ya hapo, nchi yetu imeaminiwa kuongoza jumuiya mbili za kikanda, Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanzia 2016 hadi 2017 na pia kuongoza SADC kuanzia Agosti 2019 hadi mwezi Agosti 2020 tutakapokabidhi. Na moja ya mafanikio tuliyoyapata katika kuongoza taasisi hizo, ni kuzishawishi Nchi Wanachama kuridhia lugha ya Kiswahili kutumika kwenye Taasisi hizo.
Mheshimiwa Spika;
Katika Ibara 151 (c) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020, Chama Cha Mapinduzi kiliahidi, nanukuu “kusimamia azma ya Serikali ya kuhakikisha majengo yote ya Wizara za Serikali yanajengwa Dodoma badala ya Dar es Salaam”, mwisho wa kunukuu. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa ahadi hiyo tumeitekeleza. Sio tu kwamba majengo ya Wizara zote yamejengwa Dodoma, bali Serikali yote tayari imehamia, ambapo tarehe 13 Aprili, 2019 nilizindua Mji wa Serikali pale Mtumba. Hii ina maana kuwa tumetekeleza ahadi yetu zaidi ya tulivyoahidi. Nina imani, kwa kutekeleza ndoto hiyo iliyodumu kwa miaka 47, sio tu tumemuenzi Baba wa Taifa lakini pia Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu TANU waliofikia uamuzi ya kuhamishia Makao Makuu ya nchi Dodoma mwaka 1973. Hivyo, naamini, Mheshimiwa Spika utanisemehe nikisema “CCM Oyee”. Hapo nilikuwa nachomekea tu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kifupi sana, haya ni baadhi tu ya mafanikio tuliyoyapata. Lakini, kama nilivyosema awali, tumefanya mengi, ambayo kama ningeamua kuyaeleze yote hapa, tunaweza kukesha. Kwa bahati nzuri, Watanzania wengi wameona na wanayajua. Hivyo basi, nina imani wataendelea kutuamini na kutupa dhamana ya kuongoza nchi yetu katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Na binafsi naamini, kutokana na misingi imara tuliyoiweka ya ukuaji uchumi pamoja na uzoefu mkubwa tulioupata, endapo wananchi wataendelea kutuamini na kutuchagua kuongoza nchi yetu katika miaka mitano ijayo, tutafanya mambo mengine makubwa zaidi na hatimaye kufanikiwa kutimiza ndoto na dhamira yetu ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wenye kuongozwa na viwanda pamoja na huduma za kiuchumi (economic services) ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, zilijitokeza baadhi ya changamoto. Kama ujuavyo, hapa dunia sio rahisi kufanya jambo lisikumbane na changamoto ama vikwazo. Hivyo basi, sisi pia, katika miaka hii mitano, tumekumbana na changamoto/vikwazo mbalimbali; lakini kikubwa zaidi ni kuibuka kwa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona.
Napenda nitumie fursa hii kulishukuru Bunge hili Tukufu kwa kupitisha Azimio la kunipongeza; japo ukweli ni kwamba pongezi hizi zinatustahili Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na Bunge hili. Pamoja na hofu kubwa iliyokuwa imetawala, Bunge hili liliendelea na vikao vyake kama kawaida kwa lengo la kuwatumikia Watanzania; ingawa nafahamu wapo wachache walikimbia. Lakini niseme tu kwamba, kukimbia haikuwa jambo sahihi kwa sababu matatizo au changamoto hazikimbiwi. Kukimbia matatizo au changamoto ni ishara ya udhaifu, ni ishara ya woga lakini pia ni ishara ya kutojiamini. Siku zote njia sahihi ya kukabiliana na matatizo ni kukabiliana nayo.
Na hii ndiyo sababu sisi, tuliamua kukabiliana na ugonjwa wa corona, huku tukiwa tumemtanguliza Mwenyezi Mungu. Na tunashukuru, kwa kufanya hivyo, tumeweza mpaka sasa, kwa kiasi kikubwa, sio tu kufanikiwa kuushinda ugonjwa huo lakini pia kupunguza athari zake, zikiwemo athari za kiuchumi. Kama mnavyofahamu, Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha Dunia, yamebashiri kwamba asilimia 60 ya nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Janga la Sahara zitashuhudia ukuaji hasi wa uchumi mwaka huu (2020). Hata hivyo, sisi Tanzania, kutokana na hatua tulizochukua, uchumi wetu unatarajiwa kuendelea kukua vizuri kwa asilimia 5.5. Zaidi ya hapo, tumeweza kulinda ajira za wananchi wetu, tuna uhakika wa usalama wa chakula na pia tumeweza kuendelea na utekelezaji wa miradi yetu mikubwa ya kimkakati. Na hii inadhihirisha kuwa maamuzi yetu yalikuwa sahihi na maamuzi ya Bunge hili kuendelea na vikao nayo yalikuwa sahihi sana. Hongera sana Mheshimiwa Spika na hongereni sana Waheshimiwa Wabunge.
