Matokeo chanyA+ online




Monday, June 29, 2020

‘WALIOKACHA’ KUCHUKUA HATI ZA ARDHI KUANZA KUDAIWA KODI JULAI MOSI


Na Munir Shemweta, WANMM NJOMBE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema kuanzi Julai Mosi mwaka huu wananchi wote wasiochukua hati za ardhi huku maeneo yao yakiwa yamepimwa na michoro yake kuidhinishwa wataanza kudaiwa kodi ya pango la ardhi.

Hatua hiyo inafuatia Bunge la kumi na moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Sheria inayomtaka mwananchi aliyepimiwa ardhi na michoro kuidhinishwa kuchukua hati katika kipindi kisichozidi siku tisini na asipofanya hivyo ataanza kudaiwa kodi ya ardhi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikata utepe kuzindua rasmi Ofisi ya Ardhi mkoa wa Njombe jana. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Lucy Msafiri, wa tatu kulia ni katibu Tawala mkoa wa Njombe Catarina Revocatu na kulia ni Kamishna Msaidzi wa Ardhi mkoa wa Njombe Christopher  Mwamasage.

Akizungumza na wananchi mkoani Njombe jana wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya ardhi ya mkoa  huo, Naibu Waziri Mabula alisema, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wamiliki wa ardhi  kukwepa kuchukua hati za ardhi wakati taratibu zote zikiwa zimekamilika ikiwemo  kuidhinishwa michoro na kuwekewa alama za mawe.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi hati yake ya ardhi mkazi wa Njombe Naomi Msafiri wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi  mkoa wa Njombe jana. kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Lucy Msafiri.

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, kuanzia Julai Mosi mwaka huu muarobaini kwa wamiliki wasiotaka kuchukua hati za ardhi umefika kwa kuwa atakayeshindwa kuchukua hati atalazimika kudaiwa kodi kuanzia pale michoro yake ilipoidhinshwa.

‘’Kuanzia leo wamiliki wa ardhi hapa Njombe ambao wamepimiwa na michoro yao kuidhinishwa waende halmashauri za wilaya kurekebisha kumbukumbu zao na baada ya hapo asiyerekebisha baada ya siku tisini tunaanza kumdai’’ alisema Dkt Mabula


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Ramani ya Tanzania pamoja na ile ya mkoa wa Njombe Mkuu wa wilaya ya Njombe Lucy Msafiri wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi  mkoa wa Njombe jana.

Aliwaagiza maafisa ardhi katika halmashauri za wilaya kuhakikisha kuanzia Julai mosi wanawapelekea hati ya madai wale wote waliopimiwa na michoro kuidhinishwa ili waanze kulipa kodi ya pango la ardhi.

Alisema, pamoja na wananchi wakiwemo wa Njombe kufurahia usogezwaji huduma za sekta ya ardhi karibu lakini ni lazima wawajibike kwa kulipa kodi ya ardhi na kupatiwa hati aliyoieleza kuwa inaongeza thamani ya ardhi sambamba na hati miliki yake kutumika katika shughuli za kiuchumi.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya majalada katika ofisi ya ardhi mkoa wa Njombe jana wakati wa uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa huo.wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Lucy Msafiri na kulia ni  Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Njombe Christopher Mwamasage.

Aidha, amezitaka ofisi za ardhi katika halmashauri zote nchini kutoa elimu kwa wananachi wa maeneo yao kuhusiana na umuhimu wa kuchukua hati ili kujua takwa la kisheria hasa ikizingatiwa wengi wao wameshindwa kuchukua hati kwa sababu mbalimbali.

Akiegeukia uchukuaji hati za ardhi kwa mkoa wa Njombe, Dkt Mabula alisema mkoa huo una jumla ya hati 42,516 zilizoidhinishwa lakini kati ya hizo ni hati 11,246 tu ndizo wamiliki wake walijitokeza kuzichukua huku wamiliki 31,270 wakiwa hawajachukua.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia Kabati za kutunzia nyaraka za ardhi katika ofisi ya ardhi mkoa wa Njombe jana wakati wa uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa huo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Lucy Msafiri.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe Lucy Msafiri aliyemuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Njombe katika hafla ya uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa alisema, uanzishwaji ofisi za ardhi katika mkoa wa Njombe utaondoa changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika masuala ya ardhi kwenye mkoa huo.

Mkuu huyo wa wilaya ya Njombe alibainisha kuwa, mkoa wa Njombe ni maarufu kwa kilimo cha Miti, Chai, Mahindi, Viazi na Parachichi na baadhi ya wamiliki wa mashamba hayo hawana hati miliki za ardhi hivyo uanzishwaji ofisi hizo unafungua milango kwa wamiliki wa mashamba  kumilikishwa kwa haraka.


Kamishna Msaidizi wa ardhi kutoka Makao Makuu ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wilson Ruge akisoma taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu wake wakati wa uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa wa Njombe jana. (PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE WA WIZARA YA ARDHI)


Naye Kamishna Msaidizi wa ardhi Wilson Ruge ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo, alisema uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa ni moja ya mikakati iliyopewa kipaumbele na serikali ya awamu ya tano katika kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kubainisha kuwa tayari kazi kubwa imefanyika ikiwemo usambazaji vifaa na kuwataka wananchi kujitokeza kumilikishwa ardhi zao.

No comments:

Post a Comment