Matokeo chanyA+ online




Friday, July 17, 2020

PROF. MCHEMBE AWATAKA WAFAMASIA KUSIMAMIA MAADILI



Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Mabula Mchembe akiongea na wafamasia na wadau wa mnyororo wa ugavi na usambazaji wa bidhaa za afya (hawapo pichani) wakati akifungua kikao kinachoendelea mkoani Morogoro. 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amewataka Wafamasia nchini kote kuzingatia maadili na kutumia taaluma waliyonayo ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Prof. Mchembe amesema hayo wakati akifungua semina inayojumuisha Wadau wa mnyororo wa ugavi na usambazaji wa bidhaa za afya kutoka Sekta mbalimbali za Serikali na Binafsi waliokutana Mkoani Morogoro.

“Ninawataka Wafamasia wote mbadilike kulingana na mazingira yaliyopo, hivi sasa nchi imeingia kwenye uchumi wa kati, hii inamaana mboreshe utaalamu wenu ili kukidhi mahitaji ya nchi. Corona imekuja na faida kubwa, imetufanya sasa tunaweza kutengeneza Vitakasa mikono vyetu (Hand Sanitizer) na barakoa jambo ambalo hapo awali halikuwepo”. Amesema Katibu Mkuu Prof. Mchembe.
 
 
Mfamasia Mkuu Ndg. Daud Msasi akitolea ufafanuzi moja ya hoja wakati akiwasilisha mada katika kikao cha wafamasia na wadau wa mnyororo wa ugavi na usambazaji wa bidhaa za afya kinachoendelea Mkoani Morogoro.

Dkt. Mchembe amesisitiza kuboreshwa kwa huduma za dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya zikiwemo Zahanati na vituo vya afya vya umma kuhakikisha dawa zote muhimu zinapatikana ili mwananchi anapofika kupata huduma asikose dawa na kulazimika kwenda kununua kwenye maduka ya watu binafsi.

Aidha, Prof. Mchembe amewataka wataalamu hao kutochagua vituo vya kazi kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kuwa wanadidimiza taaluma yao kwa kufanya kazi maeneo ambayo hayana vifaa.

“Rais wetu ana nia njema katika kuboresha huduma za afya nchini, utakuta Hospitali fulani ina vifaa vizuri sana vya kufanyia kazi lakini haina wataalam wa kuvitumia”. Amesema Katibu Mkuu huyo.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Mabula Mchembe akiwa na Mtendaji Mkuu Wakala wa ununuzi Serikalini Prof. Geraldine wakifuatilia moja ya mada zilizokua zinawasilisha katika kikao cha wadau mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini.

Na WAJMW-MOROGORO

Katika kutatua changamoto hizo Katibu Mkuu Mchembe amemuagiza Mfamasia Mkuu wa Serikali Ndg. Daud Msasi kuweka muongozo mzuri katika kuwapangia vituo vya kazi Wafamasia na wataalam wengine ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya popote walipo.

Pia Prof. Mchembe amesisitiza matumizi ya data katika kutoa huduma na kutunza kumbukumbu kupitia mifumo ya GOTHOMIS na mingineyo ili kurahisisha utoaji wa huduma na kutunza rekodi za wagonjwa na pia kuweka mnyororo wa huduma zote za Hospitali kuwa katika hali nzuri.

Kwa upande wake Mfamasia Mkuu wa Serikali Ndg. Daud Msasi amewataka wadau waliohudhuria katika kikao hicho kuhakikisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya unatekelezwa ipasavyo kwa kuzingatia mambo ya msingi ambayo ni Pamoja na uzuiaji wa kukua kwa madeni yasiyolipika, nyaraka za mali za serikali zitunzwe vizuri, matumizi ya miongozo ili kuepika gharama zisizo za lazima, uwepo wa maduka ya dawa yanayojiendesha bila kuathiri huduma nyingine Pamoja na kuweka taarifa zilizo sahihi.

No comments:

Post a Comment