Nitumie fursa hii, kwa mara nyingine tena, kurudia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuliepusha Taifa letu dhidi ya ugonjwa wa corona. Nawashukuru pia viongozi wa dini pamoja na madhehebu mbalimbali kwa kuitikia wito wa Serikali wa kufanya maombi maalum ya kumwomba Mwenyezi Mungu kutuepusha na Janga la Corona. Dua na maombi yao yamedhihirisha kuwa penye hakuna linaloshindikana. Namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja wajumbe wote wa Kamati ya Kitaifa ya kukabiliana na ugonjwa wa corona. Kwa namna ya pekee, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa kufanya kazi kwa ujasiri mkubwa sana. Vilevile, navishukuru vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na madaktari na wauguzi wetu kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya na wanaoendelea kuifanya ya kuwahudumia wagonjwa wa corona.
Na kutokana na hali ya ugonjwa wa corona nchini kuendelea vizuri, napenda kutumia fursa hii kutangaza kuwa, kuanzia tarehe 29 Juni, 2020 shule zote kuanzia za awali, zifunguliwe na pia shughuli nyingine zote ambazo tulizizuia nazo zifunguliwe. Maisha ni lazima yarudi kama ilivyokuwa zamani. Hata hivyo, naendelea kuwasihi Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari na pia kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalam wetu wa afya.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge;
Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu napenda nirudie kuwashukuru Watanzania wote, wa makundi yote, wakiwemo wakulima, wafanyakazi, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara; kwa kuiunga mkono Serikali yetu, hususan kwa kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa bidii, kulipa kodi; lakini pia kwa kuwa tayari kufunga mkanda ili kuijenga Tanzania mpya. Nawashukuru pia viongozi wenzangu wote wa Serikali tulioshirikiana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Namshukuru Makamu wa Rais, Mwanamama shupavu na jasiri, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kunisaidia majukumu; Namshukuru Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa ushauri na ushirikiano alionipa; namshukuru na kumpongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa heshima na unyenyekevu wake, uchapaji kazi wake mzuri na kutanguliza mbele maslahi ya taifa. Kwa hakika, amenisaidia sana. Aidha, namshukuru Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi, Mheshimiwa Balozi John Kijazi, kwa kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka. Vilevile, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kufanya kazi bila kuchoka. Nawashukuru pia Makatibu Wakuu; Wakuu wa Mikoa; Makatibu Tawala wa Mikoa; Wakuu wa Wilaya; Makatibu Tawala wa Wilaya; Wakurugenzi wa Wilaya, Manispaa na Majiji; Maafisa Tarafa; Watendaji wa Kata na Vijiji, Mabalozi wa nyumba kumi pamoja na watumishi wote wa Serikali kwa kufanikisha kupatikana kwa mafanikio yote niliyoyataja. Kwa ujumla wao, wote wamenisaidia sana kwenye kufanya kazi. Nawashukuru sana.
Natambua kuwa Mhe. Rais Dkt. Shein anamaliza muhula wake kwa mujibu wa Katiba. Hivyo, napenda kutumia fursa hii kumpongeza kwa utumishi uliotukuka akiwa Makamu wa Rais kwa miaka nane na Rais wa Zanzibar kwa miaka kumi. Mhe. Rais Dkt. Shein ameweka historia ya namna yake katika utumishi wa umma na ametoa mchango mkubwa kwenye Taifa letu. Hivyo basi, sasa anapokwenda kupumzika, namtakia kila la heri na tumwahidi kuendelea kumuenzi kama tunavyowaenzi viongozi wengine wastaafu.
Nakishukuru pia Chama changu, CCM, kwa kuisimamia vizuri Serikali na kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 inatekelezwa. Usimamizi mzuri uliofanywa na CCM kwa Serikali katika miaka hii mitano umedhihirisha maneno yaliyowahi kutamkwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwamba “Chama legelege huzaa Serikali legelege na Chama kikiwa imara, Serikali nayo huwa imara”.
Navishukuru pia vyama vingine vya siasa ambavyo vilitoa ushirikiano kwa Serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kama mnavyofahamu, wapo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ambao, licha ya tofauti zetu za kiitikadi, walikuwa pamoja na Serikali wakati wote. Na hivyo kusema kweli ndivyo inapaswa kuwa. Sisi sote ni wamoja na tunajenga Taifa moja. Aidha, ninawashukuru wana-habari kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kuhabarisha na kuelimisha umma wa Tanzania pamoja na dunia nzima kwa ujumla kuhusu masuala mbalimbali ya nchi yetu, hususan mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii tuliyoyapata katika kipindi hiki.
Kwa mara nyingine, narudia kulishukuru Bunge hili kwa ushirikiano mkubwa iliotoa kwa Serikali katika kipindi cha miaka mitano. Mbali na kuishauri na kuisimamia Serikali, Bunge hili ndilo lilikuwa likipitisha bajeti na miswada mbalimbali ya sheria iliyoiwezesha Serikali kutimiza majukumu yake kwa ufanisi. Kwa namna ya pekee kabisa, nawashukuru Wabunge wa Chama changu, Cha Mapinduzi, kwa kuiunga mkono Serikali yetu. Kusema kweli mmedhihirisha ule usemi usemao “uchungu wa mwana aujuaye mzazi”.
Nawashukuru pia wabunge wa vyama vingine kwa ushirikiano wao; japo walikuwepo baadhi ambao wenyewe kila jambo walikuwa wakipinga. Lakini nao tunawashukuru. Naamini, wakati ujao watakuwa wamejifunza kwamba kupinga pinga kila kitu sio vizuri.
Napenda pia nitumie fursa hii kuwashukuru washirika na wadau wetu mbalimbali wa maendeleo kwa ushirikiano mkubwa walitupatia. Ushirikiano wao ulitupa nguvu na ari ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Hivyo basi, tunawashukuru sana washirika wetu wa maendeleo, ambao kwa bahati nzuri, wiki iliyopita, Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Serikali aliwataja. Na nimefurahi baadhi ya Waheshimiwa Mabalozi na washirika wetu wa maendeleo tupo nao hapa leo. Ahsanteni sana.
Mwisho lakini sio kwa umuhimu, namshukuru sana Mke wangu, Janet, na pia niwasihi muendelee kumwombea Mama yangu ambaye anaendelea kupambana na ugonjwa wa kiharusi kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Mheshimiwa Spika;
Mwanzoni mwa hotuba yangu, nilieleza kuwa, nimekuja kulihutubia Bunge hili la 11 kwa mara ya mwisho ili kuruhusu kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwezi Oktoba 2020. Nyote mnfahamu, uchaguzi ni zoezi muhimu katika kukuza demokrasia katika nchi. Mbali na kuwapa wananchi fursa ya kuwachagua viongozi wawatakao, inatoa nafasi kwa viongozi kujua endapo bado wanaaminiwa na wananchi.
Na katika hilo, natambua kuwa baadhi yenu hapa mmeonesha nia ya kuwania tena na wapo waliotangaza kutowania tena. Nawatakia maisha mema wale waliotangaza kustaafu na nawatakia kila la kheri wale wanaowania tena. Naamini wengi wenu, hususan wale wenye kuvaa nguo za kijani, watarejea; lakini kwa wale ambao hawatabahatika kurejea, tunawashukuru kwa mchango wao kwenye Bunge hili.
Kwa upande wa Serikali, tumejipanga kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu, kama ilivyokuwa chaguzi zilizopita, unakuwa huru na haki. Kwa sababu hiyo, navisihi vyama vya siasa na wanasiasa kujiandaa vizuri kushiriki katika Uchaguzi huo. Navihimiza pia vyama kutoa fursa za kutosha kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu; aidha, na nawasihi wagombea kuepuka matusi na vurugu. Kama nilivyosema, sisi sote ni wamoja. Hivyo, tubishane kwa hoja kwa kushindanisha Ilani zetu. Lakini niseme, kwa yeyote atakayetaka kuleta vurugu, namtahadharisha kwamba Serikali ipo macho. Uchaguzi haumaanishi kuwa Serikali inaenda kulala. Serikali itaendelea kuwepo kusimamia sheria na taratibu za nchi.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tumepata mafanikio mengi makubwa. Na mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano ulikuweko miongoni mwa Watanzania wote. Hivyo, hatuna budi kuendelea kushirikiano kwa lengo la kuiletea maendeleo nchi yetu. Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara nyingi, “Sisi Watanzania Tukiamua, Tunaweza”. F
Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa Bunge hili litavunjwa rasmi kwa tarehe itakayotangazwa kwenye gazeti la Serikali.
Mungu Libariki Bunge la Tanzania!
Mungu Wabariki Wabunge Wote!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza’
No comments:
Post a Comment